Dar es Salaam. Mwalimu wa Jiografia katika Shule ya Sekondari Hai, mkoani Kilimanjaro, Geofrey Pascal Paul (39), ameibuka mshindi wa gari jipya aina ya Mazda CX-5 baada ya kushiriki katika promosheni ya Mwaka Umenyooka kupitia matumizi ya My Airtel Money App.

Ushindi huo umegeuza simulizi ya maisha yake ambayo kwa muda mrefu yaligubikwa na changamoto za kifedha, zikiwemo mikopo na majukumu ya kifamilia yaliyokuwa yakimtegemea mshahara wake wa ualimu.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa gari hilo Aprili 30, 2026, Paul alisema hakuwahi kufikiria kama angeweza kumiliki gari akiwa na makato mengi ya mikopo kwenye mshahara wake.

“Kwa hali ya makato kwenye salary slip yangu, sikuwahi kuona kama naweza kufikia ndoto ya kumiliki gari. Ndiyo maana nilipopigiwa simu mara ya kwanza nilidhani ni utani,” alisema.

Alieleza kuwa ushindi wake ulitokana na matumizi ya kawaida ya Airtel Money App katika shughuli zake za kila siku, ikiwemo kutuma fedha, kulipa bili na huduma nyingine.

“Nilituma Sh100,000 kwa baba yangu aliyekuwa mgonjwa kupitia Airtel Money App, muda mfupi baadaye nikapigiwa simu nikielezwa nimeshinda gari. Nilishangaa sana,” alisema.

Kwa upande wake, mke wake, Beatrice Geofrey, alisema ushindi huo umetimiza ndoto ya muda mrefu ya familia yao.

“Alikuwa akitamani kumiliki gari, lakini niliona kama ndoto kwa sababu ya majukumu mengi. Leo imekuwa kweli,” alisema.

Aliongeza kuwa familia yao imekuwa ikitumia huduma za Airtel kwa zaidi ya miaka 15 kutokana na urahisi na usalama wake.

Katika shule anapofundisha, ushindi huo umeibua furaha miongoni mwa walimu na uongozi. Mkuu wa Shule, Alex John Warioba, alisema mafanikio hayo ni chachu kwa wengine kuamini katika matumizi ya teknolojia ya kidigitali.

“Ni jambo la kujivunia kuona mwalimu wetu amefanikiwa kupitia huduma za kidigitali. Hii inahamasisha wengine,” alisema.

Aidha, alibainisha kuwa uwepo wa intaneti bila malipo katika baadhi ya shule wilayani humo kupitia mpango wa SmartWasomi umeboresha ufundishaji na ujifunzaji.

Kwa upande wa Airtel, Mkurugenzi wa Airtel Money, Andrew Lugamba, alisema ushindi huo ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha kidigitali nchini.

“Tunatimiza ahadi kwa wateja wetu. Ushindi huu unaonesha namna matumizi ya mara kwa mara ya Airtel Money App yanavyoweza kuleta manufaa makubwa,” alisema.

Aliongeza kuwa huduma hizo zinachochea ujumuishwaji wa kifedha kwa Watanzania, hasa katika maeneo ya vijijini ambako shughuli za kilimo na biashara ndogo ndogo zinategemewa zaidi.

Meneja wa Kanda wa Airtel, Faustine Mtui, alisema teknolojia imekuwa nyenzo muhimu katika kubadili maisha ya wananchi, akitolea mfano wakulima wanaopokea malipo yao kwa haraka kupitia simu.

“Hii ni hatua muhimu katika kuimarisha uchumi wa kidigitali na kurahisisha miamala kwa wananchi,” alisema.

Hafla ya makabidhiano ya gari hilo ilihitimisha tukio hilo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Airtel kuendeleza matumizi ya huduma za kifedha za kidigitali nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *