Kila siku, wastani wa wanawake 700 hupoteza maisha kutokana na sababu zinazohusiana na ujauzito au uzazi duniani kote, hiyo ni kwa mujibu wa Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mwenendo wa Vifo vya Uzazi 2000-2023. Takwimu hizi za kushtua zinatokea wakati ambapo karibu vifo vyote hivi vinaweza kuzuilika.

Ikiwa leo dunia inaadhimisha Siku ya Mama Duniani inayoadhimishwa tarehe 10 Mei, kila mwaka, UNFPA kupitia makala iliyochapishwa kwenye wavuti wake kutokea jijini New York, Marekani, imewauliza wakunga kuhusu kumbukumbu zao za kuwasaidia wanawake kunusurika katika safari ya kuelekea kuwa mama.

© UNFPA Mzazi Kindness Ngoh (kulia) amemshika mtoto mchanga na mama wa mtoto huyo akimtazama mtoto pia huko Cox’s Bazar, Bangladesh.

Kindness, ambaye asili yake ni nchini Cameroon, amehudumu katika maeneo ya dharura kote duniani, kuanzia Yemen hadi Sierra Leone, akisaidia wanawake kujifungua katikati ya migogoro, magonjwa na njaa. Amesimulia akisema, “Nikiwa mkunga, nimejifunza kuwa kuokoa maisha ya mama kunamaanisha kuokoa zaidi ya maisha ya mtu mmoja,” akaongeza.“Inamaanisha kuwalinda watoto wasipoteze chanzo chao cha kwanza cha upendo, kuziweka familia pamoja, na kuhifadhi nguvu na matumaini ya jamii.”

Nini hupotea mama anapofariki?

Kwa muda mrefu, tafiti zimeonesha kuwa kifo cha mama huongeza hatari ya kifo cha mtoto pia. Watoto wanaobaki hai mara nyingi hukumbana na changamoto za lishe duni na umasikini uliokithiri. 

“Wakati mama anapofariki, watoto wanapoteza malezi, familia zinapoteza utulivu, na jamii zinapoteza matumaini. Kidonda cha kihisia ni cha muda mrefu, lakini pia kuna madhara katika malezi: nani atamlisha mtoto mchanga, nani atamtunza mtoto akikua, nani atatengeneza kaya, na nani atabeba maombolezo ya huzuni hiyo?” amefafanua Kindness.

Kwa Mkunga Kindness, vifo hivi pia hupoteza uwezo na ujuzi wa wanawake kuchangia mawazo na ubunifu wao duniani. Ameeleza, “Kwangu mimi, kifo cha uzazi si tukio la kitabibu tu. Ni upotevu wa mustakabali wa mwanamke, nanga ya familia, na matumaini ya jamii.” 

© UNFPA/Siegfried Modola Wanawake wote wanastahili matibabu yanayohitajika ili kuokoka ujauzito na kujifungua. Anastasia anatabasamu anapokuwa amelala kando ya mtoto wake mchanga huko Chisinau, Moldova.

Ndoto za wasichana humezwa na vifo vya uzazi

Mara nyingi, akina mama wanaofariki ni wasichana wadogo ambao bado wana maisha mbele yao. Elestina Yvonne Phuka, mkunga kutoka Malawi anasema, “Mwanadarasa mwenzangu wa shule ya sekondari alikuwa mwerevu, mwenye ndoto nyingi na mrembo. Kila mtu aliamini alikuwa na mustakabali mzuri mbele yake.” Msichana huyo alifariki baada ya kupata ujauzito akiwa na umri wa miaka 16, “Msichana mdogo mwenye uwezo mkubwa alitoweka kabla hata hajapata nafasi ya kuishi maisha yake kweli.”

Ni changamoto inayoendelea kwa miaka na mikaka

Historia imejaa wanawake waliopoteza ndoto zao mapema, kama mwanafalsafa Mary Wollstonecraft (1797) na shujaa Raden Adjeng Kartini (1904). Hata leo, vifo hivi vinaendelea; kuanzia mbunge wa Uganda Grace Kaudha (2017) hadi mshindi wa dhahabu wa Olimpiki Tori Bowie (2023). Inakadiriwa kuwa vifo 260,000 vya uzazi hutokea kila mwaka, na asilimia 60 ya vifo hivyo vipo kwenye nchi zenye migogoro.

Ingawa vifo vimepungua kwa asilimia 40 duniani kati ya mwaka 2000 na 2023, vimeongezeka katika nchi 16 ikiwemo Marekani, Jamaica, na Venezuela.

© UNFPA/Miléquêm Diarassouba Mariama, huko Togo, aliogopa kwamba huenda asingpona wakati wa kujifungua, lakini kwa msaada wa mkunga Boame Mone, yeye na mwanae wako hai na wanaendelea vizuri.

Wakunga waonesha ushujaa

Licha ya takwimu hizi, wakunga wameazimia kuleta mabadiliko. Noor Hadi, mkunga nchini Yemen, anamkumbuka Wijdan, msichana wa miaka 16 aliyekuwa na utapiamlo: “Yeye mwenyewe alikuwa bado mtoto. Alikuwa na uoga sana.” Wijdan mwenyewe aliiambia UNFPA: “Sikudhani kama ningenusurika. Lakini shukrani kwa mkunga, nilifanikiwa.”

Vikwazo vya mfumo dume pia vimechangia. Mkunga Elena Estela Santiago Raimundo amesema: “Ni mwanamume ndiye anayeamua ikiwa mwanamke aende au asiende kliniki. Ukosefu wa usawa wa kijinsia unamaanisha wanawake hawana haki ya kutafuta huduma za afya.”

Goitom Assefa wa Ethiopia ameeleza jinsi walivyosaidia wanawake 115 kujifungua wakati wa vita: “Tulisaidia wanawake 115 kujifungua watoto wao salama katika hali ngumu, mara nyingi tukitumia mifuko ya plastiki kama ndio glavu na bila oxytocin ya kuzuia damu kuvuja kwa wingi.”

Boame Mone, mkunga nchini Togo, amesisitiza: “Tunaweza kubadili mwelekeo huu. Tunashughulikia ujauzito zenye hatari kubwa, tunachukua hatua haraka, na tunaokoa maisha hapa hapa.”

Taswira ya dunia bila vifo vya uzazi 

Mkunga Kindness anahitimisha kwa kukumbuka wanawake aliowahudumia: “Ninakumbuka wanawake waliokuwa na ndoto mbali zaidi ya chumba cha kujifungua. Wanawake wanaotunza familia nzima, akina mama wanaoendesha biashara ndogondogo, wanafunzi vijana, na wasichana balehe waliotaka kurudi shule.”

Ameongeza: “Kama kusingekuwa na mama anayefariki katika ujauzito au uzazi, dunia ingekuwa na huruma zaidi, yenye nguvu zaidi, na yenye usawa zaidi. Watoto wengi zaidi wangekua na mama zao wenye upendo. Familia nyingi zaidi zingebaki imara. Wanawake wengi zaidi wangeishi kutimiza ndoto zao, kulea watoto wao, kuongoza jamii zao, na kuchangia katika jamii.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *