Dar es Salaam. Baada ya zaidi ya miaka mitatu ya vita vilivyoitikisa Ulaya Mashariki, hatimaye kuna ishara ambazo wachambuzi wa siasa wanazitafsiri kama hatua za mwanzo kuelekea kupungua kwa mvutano kati ya Urusi na Ukraine.

Wiki hii, Urusi ilitangaza kusitisha mashambulizi kwa siku tatu ili kupisha maadhimisho ya kumbukumbu ya Victory Day, ambayo hufanywa Mei 9, kila mwaka, kuadhimisha ushindi wa Soviet dhidi ya Ujerumani katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Ukraine nayo, licha ya kutokuwa sehemu ya maadhimisho hayo, ilionekana kupunguza mashambulizi katika kipindi hicho huku pande zote zikitupiana lawama za ukiukaji wa usitishaji huo wa mapigano.

Hatua hiyo, imezua mjadala kuhusu iwapo huo ndio mwanzo wa safari ya kuelekea mwisho wa vita hiyo iliyogharimu maelfu ya maisha, kuharibu uchumi wa nchi hizo mbili na kuutikisa mfumo wa kisiasa na kiusalama duniani.

Wachambuzi wengi wanaona nyuma ya tamko hilo la kusitisha mapigano kuna hali ya uchovu wa kivita, gharama za kiuchumi, shinikizo la kisiasa na mabadiliko ya nguvu za kimataifa yanayoanza kuzisukuma pande zote kutafuta njia ya kutoka kwenye mgogoro huo.

Wachambuzi

Akizungumzia hilo, Mchambuzi wa siasa za kimataifa, Leonard Mvungi, anasema dalili ya kwanza ya kumalizika kwa vita hiyo ni mabadiliko ya lugha za viongozi wa pande zote mbili.

Anaeleza kwa miezi mingi viongozi wa Urusi na Ukraine walikuwa wakizungumza kwa misimamo migumu isiyoonyesha nafasi ya mazungumzo, lakini sasa kauli zimeanza kubeba ishara za kulegea.

“Katika vita nyingi duniani, mwisho wake hauanzi kwa kutiwa saini mkataba wa amani. Huanzia kwenye mabadiliko ya lugha za viongozi. Ukiona pande mbili zinaanza kuzungumza kuhusu usalama haya yote yameanza, ujue mlango wa mazungumzo umeanza kufunguliwa,” anasema.

Anasema Urusi imeingia kwenye kipindi kigumu kiuchumi kutokana na vikwazo vya muda mrefu kutoka mataifa ya Magharibi huku Ukraine nayo ikianza kuathiriwa na uchovu wa misaada kutoka kwa washirika wake.

Kwa mujibu wake, mataifa yanayoifadhili Ukraine yameanza kuelekeza nguvu kwenye changamoto nyingine za kiusalama duniani hali inayopunguza kasi ya msaada wa kijeshi iliyokuwa ikitolewa awali.

“Vita huwa zina mwisho pale gharama zake zinapozidi uwezo wa kisiasa. Leo Urusi inahitaji uthabiti wa uchumi wake wa ndani, wakati Ukraine inahitaji kurejesha miundombinu na wananchi wake. Hakuna upande unaoweza kuendelea na kasi ileile ya mwanzo,” anasisitiza.

Kwa upande wake, Mchambuzi wa Siasa za Kimataifa, Profesa Elias Kiwale, anaamini kusitishwa kwa mapigano kwa siku tatu si jambo la kawaida bali ni jaribio la kupima mazingira ya mazungumzo.

Anaeleza kuwa katika migogoro mingi duniani, hatua ndogo kama hizo hutumiwa kuangalia uwezo wa majeshi kujizuia na kutathmini mwitikio wa jamii ya kimataifa.

“Kama pande zinazopigana haziwezi hata kusimamisha mapigano kwa saa 24, basi mazungumzo huwa magumu zaidi. Lakini ukiwaona wanakubaliana kimyakimya kupunguza mashambulizi kwa siku kadhaa, hiyo ni dalili kuwa kuna mawasiliano ya chini kwa chini yanaendelea,” anasema.

Anasema Marekani na mataifa ya Ulaya yanaonekana pia kutafuta suluhisho la kidiplomasia zaidi kuliko mwendelezo wa vita.

Anaeleza uchaguzi unaokuja katika baadhi ya mataifa ya Magharibi umeanza kufanya viongozi wao kufikiria gharama za kuendelea kuifadhili vita hiyo kwa kiwango kikubwa.

“Wananchi wa Ulaya wanataka kuona mwisho wa mfumuko wa bei wa nishati, wakati Marekani nayo ina changamoto nyingi za ndani. Shinikizo la kisiasa linaanza kubadilisha namna mataifa hayo yanavyoitazama vita hii,” anafafanua.

Profesa Kiwale anaamini hata Urusi yenyewe imeanza kuelewa kuwa ushindi wa kijeshi wa moja kwa moja unaweza kuchukua muda mrefu sana.

“Ndiyo maana sasa tunaona diplomasia ikianza kupata nafasi ambayo kwa muda mrefu ilikuwa imefungwa na milio ya makombora,” anasema.

Profesa Kiwale anasema Afrika itanufaika zaidi kisiasa na kidiplomasia iwapo vita hiyo itafikia mwisho.

Anafafanua kwa sasa dunia imegawanyika katika misimamo mikali kuhusu mgogoro huo jambo ambalo limeziweka baadhi ya nchi za Afrika kwenye wakati mgumu wa kisiasa kati ya Mashariki na Magharibi.

“Afrika imejikuta ikibeba shinikizo la kijiografia ambalo haihusiani nalo. Mwisho wa vita utapunguza mgawanyiko wa kimataifa na kuipa Afrika nafasi nzuri ya kushirikiana kiuchumi na pande zote bila presha kubwa za kisiasa,” anasema.

Anaongeza kuwa utulivu wa kimataifa pia unaweza kusaidia kupungua kwa gharama za mikopo na kuongeza utulivu wa masoko ya fedha duniani, hali itakayosaidia nchi nyingi za Afrika zinazokabiliwa na madeni makubwa.

Mchambuzi mwingine wa siasa za kimataifa, Said Majjid, anasema dalili nyingine muhimu ni uchovu wa wananchi ndani ya nchi hizo mbili.

Anaeleza vita vya muda mrefu huwa na athari kubwa za kijamii ambazo mwanzoni hazionekani kwa haraka, lakini kadri muda unavyokwenda, shinikizo la wananchi huanza kuathiri maamuzi ya kisiasa.

“Leo kuna maelfu ya familia zilizopoteza ndugu, mamilioni ya wakimbizi na kizazi cha vijana kilichokulia kwenye hofu ya vita. Serikali zinaweza kuhimili silaha, lakini ni vigumu kuhimili uchovu wa wananchi,” anasema.

Anasema hata ndani ya Urusi ambako Serikali imeendelea kuonyesha uimara wa kisiasa, kuna dalili za wananchi kutaka maisha ya kawaida kurejea.

Ukraine nayo imeendelea kuishi katika mazingira magumu ya mashambulizi ya mara kwa mara, hali inayoongeza kiu ya kuona suluhisho la kudumu.

“Vita vinapoanza, uzalendo huwa mkubwa. Lakini vikichukua miaka mingi, wananchi huanza kuuliza mwisho wake. Hilo ndilo swali linaloanza kusikika sasa katika pande zote mbili,” anasema.

Anasema dunia pia imeanza kuhamia kwenye siasa za uchovu wa migogoro, ambapo mataifa mengi yanataka kuona nguvu zikielekezwa kwenye uchumi, biashara na changamoto za maendeleo badala ya vita vya muda mrefu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *