
Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetenga Sh5.397 bilioni kujenga nyumba ya makazi ya Makamu wa Pili wa Rais kisiwani Pemba.
Mradi wa ujenzi wa nyumba ya makazi ya Makamu wa Pili wa Rais,Tibirinzi Pemba umeanzishwa kwa lengo la kuimarisha na kuweka mazingira mazuri ya makazi ya Makamu wa Pili wa Rais ili kuwa na makazi yanayoendana na hadhi yake.
Hayo yameelezwa leo Mei 11, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu Dk Saada Mkuya wakati wa kipindi cha maswali na majibu katika Mkutano wa 11 wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, Nguja Zanzibar.
Dk Saada alikuwa akijibu swali la mwakilishi wa Chambani, Mahmoud Shineni Ali (CCM) aliyetaka kujua mpango wa Serikali katika kuboresha makazi ya viongozi wa kitaifa katika Kisiwa cha Pemba na mradi wa ujenzi na maboresho ya Ikulu ya Tibirinzi Pemba umegharimu kiasi gani cha fedha.
Akijibu swali hilo la msingi, Dk Saada amesema mradi huo ulianza rasmi Mei 2025 na umepangwa kukamilika Novemba, 2026 ikiwa ni miezi 18.
“Ujenzi huu unahusisha jengo kuu la makazi lenye ghorofa mbili pamoja na majengo saidizi. Hatua ya ujenzi iliyofikiwa hadi Machi, 2026 ni asilimia 58 ya utekelezaji halisi wa kazi,” amesema Dk Saada.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, mradi huo unaokisiwa kutumia Sh5.397 bilioni pamoja na Ongezeko la Thamani (VAT), kiasi cha fedha kilicholipwa hadi Machi, 2026 ni Sh2.932 bilioni ikiwa ni asilimia 54 ya fedha iliyopangwa kwa mradi mzima.
Amesema katika mpango wa Serikali wa kutambua umuhimu wa kuwa na makazi bora na yenye hadhi kwa viongozi wa kitaifa ili kuwawzesha kutekelza majukumu yao, Serikali inaendela kuimarisha makazi yaliyopo kufanya tathmini za mara kwa mara pamoja na matengenzo ya msingi na uendelezaji wa miundombinu muhimu kama maji, umeme na mawasiliano.
Lengo ni kuhakikisha ubora, usalama na matumizi sahihi ya majengo yanaendelea kudumishwa.