HAKUNA msimu unakosa kusikia kauli hii ‘Klabu fulani imegoma kutumia vyumba vya kubadilishia nguo na kukaa eneo lingine.’

Ukiikosa kauli hiyo, utakuja kuona hili, ‘Kamati ya Usimamizi ya Bodi ya Ligi Kuu imeipiga faini ya Sh5 milioni au zaidi) klabu fulani kwa kwa kukataa kutumia chumba rasmi cha kubadilishia nguo kwenye uwanja fulani, adhabu hiyo ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 ya ligi kuhusu taratibu za mchezo’.

Matukio haya mawili yamekuwa ni kawaida kwasasa kwenye mechi za Ligi Kuu na baadhi ya klabu zimekuwa zikichukua maamuzi kama hayo ambayo baadaye yamezalisha adhabu mbalimbali kwenda kwa klabu husika iliyogoma kutumia vyumba stahiki.

Klabu zimekuwa zikibadilishia nguo kwenye korido, sehemu ya waandishi wa habari au vyumba vingine ambavyo vinapatikana kwenye uwanja husika kwa hofu moja tu, ‘vyumba siyo salama’.

Matukio haya sasa yamechukua sura mpya na tukio kama hili lililoenda mbali zaidi ni Mei 3, 2026 wakati wa mechi ya Dabi ya Kariakoo na mgeni Yanga iliamua kuachana kabisa na majengo ya Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam na kwenda kutumia nyumba iliyopo mkabala na uwanja huo kama sehemu ya kubadilishia nguo wakati ikijiandaa kucheza dhidi ya Simba ambayo ilikuwa mwenyeji.

Kabla ya hapo, itakumbukwa Simba ikiwa mgeni wa Yanga kwenye mechi ya duru la kwanza iliyochezwa Machi Mosi, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ilitumia eneo la wanahabari ikidai kugundua matundu yaliyokuwepo ndani ya chumba cha kubadilishia nguo cha timu mgeni na kuhofia labda yametumika kupitisha dawa.

Hata hivyo, mamlaka ya Serikali kupitia kamishna ya viwanja Zanzibar ilikuja na kufafanua tuhuma hizo za matundu hayo lakini Simba bado haikukubaliana na tamko hilo ikigomea tena vyumba hivyo kwenye mechi ya Fainali ya Kombe la Muungano na kutumia vya zamani vilivyokuwa vinatumika kabla ya uwanja huo kufanyiwa marekebisho.

Hili limekuwa halivumi kwa klabu hizo kongwe pekee na hatua hiyo imeendelea kushamiri na sasa hata klabu nyingine za madaraja ya kati zimekuwa zikishutumiana juu ya mambo hayo, hatua ambayo ikalilazimu Mwanaspoti kuingia msituni na kutafuta shida halisi ni ipi na kama kuna ukweli kuhusu jambo hilo kwa kuwatafuta viongozi mbalimbali wa klabu za ligi na zile za Championship.

KANUNI ZINASEMAJE?

Kwa mujibu wa kanuni ya 17 kuhusu taratibu za mchezo kifungu cha 37 inasema: “Timu inaruhusiwa kutumia vyumba vya kuvalia (dressing room) saa 8 (nane) kabla ya mchezo kuanza.”

Kanuni hiyohiyo kifungu cha 62, inasema: “TPLB itachukua hatua kwa ukiukwaji wowote wa Taratibu za Mchezo kama zilivyoainishwa kwenye kanuni ya 17 kwa kutoa onyo kali au karipio au kutoza faini kuanzia Sh5 milioni hadi Sh10 milioni na/au kufungia michezo isiyozidi mitatu au kipindi kisichozidi miezi mitatu. Faini kwa makosa yanayojirudia itatozwa kati ya Sh11 milioni na Sh20 milioni kwa mchezaji, kiongozi au timu.”

MATUKIO NA ADHABU ZAKE

Msimu uliopita, kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Julai 15, 2025, iliitoza Fountain Gate faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kukataa kutumia chumba maalum cha kuvalia kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Msimu huu baadhi ya matukio hayo ya timu kukataa kutumia vyumba iliwagusa Simba na kamati hiyo katika kikao chake cha Machi 4, 2026, iliitoza faini ya Sh5 milioni kwa kosa la kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ilipokuwa na mechi dhidi ya Yanga Machi 1, 2026.

Azam pia ilitozwa faini ya Sh5 milioni kwa kukataa kutumia chumba rasmi cha kubadilishia nguo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, katika mechi dhidi ya Yanga Machi 15, 2026 na kumalizika kwa suluhu.

Tukio la karibuni ni lile la Yanga na wachezaji na maofisa wake wa ufundi kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam na badala yake walitumia nyumba iliyo nje ya uwanja upande wa pili wa barabara kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Faini yake imekuwa kali zaidi kwani ni Sh30 milioni, likiwa ni tukio la kwanza kwenye historia kwa klabu kutumia nyumba ya nje ya uwanja.

“Tunasubiri tuone adhabu yake itakuwaje, kwa kuwa sisi kambi yetu ipo hapa jirani na uwanja tunaweza kuvalia huko huko na kuja uwanjani na wakati wa mapumziko tukawasha gari kwenda kupumzika kambini kwetu,’’ hii ilikuwa kauli ya kiongozi mmoja wa Simba baada ya tukio la Yanga kuvalia kwenye nyumba ya jirani.

TUHUMA ZILIVYO

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali kutoka kwa wadau wa klabu hizo tofauti zimeonyesha ukiacha masuala ya kishirikina lakini msukumo mkubwa wa kugomea vyumba unatokana na tuhuma za kupuliziana dawa za kuathiri utendaji wa  wachezaji uwanjani.

ZINAPIGWA WAPI

Uchunguzi wa Mwanaspoti umefichuliwa ukiacha hatua ya upuliziaji dawa katika vyumba, zipo njia nyingine tofauti na mifumo ya hewa ndani ya vyumba hivyo ikiwemo viyoyozi hutumika katika kufanikisha hilo.

“Kuna njia tofauti zipo dawa ambazo zinapigwa ndani ya vyumba tu ukiingia kichwakichwa unakutana nazo, unajua zipo ambazo zina harufu na zingine harufu yake sio kali, mara nyingi hizo zinapigwa kwenye viwanja vya mikoani huko.

“Zingine zinapigwa kwenye mifumo ya AC (viyoyozi), wahusika wanajua namna ya kufanya hilo, ukiingia unataka kiyoyozi, ukiwasha tu unakutana nazo na unajua uwanjani timu zinafika mapema, hebu fikiria unafika uwanjani saa moja na nusu kabla mchezo kuanza.

“Ukifika kuna taratibu mbalimbali zinafanyika kama ukaguzi na makocha kujipanga, wakati wote huo mnavuta ile hewa, sasa hadi mkiingia uwanjani tayari mnakuwa mmeshaathirika, wenzetu hawa (anaitaja timu kubwa) wao wanapiga sana wakati wa mapumziko wanajua pale lazima mnahitaji kupoza miili mkiwasha AC tu mmeumia, mkirudi kipindi cha pili wanawapiga wanavyotaka kwa kuwa zinawachosha wachezaji na kuwafanya kulegea.

Aidha kigogo mwingine ameeleza dawa hizo hazipigwi kwenye vyumba pekee na klabu moja ya nje ilishawahi kukumbana nazo zikiwekwa kwenye maji katika moja ya hoteli kubwa ambayo timu ya kutoka nje ilifikia.

“Kuna timu moja kutoka nje iliwahi kuja hapa kucheza na sisi kule walitufunga lakini tukasema hawa lazima watuachie pointi tatu hapa ili twende zetu sasa hawa jamaa zetu (anaitaja timu moja kubwa ya hapa ndani) tulihisi wangevujisha siri yetu, tukapata akili ya kuwatafuta hawa wageni hadi hotelini tukafanikiwa, njia ni nyingi hata kwenye maji mnaweza kuathiriwa tu.’’ 

WASIKIE MAMENEJA WA VIWANJA

Meneja wa Uwanja wa Mkapa, Gabriel Mwasele akizungumzia tuhuma hizo alikiri kusikia taarifa hizo za malalamiko, lakini akasema hakuna timu ambayo imewahi kulalamika kwa maandishi juu ya hicho ilichokutana nacho.

Mwasele alisema ni wakati mwafaka kwa klabu zinazokutana na kadhia hiyo, kuchukua maamuzi ya kulalamika rasmi ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wahusika ambao watabainika kufanya mambo hayo.

“Nimesikia malalamiko ya namna hiyo, zipo hizo taarifa mtandaoni lakini bahati mbaya sana huwa tunazisikia huko nje, hakuna klabu ambayo imewahi kuja hapa kwetu na kutupa malalamiko rasmi juu ya hayo yanayosemwa.

“Mpira una taratibu zake, kuna wenzetu wa TFF ambao kimsingi wameweka taratibu nzuri na urahisi kuanzia wasimamizi wa michezo na wengine ambao wangetumika kufikisha malalamiko kama haya.

“Hapa kwetu Uwanja wa Mkapa utaratibu wetu ni ikifika saa mbili kamili asubuhi tunagawa funguo kwa watu wa ulinzi wa timu husika ili wajihakikishie usalama wa vyumba vyao lakini bahati mbaya wale watu wanakuwa pale hadi timu zao zinapofika, timu zikifika ndiyo utasikia hayo mambo.

“Unajiuliza hawa waliokuwa hapa hawakuwa wanasikia hizo harufu? Wakishaona hivyo wanakwenda kulalamika kwenye vyombo vya habari na siyo kutuletea malalamiko rasmi, tukisikia tunawauliza TFF kuna hili linazungumzwa kwenu limewafikia, wanatujibu hakuna na sisi tunaishia hapo.”

Akizungumzia ishu ya mifumo ya kiyoyozi kuchezewa, Mwasele alisema: “Sio rahisi kufikia hiyo mifumo na kuchezewa kama ambavyo inaelezwa, hapa tuna wataalamu mbalimbali ambao wanafanya ukaguzi kila wakati tungeshaligudua hilo.”

MENEJA WA ISAMUHYO HUYU HAPA

Kwa upande wa meneja wa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Said Mpuche alisema uwanja huo siyo rahisi kufanyika vitendo hivyo kutokana na ulinzi mkubwa unaozunguka eneo hilo na hawajawahi kupokea malalamiko ya madai hayo zaidi ya kuyasikia sehemu mbalimbali.

“Kweli hayo mambo yanasemwa lakini hapa kwetu hakuna ambaye amewahi kufanya kitu cha namna hiyo, huu uwanja una ulinzi mkubwa sana na siyo uwanja tu hili eneo lote lipo chini ya usimamizi mkubwa na makini,” alisema Mpuche.

“Ni kweli tumeona juzi hilo limetokea kwa timu ngeni kukimbia kutumia vyumba vya uwanja, lakini hadi tunavyoongea hakuna ambaye amekuja kutulalamikia lolote kuhusu hilo, tunasikia tu huko nje, kawaida timu zote ikifika saa tatu asubuhi ile siku ya mechi tunatoa funguo za vyumba kwa kila timu kwa maafisa wake ili wajipangie kila kitu.

“Huu uwanja wetu ukisema wanaweka dawa kwenye kiyoyozi kuna njia ya feni unaweza kuacha kutumia kiyoyozi na ukatumia feni lakini kama ukifika hapa utajionea madirisha ya uwanja wetu ni makubwa sana kuanzia futi sita hadi saba, ni vigumu kuwaathiri wachezaji kama hata mtafungua madirisha endapo hayo mambo yangekuwa yanafanyika lakini ukweli ni hakuna uwezekano wa hayo mambo kufanyika hapa.”

Uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini shida hiyo inatokea katika mechi mbalimbali za mashindano ya ndani na zipo mechi za kimataifa hali hiyo imekuwa ikijitokeza kwa klabu kulalamikia hilo.

“Haya mambo yapo, najua hakuna kiongozi wa klabu anaweza kuliongelea hili kwa kina, lakini mambo haya yanafanyika kwa viwanja vyetu na mashindano yote, hii ligi yetu na hata mechi za kimataifa,”  alisema mmoja wa viongozi wa klabu moja kongwe nchini.

“Unajua mpira wetu bado uko nyuma, wakati wenzetu wakiondoka huku, sisi ndio tumeyapokea na yanashamiri, zilianza klabu zetu kubwa na sasa hata klabu ndogo nazo zinapigana dawa kama kawaida katika harakati za kutafuta matokeo.”

SIMBA INASEMAJE?

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally akizungumzia hilo alisema ishu ya kupuliziana dawa ni tuhuma zinazotoka kwenye klabu mbalimbali ambazo zimekuwa zikiongeza taharuki kwa timu ngeni katika mechi za mashindano mbalimbali.

“Sina uhakika sana kama hayo mambo yapo hasa kwa ligi zetu za ndani ingawa ni kweli hayo mambo yapo na yanazungumzwa sana, ukiwa unakwenda kucheza mechi hasa ukiwa timu ngeni utazisikia sana hadi zitakufanya unakosa amani na kuamua kuchukua tahadhari na kukosa imani na ile timu mwenyeji wako,” alisema Ahmed.

“Unajua hadi sasa shida imekuwa unakosa kitu cha kupima kweli kwenye hiki chumba hii harufu ninayoisikia ni sumu, vipimo hivyo tumekuwa tukikosa lakini mazingira ya kukuta harufu yamekuwa yapo, sasa kuanzia hapo inabaki kuwa hisia tu.”

Ahmed alisema kuondoa hali hii ni wakati wa mamlaka kukaribisha utoaji wa ushahidi, pia kutafutwa vifaa maalumu vya kugundua kama hizo taarifa zinapokuwa zinatolewa na klabu tofauti kama zina ukweli.

“Haya mambo yamebaki huku kwetu, ukimfanyia vitu kama hivyo klabu kubwa kama Al Ahly atakuja kwenye chumba chako, atapima akiona ni kweli umefanya mambo, atachukua tahadhari au atakula dawa, mkienda uwanjani atakupigia mpira mwingi kama kawaida.

“Huku kwetu ukisikia hivyo basi utapambana kivyako, unaweza kufungulia mabomba ya maji kwenye masinki ya kunawia au utafungua milango, mnaweza kudeki kabisa hicho chumba au ili usiiingie kwenye mtego.”

AZAM HAWA HAPA

Makamu wa Rais wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amekiri suala la upuliziaji dawa lipo kwenye mechi za Ligi Kuu Bara na kikosi chao kimewahi kukutana mara tofauti na hali hiyo kwenye mechi zake.

“Watu wanakataa kutumia vyumba kwa sababu ya ishu ya kupuliziana dawa vyumbani, sisi tumekutana nayo hayo mambo mara nyingi tu, tumeshaumizwa sana lakini sio kwamba tumekuwa hatutoi taarifa, tumekuwa tukikutana na hii hali tunawaita wasimamizi na wanaona kabisa hali halisi,” alisema Popat.

“Kuna mechi tulicheza na timu (anaitaja) wakati tunafika uwanjani tu, tulikutana na hayo mambo, tukawaita wasimamizi wa mchezo na viongozi wa uwanja wakajionea hali halisi, ilikuwa huwezi kuingiza wachezaji wako mule.

“Acha mechi hiyo, kuna mchezo mwingine tulifungwa na timu (anaitaja timu nyingine kubwa), walitufunga mabao matatu kipindi cha pili, karudie ile mechi utaiona, angalia wachezaji wetu walivyocheza kipindi cha kwanza na walivyocheza kipindi cha pili, hicho kipindi cha pili mpaka penalti tulikosa hayo yote yametutokea hapa hapa Dar es Salaam, kwa hiyo hayo mambo yapo.”

WASIKIE YANGA

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo akizungumzia hilo alisema timu yao imekuwa ikikimbia kutumia chumba katika kuchukua tahadhari juu ya tuhuma za kupuliziana dawa vyumbani.

“Ni kweli tumekuwa tunatumia vyumba tofauti, unajua sisi ni viongozi na hizi ni klabu za wanachama nadhani hujawahi kuona sisi viongozi tukiongoza misafara ya timu kwenda uwanjani, mara nyingi unakuta wanachama wetu ndio wanatangulia na wakiona kuna dalili ya mambo hawayaelewi hasa kupuliziana dawa watasema hawataki timu iiingie hapo,” alisema Gumbo.

“Umati ule unakuwa ni vigumu kuwabishia ukizingatia wenzako walikuwa hapo kabla kwa hiyo ni tuhuma, hadi sasa ni hisia tu hakujapatikana ushahidi sahihi kuthibitisha hii unayosikia ni sumu kweli, nadhani ni wakati wa wenye mpira wao wakae chini na klabu zote, kulipatia ufumbuzi hili, unajua mataifa mengi haya mambo yameshapitwa na wakati wamebaki huku kwetu.”

KAGERA YAMEWAKUTA

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kagera Sugar inayoshiriki Ligi ya Championship, Ramadhan Kalula alisema ukiondoa imani za kishirikina, klabu zimekuwa zikikimbia kutumia vyumba vya kubadilishia nguo viwanjani kutokana na mambo ya kupuliziana dawa.

“Kuna mambo mawili, kwanza ni imani za kishirikina lakini la pili na kubwa ni mambo ya kupuliziana dawa, kuna wakati unaweza kuona kama hisia tu lakini ukweli hata sisi Kagera Sugar limewahi kutukumba wakati tukiwa ligi kuu,” alisema Kalula.

“Hizo mechi wachezaji wetu walichoka sana kuliko kawaida, wakati wa mapumziko tulikutana na mambo siyo mazuri, wachezaji wengi kulalamika misuli imewabana wengine wanakuwa na uchovu mkubwa na tulipoteza hiyo mechi kwa hiyo hayo mambo yapo na yanaumiza kwa kweli.”

TFF HAWA HAPA

Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), James Mhagama alisema wamekuwa wakisikia ishu hizo.

Mhagama alisema masuala hayo yanaegemea kwenye imani na tuhuma na imekuwa vigumu kuthibitisha lakini watakuja na uamuzi mzito juu ya masuala hayo.

“Ni kweli tunasikia hayo mambo, hakuna ambaye hasikii lakini unajua hizi ni tuhuma na wanaojua ni wale wanaofanya vitendo hivyo na wale wanaofanyiwa,” alisema Mhagama.

“Itoshe kwa kusema tumeyasikia na tunayachukua kwa uzito mkubwa, tutakuja na maamuzi mazito juu ya haya yote wakati wowote kutoka sasa.”

MSIKIE DAKTARI

Akizungumza na Mwanaspoti, Dokta Shita Samwel, alisema: “Sumu au kitu kinachoweza kumdhuru mwanadamu kinaweza kuwa katika mtindo wa gesi, kimiminika kinachoweza kuyeyuka haraka na kuwa hewa, au maji au hali ya ugumu au poda poda, yaani hali ya ungaunga.

“Vitu ambavyo ni sumu kwa mwili vinaweza kuingia kwa njia ya hewa, ngozi, kinywa au njia ya mishipa na mwilini vinaweza kuleta madhara ya hapo kwa hapo kwa muda mfupi au madhara ya baadaye kwa muda mrefu.

“Sumu hewa ambayo ni hatari inayoweza kumuua mwanadamu ni hewa ya ‘carbon monoxide’. Hii inatokana na vitu vinavyoungua kama vile mkaa na mafuta.

“Pia zipo sumu au viambata vyenye kuleta madhara vinaweza si kwa kupulizia, bali hata kupakazwa na mtu akagusana navyo akapata madhara, lakini kubwa na la haraka pia kama vyakula vinaweza kugusana na vitu vyenye sumu na kuleta madhara. Mara nyingi ni dawa na mimea, Insecticides za kupulizia, za kuulia wadudu.

“Pia kuna baadhi ya dawa za kupulizia kwa ajili ya maumivu ya nje ya mwili katika misuli, kwa bahati mbaya au mtu akigeuza matumizi, mtu akivuta dawa hizo za kupulizia zinaweza kumsababishia kulegea, kukosa nguvu na kulal. Pia zinaweza kusababisha kasi ya moyo kuwa juu na kudunda ovyo na kifo kinaweza kutokea.”

Kuhusu dalili za mtu ambaye ameathirika na sumu, Dokta Shita alisema: “Dalili zake ni kushindwa kupumua vizuri, kutapika, kichefuchefu, hali ya kuweweseka, kupoteza fahamu, kichwa kuuma, kizunguzungu, mwili kulegea, maumivu ya tumbo na kuharisha.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *