
KAIMU Kocha Mkuu wa Ceasiaa Queens, Sultan Juma amesema kukosekana kwa wachezaji wawili wa kigeni, Anita Adongo na Diana Cherono, ni pigo kubwa kwa timu hiyo kutokana na mchango waliotarajiwa kuutoa kwenye kikosi hicho.
Akiwazungumzia wachezaji hao raia wa Kenya, Juma amesema wachezaji wa kigeni walisajiliwa ili kuongeza ubora na ushindani ndani ya timu, hivyo kutokuwepo kwao kunaleta pengo kubwa kiufundi na kimkakati.
“Timu inaposajili wachezaji wa nje ina maana wanakwenda kuongeza kitu na kuleta ushindani kwa wenzao, hivyo kuwakosa ni pigo,” amesema Juma.
Kocha huyo amehoji hali hiyo kwa kusema klabu huwekeza rasilimali kubwa kupata wachezaji hao, ikiwemo gharama za vibali na maandalizi ya kambi.
“Ndiyo hivyo changamoto ya kuwalipia vibali halafu hadi waje waruhusiwe kama umechelewa unakuta tena hadi dirisha lingine hawachezi, tunakaa nao kambini tu,” aliongeza.
Timu hiyo tangu Desemba imekuwa ikipitia changamoto ya kushindwa kukamilisha vibali vya wachezaji wa kigeni jambo linalowafanya nyota hao waendelee kukaa jukwaani.
Msimu uliopita timu hiyo ilimaliza katika nafasi ya sita kwenye mechi 18, ilishinda sita, sare tatu na kupoteza tisa, ikifunga mabao 25 na kuruhusu 37, ikikusanya pointi 21.