Colombia. Nyota wa muziki wa pop kutoka Colombia, Shakira, amezindua rasmi wimbo wake wa Kombe la Dunia 2026.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 49, anayejulikana kwa vibao kama Whenever, Wherever na Hips Don’t Lie, alidokeza wimbo uitwao “Dai Dai” usiku wa jana, ukiwa ndio wimbo maalumu kwa mashindano ya Kombe la Dunia 2026 yatakayofanyika Marekani, Mexico na Canada.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram amechapisha video ambayo ilirekodiwa katika Uwanja wa Maracanã nchini Brazil, akidokeza wimbo huo ambao amemshirikisha mkali wa Afrobeat Burna Boy unaotarajiwa kutoka Mei 14.

Hii ni mara ya pili kwa Shakira kuwa na wimbo rasmi wa Kombe la Dunia, utakumbuka aliwahi kutamba na wimbo wa Waka Waka (This Time for Africa) katika mashindano hayo ya mwaka 2010 yaliyofanyika Afrika Kusini.

Wimbo mwingine ambao ulikuwa wa ziada ulikuwa katika mashindano ya mwaka 2014 wimbo uitwao La La La (Brazil 2014), aliouimba katika hafla ya kufunga mashindano jijini Rio de Janeiro.

Shakira, ambaye ana watoto wawili kutoka kwenye uhusiano wake wa zamani na beki wa zamani wa Barcelona na Hispania, Gerard Piqué, pia aliwahi kuimba wimbo wa Hips Don’t Lie katika hafla ya kufunga Kombe la Dunia 2006 nchini Ujerumani.

Nchi yake ya Colombia inashiriki katika mashindano hayo ya timu 48 ya FIFA World Cup 2026, ambayo yatafanyika kuanzia Juni 11 hadi Julai 19.                                                                                                              

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *