Moshi. Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Moshi, imeitupa rufaa iliyowasilishwa na mfanyabiashara anayemiliki vitega uchumi kadhaa ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro, Frank Marealle aliyoifungua dhidi ya mdogo wake, Ackley Marealle.

Katika hukumu ya rufaa hiyo iliyotolewa na Jaji Adrian Kilimo na kuwekwa katika mtandao wa Mahakama jana Jumatano, Mei 6, 2026,

Frank ambaye pia ni Mangi wa Wachaga wa Marangu, alifungua rufaa hiyo namba 12608 ya 2025, baada ya kushindwa katika shauri la mgogoro wa ardhi kugombea eneo lenye ukubwa wa hekari 2.12 lililopo Kijiji cha Lyamrakana huko Marangu.

Katika maombi hayo namba 51 ya 2020 yaliyokuwa yamefunguliwa Baraza la Ardhi na Nyumba Moshi, Frank aliomba mahakama imtaje ndiye mmiliki halali na itoe amri ya kuondolewa kwa mwili wa mama yake mdogo uliozikwa eneo hilo.

Kulingana na maombi hayo, Frank aliyekuwa akiwakilishwa katika baraza hilo na Wakili Modestus Njau, alitaka jeneza lenye mwili wa Veronica Mlang’a, liondolewe katika kaburi alimozikwa na akazikwe katika eneo lake la Pata huko huko Marangu.

Frank alijenga hoja kwamba yeye ndiye mmiliki halali wa ardhi ya shauri hilo, kwa sababu alimiliki kihalali kupitia marehemu mama yake aitwaye Asinath David Marealle, ambaye aliolewa akiwa ni mke wa nane wa marehemu Mangi David Marealle.

Kwamba, marehemu mama yake alimiliki ardhi hiyo tangu mwaka 1931 kwa mujibu wa sheria ya kimila ya Kichaga na kuendeleza sehemu hiyo ya ardhi kutoka 1931 baada ya ndoa yao ya kimila na Mangi David Marealle.

Alidai kuwa mwaka 1961, Mangi David Marealle ambaye alikuwa baba yake mzazi na pia baba wa Ackley, lakini kwa mama tofauti, aligawa ardhi hiyo kwa watoto wake wawili ambao ni Wilfred Marealle na Frank ambaye ni mkata rufaa.

Frank alidai kuwa baadaye Machi 8, 2020, mdogo wake ambaye alikuwa mjibu maombi katika shauri hilo, aliingilia eneo hilo na kumzika mama yake hivyo akaomba atangazwe ndiye mmiliki na Jeneza lenye mwili huo liondolewe.

Hata hivyo, Ackley katika majibu yake, alipinga hoja ya kaka yake na kueleza kuwa ardhi hiyo ilikuwa yake kihalali na ndio maana alimzika mama yake hapo, hivyo hajavamia eneo hilo na aliomba maombi hayo kutupiliwa mbali kwa kukosa sifa.

Alidai ardhi ilikuwa yake tangu marehemu mama yake, Veronica Mlang’a alipompa mwaka 1980 na kwamba, amekuwa akiishi katika ardhi hiyo kwa zaidi ya miaka 43 na kabla yake, mama yake ndio alilimiliki na alizikwa hapo.

Ushahidi wake huo ulithibitishwa na shahidi mmoja ambaye ni James Maro na baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama ilisema Frank alishindwa kuthibitisha kwa viwango vinavyokubalika, kuwa eneo ni mali yake.

Hata hivyo, Frank hakuridhishwa na uamuzi huo na maagizo ya mahakama, hivyo akakata rufaa akiomba hukumu nzima na amri ya mahakama ifutwe na kuwekwa kando na atangazwe ndiye mmiliki halali na Ackley aamriwe kuondoka eneo hilo.

Rufaa ilivyolirejesha shauri

Baada ya kusikiliza rufaa hiyo, Mahakama Kuu Moshi chini ya Jaji Lilian Mongella ilibatilisha mwenendo wa shauri hilo katika Baraza la Ardhi  kuanzia Machi 3, 2023 wakati agizo la kutembelea eneo lenye mgogoro ilipotolewa.

Mahakama Kuu pia ilibatilisha hukumu na amri na kuweka kando amri nyingine zote zilizotokana na hilo na kesi hiyo ilirejeshwa kwenye baraza kwa ajili ya kupitia upya maelekezi hayo na kuandika hukumu mpya kwa mwenyekiti mwingine.

Baada ya amri ya Mahakama ya Desemba 5, 2023, shauri hilo liliendelea, baraza liliyatupa tena maombi ya Frank kwamba alishindwa kuthibitisha madai yake kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa ardhi hiyo inayobishaniwa.

Baraza hilo lilitangaza kwamba, kwa kuwa ilithibitishwa katika ushahidi kuwa shamba hilo lilikuwa la marehemu Veronica ambaye alimpa Ackley, basi kitendo cha kumzika mama yake kwenye ardhi hiyo, haikuwa kuingilia eneo hilo.

Kama ilivyokuwa mwanzo, Frank Marealle hakuridhishwa na hukumu hiyo akaamua kukata rufaa tena Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Moshi, lakini mahakama imeitupa rufaa ya mfanyabiashara huyo mashuhuri nchini.

Katika sababu zake za rufaa, Frank alijenga hoja kuwa Mwenyekiti wa Mahakama ya Ardhi alikosea kisheria na ukweli, kwa kushikilia kuwa mmiliki halali ni Ackley bila kuzingatia ushahidi wa mashahidi wake waliounga mkono ushahidi wake.

Pia, alidai mwenyekiti alikosea kisheria kutamka kuwa mmiliki halali wa ardhi ya shauri ni Ackley bila kuzingatia kuwa yeye alitoa kielelezo P1 kama ushahidi wa umiliki wake wa ardhi hiyo na kwamba, hoja hiyo haikuamuliwa vyema.

Halikadhalika, alidai Mwenyekiti alikosea kisheria kwa kushindwa kurekodi, kutathmini na kuzingatia ushahidi hasa wa kesi ya marejeo ya Dk Wilfred Marealle dhidi ya Jamhuri wa Agosti 2, 1985 na hatimaye ilifika katika uamuzi mbaya.

Kwamba Mwenyekiti alikosea kisheria na ukweli kwa kuenyesha kwenye hukumu yake kuwa shahidi wa pili wa mdai, Dk Wilfred alikuwepo wakati mahakama ilipotembelea eneo lenye mgogoro wakati alikuwa ameaga dunia Machi 2024.

Mwenyekiti alikosea kisheria kwa kushikilia kuwa mmiliki halali wa ardhi hiyo ni Ackley bila kuzingatia ukweli na uamuzi wa familia katika baraza lililoitishwa Oktoba 7, 1980 na Mangi mkuu, Thomas Marealle.

Kwa upande wake, Wakili Semali alipangua hoja hizo na kudai mrufani alikuwa ameshindwa kuthibitisha kwa viwango vinavyokubalika katika kesi za madai kuwa alikuwa mmiliki halali na kwamba Ackley alilipata eneo hilo tangu mwaka 1980.

Akijibu hoja kuhusu kielelezo P1, wakili alisema kielelezo hicho ilikuwa tu nakala ya maombi ya umiliki wa ardhi hiyo na sio hati miliki na kwamba yalisitishwa kwa sababu mlalamikiwa alisimamishwa tayari kutambuliwa kama mmiliki.

Alisisitiza zaidi kuwa hakuna chama kilichotoa cheti cha umiliki, kwa hivyo kutegemewa kwa utoaji ulikosewa na uamuzi uliotajwa ulikuwa wa kutofautisha, usio na umuhimu na sio hakuna makubaliano au hati za manispaa zilizotolewa.

Hukumu ya Rufaa

Katika hukumu yake, Jaji Kilimi alisema baada ya kuzingatia rekodi za mahakama, sababu za rufaa na mawasilisho ya pande mbili, mahaka yake ina wajibu mmoja tu wa kuamua kama rufaa hiyo ina sifa (mashiko) ama haina mashiko.

Baada ya kupitia hukumu ya Baraza, Jaji alisema ana maoni kuwa mahakama ya ardhi haikutangaza mmiliki, badala yake ilisema kwamba mlalamikaji alishindwa kuthibitisha madai yake ya umiliki wa ardhi hiyo iliyokuwa na mgogoro.

“Kwa msingi wa ushahidi kwenye kumbukumbu, ingawa mrufani (Frank) alidai umiliki na madai ya kuendelea kuishi katika eneo hilo, lakini ushahidi mahakama ilipotembelea eneo hilo unazungumza tofauti na madai yake,” alisema Jaji.

“Hakuna ushahidi uliotolewa kuonyesha kwamba mlalamikaji aliishi au aliendelea kumiliki eneo hilo. Baada ya ziara ya mahakama iliona kuna nyumba mbili za mjibu rufaa, makaburi mawili, moja la Veronica na lingine la Joseph,” inasema hukumu.

“Badala yake alikuwa ni mama wa mjibu rufaa ambaye alimiliki ardhi hadi kifo chake na mjibu rufaa (Ackley) aliishi humo tangu kuzaliwa hadi sasa,” alisema Jaji.

“Kwa kuwa mrufani hakuthibitisha kama mjibu rufaa au mama yake walialikwa tu katika eneo hilo na ikizingatiwa wamekaa zaidi ya miaka 43 bila kusumbuliwa, kwa mtazamo wangu unaozingatiwa itakuwa si haki kuvuruga muda wao mrefu wa kuishi hapo na maendeleo yaliyofanywa humo kwa muda uliotajwa,” alisema.

“Kwa kuzingatia yale niliyoyaeleza, hitimisho langu la mwisho ni kwamba, mrufani aameshindwa kuthibitisha kesi kwenye mizani ya uwezekano unaohitajika katika kesi za madai”alisema Jaji Kilimi na kuongeza kusema kuwa:-

“Kwa mazingira hayo, sina sababu ya kutokubaliana na msimamo wa mahakama ya ardhi katika kesi hii ambao nashawishika nao na hapa naubariki. Kwa hiyo, ninaendelea kutupilia mbali rufaa na mrufani atalipa ghara za kesi,” alisisitiza

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *