LIGI ya Championship imebakisha mechi sita kumalizia msimu huu wa 2025-2026, huku ushindani ukiongezeka kwa kila timu kutokana na mahitaji mbalimbali, hususani kwa zile zinazotafuta nafasi ya kupanda Ligi Kuu Bara na za kushuka.

Ushindani huu unaanzia kwa timu mbili zitakazomaliza nafasi ya kwanza na ya pili zitakazokata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, zitakazocheza ‘Play-Off’ ya kupanda au kushuka na zile zitakazoshuka moja kwa moja kwa maana za nafasi ya 15, 16.

Wakati vita ya kuwania nafasi hizo ikishika kasi katika mechi sita zilizobaki, zipo rekodi mbalimbali zinazosubiriwa kwa hamu kuona ikiwa zitavunjwa au zitaendelea kutawala tofauti na msimu wa 2024-2025, kama ambavyo Mwanaspoti linazielezea.

CHAMP 05

REKODI YA POINTI NYINGI

Geita Gold na Kagera Sugar zina mtihani wa kuvunja rekodi ya msimu uliopita wa 2024-2025, iliyowekwa na Mtibwa Sugar inayocheza kwa sasa Ligi Kuu Bara ya kukusanya pointi nyingi zaidi, wakati ikiwa inashiriki Championship.

Msimu uliopita Mtibwa Sugar ilikuwa bingwa wa Championship ikiongoza na pointi 71, baada ya kucheza mechi 30, ikishinda 22, sare tano na kupoteza tatu, ikiungana na Mbeya City  iliyomaliza ya pili na pointi 68 kurejea Ligi Kuu.

Rekodi hiyo ya Mtibwa Sugar inaweza kuvunjwa na Geita Gold inayoshika nafasi ya kwanza na pointi 61, kwani ikishinda mechi zote sita zilizobakia itafikisha 79 na kurejea rasmi Ligi Kuu Bara, baada ya kushuka daraja msimu wa 2023-2024.

CHAMP 04

Pia, ikiwa Geita Gold itashinda mechi zote sita zilizobaki itaandika rekodi mpya ya kupoteza mechi chache zaidi, kwani hadi sasa imepoteza moja, tofauti na Mtibwa Sugar iliyopoteza tatu msimu uliopita.

Kagera Sugar inayoshika nafasi ya pili na pointi zake 58, inaweza kuvunja pia rekodi ya Mtibwa Sugar, kwani ikishinda mechi sita zilizobakia itafikisha 76, ikipambana kurejea Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2024-2025.

Kagera iliyodumu Ligi Kuu Bara kwa miaka 20 tangu mwaka 2005, imepoteza mechi mbili na ikishinda pia sita zilizobakia, itavunja rekodi ya Mtibwa Sugar, ambayo msimu wa 2024-2025 ilipoteza tatu.

Hata hivyo, moja ya rekodi bora iliyoweka Mtibwa Sugar msimu wa 2024-2025, ni kucheza mechi za nyumbani bila ya kupoteza wala kutoka sare, jambo ambalo hadi sasa limeshindikana kwa Geita Gold na Kagera Sugar, licha ya mwenendo wao mzuri.

CHAMP 03

Ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Kiluvya United (Kwa sasa Barberian FC) Mei 11, 2025, uliifanya Mtibwa kushinda mechi 15, kati ya 30, kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro, ikiwa ni rekodi mpya, huku ikifunga mabao 38 na kuruhusu sita.

Pia, pointi 71 ilizopata ni rekodi, kwani tangu msimu wa 2021-2022, hakuna timu iliyofikisha na 2021-2022, ilikuwa ni Ihefu (Kwa sasa Singida Black) iliyomaliza na pointi 66, huku 2022-2023, JKT Tanzania ilikusanya pointi 63.

Msimu wa 2023-2024, KenGold ya Mbeya iliyoshuka daraja msimu wa 2024-2025 ikitoka Ligi Kuu Bara, ilimaliza na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji iliyokuwa na pointi 67, iliyorejea baada ya kusota miaka 23, tangu iliposhuka daraja mwaka 2001.

CHAMP 02

UFUNGAJI BORA

Sehemu nyingine inayosubiriwa kwa hamu ni ya kuvunja rekodi ya ufungaji bora inayoshikiliwa na wachezaji watatu msimu wa 2024-2025, ambao ni Andrew Simchimba, Raizin Hafidh na Abdulaziz Shahame ‘Haaland’, waliofunga kila mmoja mabao 18.

Simchimba alifunga mabao hayo akiwa na Geita Gold japo kwa sasa anacheza Mtibwa Sugar kwa mkopo akitokea Singida Black Stars, sawa na nyota mwenzake, Raizin Hafidh huku Abdulaziz Shahame ‘Haaland’, akiichezea Namungo FC ‘Wauaji wa Kusini’.

Idadi hiyo ya mabao 18 ya nyota wote watatu, inaweza kufikiwa au kuvunjwa na mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mzambia Obrey Chirwa mwenye 15, huku Ramadhan Hashim wa B19 FC akiwa amefunga 13 na Abrahaman Mussa wa Transit Camp aliyefunga pia 12.

Nyota wengine wanaofuatia kwa kufunga mabao mengi msimu huu ni Maulid Shaban wa Geita Gold aliyefunga 11, huku Boniface Mwanjonde (Mbeya Kwanza), Emmanuel Mpuka (Polisi Tanzania) na Samson Albert wa KenGold kila mmoja akiwa amefunga 10.

CHAMP 01

REKODI YA HAT-TRICK

Wakati zikibakia mechi sita za kumalizia msimu huu wa 2025-2026, tayari zimeshafungwa hat-trick nne, zikibakia mbili ili kuifikia rekodi iliyowekwa msimu wa 2024-2025, tulioshuhudia wachezaji sita wakifunga.

Mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mzambia Obrey Chirwa ameweka rekodi ya mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga mabao matatu (Hat-Trick), wakati kikosi hicho kilipoifunga Hausung kutoka Njombe mabao 3-1, Desemba 2, 2025.

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, Azam, Namungo, Ihefu (kwa sasa Singida Black Stars) na KenGold, alifunga mabao hayo, akiwa ndiye anayeongoza hadi sasa baada ya kufunga 15.

Mwingine ni Boniface Mwanjonde wa Mbeya Kwanza katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 5-0, dhidi ya B19 FC, Desemba 17, 2025 na mshambuliaji huyo amerejea tena baada ya uhamisho wake kwenda Fountain Gate kukwama.

Wengine ni Japhet Makarai wa TMA FC ya Arusha aliyeifungia timu hiyo katika ushindi wa mabao 4-2, dhidi ya Stand United, Aprili 19, 2026 na wa nne ni Salum Ngadu wa Gunners FC wakati kikosi hicho kikiichapa Mbuni FC 3-2, Aprili 20, 2026.

Msimu wa 2024-2025, zilifungwa ‘Hat-Trick’ sita, akianza Faraji Kilaza Mazoea aliyekuwa Mbeya City ingawa kwa sasa yupo Geita Gold, aliyeifungia timu hiyo katika ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya maafande wa Polisi Tanzania, Desemba 13, 2024.

Andrew Simchimba akiichezea Geita Gold alifunga pia timu hiyo iliposhinda mabao 4-0, dhidi ya Transit Camp, Februari 10, 2025, huku Oscar Tarimo wa Mbeya Kwanza akaifungia kikosi hicho kilipoichapa Biashara United 5-0, Februari 23, 2025. 

Wengine ni William Thobias wa Mbeya City katika ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya Kiluvya United (kwa sasa Barberian FC), Machi 17, 2025, huku, Emmanuel Manyanda akaifungia Stand United ilipoichapa Green Warriors mabao 5-1, Aprili 20, 2025.

Mchezaji wa mwisho kufunga hat-trick msimu wa 2024-2025, alikuwa ni nyota wa African Sports, Frank Edmund aliyefunga katika ushindi wa kikosi hicho cha ‘Wanakimanumanu’, kilipoichapa pia maafande wa Transit Camp mabao 3-2, Mei 11, 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *