
Nchini Uganda, baada ya kutangazwa mshindi kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Januari, rais Yoweri Museveni anaapishwa leo, kuongoza nchi hiyo kwa muhula wa saba, baada ya kuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 40.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Wakati Jenerali Yoweri Museveni akijiandaa kuchukua kiapo wadau mbalimbali wametoa maoni yao kuhusu yaliyo mbele katika miaka mitano huku wengine wakimshauri kuhusu wanachokiona anapaswa kuzingatia.
Dkt Robert Ojambo ni mchambuzi wa Kisiasa na mhadhiri katika chuo kikuu cha Kyambogo anatoa wito kwa Rais Museveni.
“Amefanya kazi kubwa kuendeleza nchi yetu na tunamshukuru lakini ni wakati umefika anastahili kusema ni lazima niwaachie mtu mwengine hii kazi.” Amesema Dkt Robert Ojambo.
Katika tamko lake la uchaguzi, Jenerali Museveni aliahidi mabadiliko ya haraka ya nchi na kulinda kile kilichoafikiwa lakini mtetezi wa haki za kibinadamu na pia mwangalizi wa siasa Timothy Chemonges anasema kuwa raia wa Uganda hawafai kutarajia mabadiliko mengi.
“Kwa upande wangu sioni tofauti kubwa sana katika muhula wake mwengine.” Amesema Timothy Chemonges.
Mwanauchumi kutoka chama tawala NRM Stephen Mukitale Birahwa pia amemshauri Jenerali Museveni kuhusu changamoto nyingi za kiuchumi.
“Sisi tunataka mambo ya maendeleo, tunataka kuona biashara zikiendelea na watu wakipata pesa.” Ameeleza Stephen Mukitale.
Sherehe ya kuapisha Jenerali Yoweri Museveni itafanyika kwenye Uwanja wa Kololo hapa mjini Kampala. Serikali imetangaza siku ya likizo ya umma kwa wanainchi wanaotaka kusherehekea.
Kenneth Lukwago, Kampala, RFI Kiswahili