Unguja. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amevunja ukimya kuhusu mazungumzo yanayoendelea baina ya chama chake na ACT Wazalendo kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Mara kadhaa viongozi wa ACT Wazalendo ndiyo wamekuwa wakizungumza kuhusu mazungumzo yanayoendelea baina ya pande hizo mbili lakini CCM kimemekuwa na ugumu kuzungumzia suala hilo.
Hata hivyo, Dk Mwinyi amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho kutokuwa na wasiwasi na mazungumzo hayo yanayoendelea kwani chama chao (CCM) kitaweka mbele masilahi yake na ya nchi kwa ujumla.
Dk Mwinyi ameyasema hayo leo Mei 9, 2026 katika ziara ya kuwashukuru na kuwapongeza viongozi na wanachama wa CCM baada ya chama hicho kushinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025 huko Mahonda katika ofisi za chama Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar, ukimalizika uchaguzi chama cha upinzani kilichopata kura nyingi kuungana na chama kilichoshinda na kutengeneza Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Tumewaandikia ACT, walete majina ya Makamu wa Kwanza wa Rais, na mawaziri wanne kwa sababu kwa mujibu wa viti walivyopata katika Baraza la Wawakilishi wanastahili nafasi nne katika Baraza la Mapinduzi,” amesema.
Dk Mwinyi amesema baada ya kuwaandikia ACT, walisema wanamalalamiko yao na kwamba hawataleta kwanza majina hayo mpaka malalamiko hayo yatakaposikilizwa.
“Sisi tuliwaambia sawa, serikali inakwenda na mambo yanafanyika, sisi tupo tayari kukusikilizeni, mkitaka njooni na kama hamtaki basi,” amesema.
Hivyo, amesema wameanza mazungumzo kuhusu malalamiko ya chama hicho ambapo wametengeneza ajenda za malalamiko hayo.
“Tutakaa tutazungumza lakini maslahi ya chama chetu na maslahi ya nchi yetu yatakuwa mwanzo, hatuwezi tukaburuzwa hata kidogo kwa sababu nia yetu ni njema, dhamira yetu ni njema ya kuleta umoja na amani katika nchi hii,” amesema.
“Mazungumzo hatutoyakataa, tutaendelea lakini wasidhani kama watatuburuza katika mazungumzo hayo, tupo tayari kwa mambo yote ambayo yana maslahi na nchi yetu na tupo tayari kushirikiana,” ameongeza Dk Mwinyi.
Amewaambia ACT kuwa hoja za mazungumzo zisiwe katika maslahi na chama chao kwani Chama cha Mapinduzi hakitakubali.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Said Mohammed Said (Dimwa) amesema ziara hiyo inaendelea kudhihirisha dhamira ya chama hicho ya kuwa karibu na watu wake na kusikiliza maoni yao na kuendeleza siasa ya maridhiano, maendeleo na mshikamano wa kitaifa.
Amesema Katiba ya CCM ibara ya 15 inaeleza kwamba nguvu na uimara wa Chama cha Mapinduzi unatokana na umoja wa wanchama wake, fikra sahihi za chama pamoja imani kubwa ya wananchi kwa chama chao.
Hivyo, amesema ni wajibu wao kuwa kila mwanachama na kiongozi wanalinda umoja huo, wanaenzi maadili ya chama na kuhakikisha CCM inaendelea kuwa ni nguzo kuu ya Amani, utulivu na maendeleo kwa wananchi.
Aidha, amesema ziara hiyo inaendana moja kwa moja na maelekezo ya ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/2030 ambayo inaelelekeza viongozi wa chama kuwa karibu zaidi na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kushiriki kikamilifu katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.
Amesema jambo hilo linaendelea kuifanya CCM kuwa ni chama kinachoaminiwa na wananchi na chenye kuendelea kupata ridhaa ya kuongoza wananchi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Idd Ali Ame amempongeza Dk Mwinyi kwa utekelezaji wa Ilani anaonendelea kuufanya ndani ya mkoa huo ambapo kwa kiasi kikubwa ameubadilisha mkoa wa Kaskazini na Zanzibar kwa ujumla.
Amesema miradi mingi ya kimaendeleo imetekelezwa ndani ya mkoa huo kama vile ujenzi wa skuli za ghorofa za kisasa zisizopungua sana, vituo vya afya, barabara za mfano zenye hadhi sambamba na ujenzi wa bandari Jumuishi ya Mangapwani.
Vilevile, amesema kuna miradi mikubwa ya maji ambapo ikikamlika kutakuwa na historia ya ukosefu wa maji katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kwa upande wa hali ya kisiasa, mwenyekiti huyo amesema hali ya kisiasa kabla, wakati na baada ya uchaguzi ni nzuri na kwamba chama kimeendelea kuwa imara na kutekeleza majukumu yake kama kawaida.