
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, Jumamosi hii ataanza ziara nyingine barani Afrika ziara inayolenga kufufua ushirika wa Ufaransa na bara hilo baada ya miaka kadhaa ya mvutano na mataifa ambayo Paris iliyatawala zamani.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Macron ataanzia nchini Kenya, ambapo siku ya Jumaratu yeye na mwenyeji wake rais wa Kenya, William Ruto, wameandaa mkutano wa Pamoja unaofahamika kama ‘Afrika Forward’, ukiwaleta Pamoja viongozi wa Afrika, wafanyabiashara, wakurugenzi na vijana.
Ni ziara ambayo anatarajiwa kuitumia kuacha urithi wake kwa bara hilo wakati huu akielekea kumaliza muhula wa pili wa utawala wake.
Rais Macron pia atatembelea nchi za Misri na Ethiopia ikiwa ni sehemu ya ziara yake barani Afrika.
Kwa mujibu wa ikulu ya Elysee, mkutano huu unatoa picha ya uhusiano we kipekee kati ya Afrika na Ufaransa, ambapo ajenda za kiuchumi, mazingira, maendeleo na biashara za kikanda zitajadiliwa.
Mkutano huu wa Nairobi utakuwa ni wa kwanza kufanyika kwenye nchi ya Afrika ambayo inazungumza kingereza.
Kupitia mkutano huu, Ufaransa imeapa kuchana kabisa na dhana ya ‘Francaafrique’, mkakati ambao Paris imekuwa ikiutumia kuziweka nchi ilizozitawala na zinazozungumza kifaransa kwenye himaya yake ikiwemo kuingilia siasa zake, kutaka makampuni yake pekee kupewa nafasi kwenye nchi hizo.