Dar es Salaam. Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) imeanzisha mfuko maalumu wenye thamani ya zaidi ya Sh34 bilioni kwa ajili ya kusaidia biashara zinazoongozwa na vijana na wanawake ukanda wa Afrika Mashariki.

Mfuko huo, wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 13 sawa na takribani Sh34.5 bilioni, umetangazwa wakati wa kikao cha Baraza la Uongozi la benki hiyo kilichofanyika jijini Kampala nchini Uganda, mwanzoni mwa wiki hii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa EADB wa mwaka 2024 hadi 2028.

Hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha kwa makundi maalum ya kijamii huku ikichochea ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Taarifa hiyo imekuja sambamba na taarifa ya mafanikio makubwa ya kifedha ya benki hiyo kwa mwaka ulioishia Desemba 2025, ambapo faida kabla ya kodi iliongezeka kwa asilimia 51 na kufikia zaidi ya Sh44.8 bilioni kutoka Sh29.6 bilioni zilizorekodiwa mwaka uliotangulia.

Aidha, EADB ilieleza kiwango cha mikopo iliyotolewa kiliongezeka kwa asilimia 140, huku mikopo ambayo haijalipwa hadi mwisho wa mwaka ikiongezeka kwa asilimia 52, jambo lililotafsiriwa kama kuongezeka kwa shughuli za uwekezaji na upanuzi wa huduma za kifedha katika ukanda huo.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Baraza la Uongozi la EADB ambaye pia ni Waziri wa Fedha wa Uganda, Matia Kasaija, alisema mafanikio hayo yametokana na uwezo wa benki hiyo kuhamasisha rasilimali na kutoa suluhisho bunifu za kifedha katika sekta mbalimbali.

“Mafanikio haya ni ushahidi wa uwezo ulioimarika wa EADB katika kuhamasisha rasilimali na kusaidia utekelezaji wa miradi muhimu katika nchi wanachama wetu,” alisema Kasaija.

Alisema mfuko huo mpya unaonyesha namna benki hiyo inavyotambua nafasi ya vijana na wanawake katika kukuza ubunifu, ajira na maendeleo ya kijamii ndani ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Kasaija, fedha hizo zitatolewa kupitia taasisi za kifedha washirika wa EADB ili kuhakikisha zinawafikia walengwa kwa ufanisi zaidi.

“Tunatambua vijana na wanawake ni nguvu muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Afrika Mashariki. Kupitia mfuko huu tunalenga kusaidia biashara zao kwa mikopo na huduma maalum za kifedha,” amesema.

Katika kikao hicho, Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi wa Rwanda, Yusuf Murangwa, alithibitishwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Uongozi la EADB akichukua nafasi ya Kasaija.

Pia, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ya Uganda, Dk Ramathan Ggoobi, aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kwa kipindi cha miaka miwili akimrithi Dk Natu Mwamba wa Tanzania.

EADB ilianzishwa mwaka 1967 chini ya Mkataba wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikiwa na jukumu la kusaidia miradi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika ukanda huo. Kwa sasa, benki hiyo inamilikiwa kwa pamoja na nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda pamoja na taasisi mbalimbali za maendeleo za kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *