
Mamia ya wazazi katika mji wa Goma, wamelazimika kusitisha masomo ya watoto wao, kutokana na ukosefu wa fedha, ambao umesababishwa pakubwa na kutatizika kwa shughuli za kiuchumi na kufungwa kwa Benki, baada ya waasi wa M 23 kuanza kudhibiti mji huo mwaka uliopita.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Mama Fatuma, mzazi wa watoto wanne ambao wote wamekatiza masomo kutokana na umaskini unaoikabili familia yake, anasema hali imekuwa ngumu mno.
“sisi tunaona ni vema watoto wetu wasalie nyumbani badala yakuongeza usumbufu kwa waalimu kwa sababu hakuna pesa za malipo ya shule.Binafsi naona ni vema wasiende tena shuleni kutokana na majukumu ni mengi lakini hakuna pesa”. Amesema Mama Fatuma.
Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watoto 500 katika shule 10 zikiwemo za binafsi na hizo za umma wamekatiza masomo tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Umaskini umeongezeka zaidi mjini Goma kufuatia kukwama kwa shughuli za benki, na hivyo kuwanyima maelfu ya wakazi fursa ya kupata mikopo. Hali hii imesababisha matatizo makubwa ya kiuchumi katika mji huu wenye zaidi ya wakazi milioni moja.
Dady Saleh, mchumi kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, anasema kuwa licha ya kuanza kushuhudiwa utulivu katika baadhi ya maeneo ya Kivu Kaskazini, hali ya kiuchumi bado ni changamoto kubwa kwa familia nyingi.
“Unafahamu mwenyewe kwamba asilimia 80 ya wakongo wanaishi katika hali ya umaskini na kwa hiyo ikiwa unataka kukwamisha mendeleo ya nchi ni sharti ukwamishe elimu na hiyo ni hatari kabisa.” Amesema Dady Saleh.
Hata hivyo, uongozi wa AFC/M23 umeahidi kuweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha watoto hao wanaendelea na masomo yao licha ya mazingira magumu yanayozikabili familia nyingi mashariki mwa Kongo.
Benjamin Kasembe, Goma – RFI Kiswahili.