Shinyanga. Sakata la tozo ya Sh200,000 kwa wachimbaji wadogo katika Mgodi wa Mwakitolyo kwa kila gari linalotoka na mchanga au mawe, limeibuka katika Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, baada ya shughuli za uchimbaji kusitishwa.
Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya kata leo Jumatano, Mei 6, 2026, Diwani wa Mwakitolyo, Masalu Nyese amesema changamoto hiyo imesababisha kusimama kwa shughuli za uzalishaji kutokana na kutokuwepo kwa muafaka kati ya wachimbaji na halmashauri.
“Kwenye kata yangu bado kuna mgogoro wa tozo kwa wachimbaji ambao umesababisha shughuli za uzalishaji kukwama. Tunaomba suluhu ipatikane ili shughuli ziendelee na halmashauri ipate mapato,” amesema Nyese.
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa dhahabu katika mgodi wa Kigera Etuma wilayani Musoma wakiwa kwenye mkutano wa hadhara ambapo waliwasilisha kero zao kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi kwaajili ya utatuzi. Picha na Beldina Nyakeke
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Seth Msangwa amesema tayari timu maalumu imeundwa kufanya tathmini ya kina kuhusu suala hilo, huku akisisitiza kuwa changamoto hiyo imeathiri mapato ya halmashauri.
“Naomba madiwani tuwe na uvumilivu ili kuipa nafasi timu ya wataalamu iliyoundwa kufanya tathmini na kuja na suluhu ya kudumu,” amesema Msangwa.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Joseph Ntomela amesema uchunguzi unaendelea na baada ya kukamilika, mapendekezo yatawasilishwa kwa madiwani kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa dhahabu katika mgodi wa Kigera Etuma wilayani Musoma wakiwa kwenye mkutano wa hadhara ambapo waliwasilisha kero zao kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi kwaajili ya utatuzi. Picha na Beldina Nyakeke
Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga, Omary Mwenda amewapongeza madiwani kwa usimamizi wao na kuwataka kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na matumizi sahihi ya fedha za Serikali.
Chanzo cha mgogoro huo kinatajwa kuwa ni sheria ndogo ya halmashauri inayotoza Sh200,000 kwa kila gari linalobeba mchanga au mawe kutoka kwenye vitalu vya uchimbaji vinavyomilikiwa na vikundi vya wananchi, bila kuzingatia thamani halisi ya mzigo.