Iringa. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewateua makada 17 kutoka kwenye vyama mbalimbali vya siasa kuwania ubunge wa Isimani mkoani Iringa ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Lukuvi, aliyefariki Machi 25, 2026.

Watiania walioteuliwa na INEC ni pamoja na Emannuela  Mtatifikolo (CCM), Farida  Mwapungu  (Demokrasia Makini), Asha Chuma (UPDP), Fidelis  Mtikile (Sau), Hadija Makawa (Ada-Tadea), Protas Mgimbila (CCK), Zavely Seleleka (UDP), Berbard Mwingila (DP) na Burton Chitenga (NCCR Mageuzi).

Wengine ni Christina  Mbaunga (NRA), Mark Mhemela (AAFP), Nassim Upete (CUF), Mwaka Mgimwa (TLP), Asma Othern (UMD), Maimuna Lumato (ADC), Daudi Masasi (Chaumma) pamoja na Subira Kalolo (NLD).

Ushindani huo unatajwa kuwa miongoni mwa chaguzi ndogo zenye mvuto wa kisiasa kutokana na idadi kubwa ya wagombea watakaoshiriki huku kila chama kuteka imani ya wananchi wa Isimani ili kushinda nafasi hiyo muhimu ya uwakilishi bungeni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 11, 2026 mkoani Iringa, msimamizi wa uchaguzi wa INEC katika jimbo hilo, Caroline Otieno amesema kukamilika kwa hatua ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi kumeashiria mwanzo rasmi wa mchakato wa kampeni kwa wagombea waliokidhi masharti ya uchaguzi.

Otieno amesema mtiania wa ACT Wazalendo hakuteuliwa kwa sababu hakurejesha fomu zake ndani ya muda uliowekwa na INEC licha ya kuwa alikuwa tayari amezichukua fomu hizo.

Otieno amesema utoaji wa fomu ulianza mapema mwezi huu na kuhitimishwa Mei 10 huku hatua inayofuata ikiwa ni uwekaji wa pingamizi kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.

“Majina ya wagombea walioteuliwa tayari yamebandikwa katika maeneo mbalimbali ya wazi ili kutoa nafasi kwa wananchi au vyama vyenye malalamiko kuwasilisha mapingamizi kabla ya kampeni kuanza rasmi,” amesema Otieno.

Amesema iwapo hakutakuwa na pingamizi lolote ndani ya muda wa kisheria, wagombea wote wataruhusiwa kuendelea na kampeni zao katika jimbo hilo lenye ushindani mkubwa ikizingatiwa kuwa wote watakuwa wagombea wapya.

Aidha, kuanza rasmi kwa kampeni kumeongeza hamasa kwa vyama vya siasa vinavyowania nafasi hiyo huku kila upande ukionesha matumaini ya kufanya vizuri katika uchaguzi huo.

Mgombea wa Chaumma, Daudi Masasi amesema chama chake kinaingia katika uchaguzi huo kikiwa na imani ya kuibuka na ushindi kutokana na maandalizi waliyojiwekea pamoja na ushirikiano kutoka kwa wananchi wa Isimani.

Masasi amesema chama hicho kitafanya kampeni za karibu zaidi kwa wananchi kwa kutumia mbinu ya kuwafikia mmoja mmoja ili kueleza sera na malengo yake kwa wapigakura.

Mgombea wa CCM, Emmanuela Mtatifikolo amesema ushindani uliopo haupaswi kuwafanya wanachama wa chama hicho kulegeza juhudi katika kutafuta kura kutoka kwa wananchi wa Isimani.

Mtatifikolo amewataka wanachama na viongozi wa CCM katika Wilaya ya Iringa Vijijini pamoja na maeneo mengine ya mkoa huo kushirikiana kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi mkubwa.

“Muda wa kampeni unapaswa kutumiwa vizuri kwa kuwafikia wananchi katika maeneo yote ya jimbo hilo ili kueleza mafanikio ya chama na mipango kwa maendeleo ya wananchi,” amesema Mtatifikolo.

Katika hatua nyingine, CCM Wilaya ya Iringa Vijijini imetangaza kuwa uzinduzi rasmi wa kampeni zake unatarajiwa kufanyika Mei 12, 2026 katika Kijiji cha Itunundu Pawaga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *