WEKUNDU wa Msimbazi, Simba baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Yanga, wameendelea kuweka hai matumaini yao ya kupigania ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya leo Jumatano kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar.

Mfungaji wa bao hilo ni Clatous Chama ambaye Mei 3, 2026 uwanjani hapo alifanya kazi kubwa katika sare ya 2-2 dhidi ya Yanga akifunga bao la kideoni na kuasisti.

Katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania, Simba ilianza kwa presha ya juu, ikitengeneza mashambulizi ya mapema kupitia Clatous Chama, Elie Mpanzu na Libasse Guaye. 

Hata hivyo, JKT Tanzania ilionekana imara kiulinzi, ikiongozwa vyema na Karim Mfaume na Laurian Makame kabla ya kupata majeraha waliziba mianya muhimu hasa katika maeneo ya pembeni ambako Simba ilijaribu kupenyeza mara kwa mara.

Licha ya Simba kujaribu mbinu mbalimbali za kushambulia, JKT iliendelea kuwa makini na kuondoa hatari zote karibu na lango lao. 

Hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika, hakuna timu iliyopata bao. Simba ilikuwa na mashuti matano, mawili yakilenga lango na kupata kona nne, huku JKT ikiwa haijapiga shuti lililolenga goli.
Dakika ya 45+2 ilishuhudiwa JKT ikilazimika kufanya mabadiliko baada ya Makame kuumia, nafasi yake ikichukuliwa na Edson Katanga.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi kutoka kwa Simba, iliyoongeza mashambulizi na kuweka presha kubwa langoni mwa wapinzani wao.

Jitihada hizo zilizaa matunda dakika ya 52, ambapo Mpanzu alitoa pasi safi iliyomkuta Clatous Chama, naye akamalizia kwa utulivu na kuipa Simba bao pekee katika mchezo.

Bao hilo lilikuwa mwendelezo wa ubora wa Mpanzu na Chama, ikumbukwe wawili hao walihusika katika bao la pili la Simba wikiendi iliyopita katika sare ya 2-2 dhidi ya Yanga kwenye Dabi ya Kariakoo. Kwa Chama, hilo lilikuwa bao lake la tano msimu huu.

Baada ya kupata uongozi, Simba ilifanya mabadiliko ya kiufundi kwa kumtoa Libasse Gueye na kumuingiza Seleman Mwalimu kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji.

Baadaye, Alassane Kante alichukua nafasi ya Ino Loemba ili kuimarisha kiungo na kudhibiti mchezo.
JKT Tanzania walijaribu kuongeza kasi kusaka bao la kusawazisha lakini Simba ilionyesha nidhamu  katika kulinda na kudhibiti kila hatari.

Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 46 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara nyuma ya Yanga yenye pointi 51, huku Azam ikishika nafasi ya tatu na pointi 43, zote zikicheza mechi 21.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *