
Unguja. Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, imeomba kuidhinishiwa jumla ya Sh135.676 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27, huku ikiainisha mikakati ya kudhibiti mfumko wa bei na kuimarisha uchumi wa visiwa hivyo.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti leo Jumatano, Mei 6, 2026 katika mkutano wa tatu wa Baraza la 11 la Wawakilishi, unaofanyika Chukwani, Unguja, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kupunguza kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma.
Amesema miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kutoa bei elekezi na kusimamia kwa karibu bidhaa zinazoingia nchini, hasa bidhaa za chakula na vifaa vya ujenzi ili kulinda masilahi ya wananchi.
Katika kuimarisha upatikanaji wa bidhaa na kupunguza gharama, Serikali imepanga kuongeza ufanisi wa Bandari ya Malindi kwa kununua vifaa vya kisasa pamoja na kuboresha bandari nyingine ili kupunguza muda wa kushusha mizigo.
Aidha, maghala ya kuhifadhi chakula yataimarishwa sambamba na mifumo ya uhifadhi ili kuhakikisha usalama wa chakula nchini, huku ruzuku ikiendelea kutolewa na kusimamiwa ipasavyo.
Hemed amesema juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda, kasi ya mfumko wa bei imepungua kutoka wastani wa asilimia 5.1 mwaka 2024 hadi asilimia 4.1 mwaka 2025.
Amesema kushuka huko kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na kupungua kwa bei za vyakula na mfumko wa bei za chakula ulipungua hadi wastani wa asilimia 5.0 mwaka 2025 kutoka asilimia 8.4 mwaka 2024, kufuatia kuongezeka kwa uzalishaji wa ndani pamoja na udhibiti wa bei.
Hata hivyo, amesema mfumko wa bei kwa bidhaa zisizo za chakula umeongezeka kidogo na kufikia wastani wa asilimia 3.4 mwaka 2025 kutoka asilimia 2.7 mwaka 2024, hali iliyochangiwa na kupanda kwa bei katika soko la dunia pamoja na gharama za usafirishaji.
Serikali, kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeendelea kuchukua hatua za kudhibiti kushuka kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu za kigeni ili kulinda uchumi wa nchi.
Katika sekta ya uwekezaji, Hemed amesema Serikali imepanga kusajili miradi 110 yenye thamani ya Dola 620 milioni za Marekani, itakayotarajiwa kuzalisha ajira 2,100.
Ameeleza kuwa jitihada hizo zinaenda sambamba na kuimarisha mifumo ya kidijitali na mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.
Ametoa wito kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uwekezaji, akisisitiza kuwa Serikali imeweka mazingira rafiki, salama na yenye ushirikiano kwa wawekezaji wote.
Kwa upande wa ajira, Serikali imethibitisha mikataba 11,613 ya wafanyakazi, idadi inayozidi makadirio ya mikataba 10,500.
Aidha, vibali vya kazi 2,877 vimetolewa kwa wataalamu wa kigeni kutoka nchi mbalimbali ili kusaidia kukuza ujuzi na tija katika sekta mbalimbali.
Kuhusu mwenendo wa uchumi, amesema uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.5 mwaka 2026, ukichangiwa na ongezeko la watalii kwa asilimia 9.3, kutoka watalii 917,167 mwaka 2025 hadi zaidi ya milioni moja mwaka 2026.
Serikali pia imeendelea kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), ambapo miradi mipya 22 imepitiwa na saba kati yake tayari imesainiwa.
Miradi hiyo ni pamoja na ile ya bandari na miundombinu mingine muhimu inayochangia ukuaji wa uchumi.
Katika kukuza sekta ya utalii, Serikali imefanikiwa kuongeza idadi ya watalii kwa asilimia 24.5 mwaka 2025 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
Aidha, muda wa kukaa kwa watalii umeongezeka, hatua inayosaidia kuongeza mapato ya Taifa.
Hemed pia amesisitiza umuhimu wa kuendeleza visiwa vidogo kwa uwekezaji wa kimkakati, baadhi ya visiwa tayari vimeanza kuvutia wawekezaji na miradi ya maendeleo inaendelea.
Akihitimisha, amesema amani na utulivu ni msingi wa maendeleo yoyote, akiwahimiza wananchi kuendelea kuilinda, hasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ili kuhakikisha mazingira bora ya utekelezaji wa mipango ya kiuchumi na kijamii.