Furaha, tabasamu zisizoisha na historia ya kipekee ndivyo ilivyokuwa jana Mei 4, 2026, wakati watoto tisa waliozaliwa kwa mpigo na kuweka rekodi duniani walipotimiza miaka mitano.

Familia ya Arby Halima na Oumar Cissé iliadhimisha tukio la kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa watoto wao ikiwa ni safari iliyojawa na simulizi ya kila aina tangu kuzaliwa kwao.

Watoto hao wa kiume wanne na wasichana watano wanatajwa kuwa kundi la kwanza duniani la watoto tisa waliozaliwa kwa mpigo na wote kuendelea kuishi baada ya kuzaliwa, kwa mujibu wa rekodi za Guinness World Records.

Watoto hao ni Mohammed VI, Oumar, Elhadji na Bah kwa upande wa wavulana, huku wasichana wakiwa ni Kadidia, Fatouma, Hawa, Adama na Oumou.

Watoto hao walizaliwa nchini Morocco kwa njia ya upasuaji wakiwa na umri wa wiki 30, kila mmoja akiwa na uzito wa kati ya kilo 1.1 hadi 2.2.

Kwa mujibu wa taarifa, baada ya kuzaliwa familia hiyo ilibaki Morocco kwa miezi 19 katika makazi maalumu yenye huduma za uuguzi ili kuwahudumia watoto hao kabla ya kurejea nchini mwao Mali.

Akizungumza na jarida la People, Cissé amesema watoto hao waliopatikana kwa njia ya kawaida bila msaada wa kitabibu maalum wanaendelea vizuri wakiwa nyumbani.

“Watoto wote wanaendelea vizuri kama familia,” amesema.

Familia ya Arby Halima na Oumar Cissé wakiwa katika picha ya pamoja na watoto wao tisa. Picha na Mtandao

Hata hivyo, ameeleza kuwa moja ya changamoto kubwa anazokabiliana nazo ni namna watoto hao watakavyojiingiza katika jamii kadri wanavyokua. Amesema familia inaandaa mipango ya kuwapeleka shule ili kuanza hatua ya elimu.

Kwa upande wake, baba wa watoto hao, Abdelkader Arby, alinukuliwa na BBC mwaka 2022 akieleza kuwa watoto hao wana tabia tofauti tofauti.

“Wapo watulivu, wengine wanapiga kelele na kulia sana, na wengine hupenda kubebwa muda mwingi. Ni jambo la kawaida kabisa kuwa tofauti,” amesema.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, familia ilisherehekea nyumbani kwao Mali ambapo picha zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha watoto hao wakiwa wamemzunguka mama yao aliyeshikilia cheti cha Guinness.

Imeandikwa kwa msaada wa Mashirika

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *