Chanzo cha picha, Getty Images
Operesheni ya Marekani ya kusindikiza meli zilizokwama katika Mlango bahari wa Hormuz itasitishwa kwa “muda mfupi”, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza Jumanne jioni.
Trump alisema operesheni ya “Project Freedom”, iliyoanza siku chache zilizopita, itasimamishwa kwa “makubaliano ya pande zote” kwa sababu “maendeleo makubwa” yamepatikana kuelekea makubaliano na Iran.
Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilielezea hatua hiyo kama ushindi, vikidai kuwa Trump “alirudi nyuma” baada ya kushindwa mara kwa mara kufungua njia hiyo muhimu kwa usafirishaji wa kimataifa.
Tangazo la Trump lilikuja wakati Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, alisema kuwa operesheni ya awali ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, “Operation Epic Fury”, imekamilika baada ya kufikia malengo yake.
Katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema alifanya uamuzi huo “kutokana na ombi la Pakistan”, ambayo imekuwa mpatanishi kati ya Marekani na Iran. Hata hivyo, aliongeza kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya bandari za Iran vitaendelea.
Tangazo hilo linaweza kuwashangaza baadhi ya watu, kwani linapingana na kauli za awali za viongozi wa Marekani akiwemo Rubio, waziri wa ulinzi Pete Hegseth, na mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi Dan Caine, ambao walisisitiza kuwa operesheni hiyo ingeendelea kuhakikisha uhuru wa usafirishaji katika eneo hilo.
Rubio alisema: “Tunapendelea njia ya amani. Kile ambacho rais anapendelea ni kufikia makubaliano.”
Kwa sasa, hatua itakayofuata haijulikani wazi. Serikali ya Marekani ilikuwa imesisitiza kuwa “Project Freedom” ni kampeni tofauti na vikwazo vya kiuchumi, ambavyo vina lengo la kuishinikiza Iran.
Unaweza kusoma;
- ‘Viongozi wawili wenye kiburi waibua mtafaruku Hormuz, nini kitatokea?” – Uchambuzi
- Je, mpango wa “Bahari 4” wa Syria kuwa mbadala wa Hormuz?
- Tunachokijua kuhusu mradi wa Trump wa “Project Freedom” katika mlango bahari wa Hormuz