Dar es Salaam. Hatimaye uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam umefanya ukaguzi wa Barabara ya Bima–Kimanga, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikilalamikiwa na wananchi kutokana na ubovu wake, huku ukiahidi kuanza haraka kazi ya ujenzi na ukarabati.

Ziara hiyo iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala pamoja na Mkurugenzi wa Jiji, imefanyika siku mbili baada ya baadhi ya wamiliki wa daladala zinazotoa huduma katika barabara hiyo kutishia kugoma, wakishinikiza mamlaka kuchukua hatua za haraka kurekebisha miundombinu hiyo.

Barabara hiyo inayotumiwa na wakazi wa Kimanga kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi imekuwa katika hali mbaya kwa muda mrefu, hasa kipindi hiki cha mvua hasa eneo la takribani mita 700 kuanzia darajani hadi Mawezi.

Eneo hilo limejaa mashimo makubwa ambayo hufurika maji kipindi cha mvua na kusababisha usumbufu kwa watembea kwa miguu, bodaboda na magari.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo leo Mei 12,2026  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala, Elihuruma Mabelya, amesema changamoto ya mashimo katika Barabara ya Tabata Kimanga imekuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi, hususan katika kipande hicho korofi cha mita 700.

“Halmashauri tayari imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji na uboreshaji wa miundombinu hiyo. Kwa maelekezo ya mkuu wa wilaya, tayari mkandarasi amekabidhiwa eneo hili ili kuanza kazi usiku wa leo,” amesema Mabelya.

Amesema ukarabati huo unalenga kuhakikisha wananchi pamoja na vyombo vya usafiri wanapata huduma bora ya usafiri na kurahisisha shughuli za kila siku za usafirishaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema Serikali tayari imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kipande hicho kwa kiwango cha zege kuanzia darajani hadi eneo la Mawenzi

“Tumetoa maelekezo ya kuondolewa kwa kifusi, mawe na zege zilizowekwa ili kupisha shughuli ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha zege kuanza mara moja,” amesema Mpogolo.

Amesema Halmashauri imetenga Sh1.7 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa zaidi ya mita 400 za barabara hiyo, na zingine huku akibainisha kuwa ndani ya muda mfupi wananchi wataanza kuona mabadiliko makubwa ya miundombinu hiyo.

“Tunaomba wananchi wa Kimanga na Tabata wawe na subira. Ndani ya mwezi huu hali ya barabara itakuwa imeimarika, na kuanzia kesho wananchi wataanza kuona matokeo ya kazi ya mkandarasi,” amesema.

Aidha Mpogolo ameiagiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), kusimamia kwa karibu matumizi ya barabara hiyo na kuhakikisha magari yenye uzito mkubwa hayaharibu miundombinu inayojengwa.

“Haiwezekani gari ya tani 50 lipite kwenye barabara yenye uwezo wa kupitisha tani 30. Tutakuja kuharibu barabara hizi kutokana na magari yanayosafirisha mchanga kupita kiwango kinachoruhusiwa,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *