Marekani. Bila shaka ukilisikia jina la Lupita Nyongo unakumbuka ile filamu ya ‘Black Panther’, ‘Wakanda Forever’, ‘12 Years of Slave’ akicheza uhusika unaoendana na maisha halisi ya uhuru wa watu weusi, utu na nguvu ya mwanamke.
Kazi yake ya kwanza maarufu kuifanya ilikuwa ‘12 Years of Slave’ humo alicheza kama Patsey mwanamke mtumwa anayefanya kazi kwenye mashamba ya miwa Marekani.
Kwenye filamu hiyo alionyesha hisia za mwanamke anayekabiliana na mateso, ukandamizaji wa kihisia na kimwili, na hali ya kutokuwa na uhuru.
Tangu acheze uhusika huo aliendelea kupata madili ya kuigiza filamu mbalimbali lakini zilikuwa zinaendana na uhusika uleule wa mwanamke mtumwa aliyeonea.
Kwenye moja ya mahojiano anasema “ Oh, Lupita, tungependa ucheze filamu nyingine ambapo wewe ni mtumwa. Lakini sasa mara hii uko kwenye meli ya watumwa.”
“Mimi sio nadharia, mimi ni mtu halisi nilikuwa tayari kufanya kazi kidogo lakini sio zile ofa kubwa za waongozaji wa Marekani waliotaka niendelee kucheza uhusika huo na kueneza dhana potofu juu ya wanawake wa Kiafrika.”
Sasa huyo ndio Lupita mmoja wa mastaa kutoka Afrika Mashariki walioweka rekodi ya aina yake Marekani na duniani. Hapa nimekuwekea rekodi zake tano ambazo hazijavunjwa hadi sasa.
Lupita alizaliwa Machi 1983, mjini Mexico City na wazazi wake wawili Wakenya, Dorothy Ogada Buyu na Anyang Nyong’o, ambaye alikuwa profesa wa chuo kikuu nchini humo.
Familia yake ilitimka Kenya mwaka 1980 kutokana na ghasia na ukandamizaji wa kisiasa na baada ya hali kutulia walirejea nchini kwao.
Akiwa na umri wa miaka 14 alivutiwa na maigizo ya shule, akafanikiwa kucheza tamthilia yake ya kwanza Romeo and Juliet iliyoandaliwa na kampuni ya Phoenix Players ya Nairobi.
Baada ya hapo, Lupita alikwenda Mexico kwa muda wa miezi saba kujifunza Kihispania na pia kuendelea na elimu ya sekondari St. Mary’s School Nairobi, akipata IB Diploma mwaka 2001.
Baadaye alisoma Marekani, akiwa na shahada ya Film and Theatre Studies kutoka Hampshire College.
1. Tuzo ya Oscar
Rekodi ya kwanza Lupita aliweka historia ya kushinda tuzo ya Oscar kwenye kipengele cha ‘Best Supporting Actress’ kupitia filamu ya 12 Years a Slave mwaka 2014.
Ikumbukwe alichukua tuzo hiyo ikiwa imepita mwaka mmoja tangu filamu hiyo iachiwe na ikafanya vizuri na kutazamwa na watu wengi.
Alikuwa mwanamke wa kwanza wa Kenya kushinda tuzo hiyo na kuwa mmoja wa Waafrika wachache kuchukua tuzo hizo kubwa duniani.
Muigizaji wa kwanza kutoka Afrika kuchukua tuzo hiyo alikuwa mwanamama, Charlize Theron kutoka Afrika Kusini ambaye ana uraia wa Marekani. Alishinda kipengele cha ‘Best Actress’ mwaka 2004 kupitia filamu ya Monster.
2. Ushawishi Ulaya
Ukitoa uigizaji Lupita anafanya kazi za uanamitindo na ni miongoni mwa mastaa wanaotamba kwenye majukwaa ya mitindo Ulaya.
Majukwaa kama Cannes Film Festival, Paris Fashion Week ni sehemu ambazo amekuwa akialikwa sana kutokana na utofauti wa mavazi yake anayoyaonesha.
Ana rekodi ya kuwa Mkenya wa kwanza kuheshimika duniani kutokana na kipaji cha kuigiza na kuvaa vizuri zaidi na amekuwa akialikwa na brand kubwa za mavazi kama Dior.
3. Heshima
Mbali na Oscar, Lupita amenyakua tuzo mbalimbali kubwa duniani, zikiwamo BAFTA Awards za Uingereza pamoja na Screen Actors Guild Awards.
Hilo linaonyesha kuwa kipaji chake kinatambulika duniani si Marekani pekee. Bali hadi kwenye masoko makubwa ya kuuza filamu Ulaya.
4. Filamu nyingine
Ni kama ‘12 Slaves’ ilimfungulia milango ya kupata madili ya kuigiza kwenye kazi mbalimbali.
Lupita aliendelea kung’ara katika filamu kubwa zilizofanya vizuri kimataifa, ikiwamo Black Panther. Filamu hii haikuwa tu ya kuburudisha, bali ilibeba utamaduni wa Kiafrika na kuwafanya Waafrika wengi kujivunia asili yao.
Alionyesha uwezo wa kipekee na kitofauti katika filamu ya kutisha ya Us. Ambapo uigizaji wake ulisifiwa na wakosoaji na wachambuzi wa filamu duniani.
Filamu hizi sio tu zilimuongezea umaarufu lakini pia kifedha zilimpa mikwanja mingi Ulaya na kuongeza jina lake kimataifa.
5. Wasanii wanamjua
Kutokana na kazi kubwa aliyoifanya kwenye uigizaji baadahi ya wasanii wakubwa kama JAY-Z na wengineo wameshamtaja kwenye ngoma zao.
Mbali na kutajwa amepata madili ya kuwa video vixen kwenye nyimbo ya JAY-Z ‘Many face God’ akimshirikisha James Blake ngoma iliyotoka miaka nane iliyopita.
Kwenye ngoma ya Beyonce ‘Brown Skin Girl’ aliyomshirikisha Wizkid mwanadada huyo alitokea kwenye video lakini pia jina lake lilitajwa kama mmoja ya wanawake shupavu anapokuwa kwenye kamera.
Lupita ni sauti ya Waafrika kwenye majukwaa makubwa, ni mfano wa kuigwa kwa vijana wanaochipukia kwenye sanaa ya uigizaji Afrika Mashariki, jarida la Times 100 lilimtaja kama mwanamke mwenye ushawishi mkubwa.