Geita. Kukamilika kwa ujenzi wa jengo la biashara la Gedeco Tower linalojengwa katika Kata ya Kalangalala, Manispaa ya Geita, kunatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi na wafanyabiashara sambamba na kuongeza mapato ya halmashauri hiyo.

Mradi huo wa ghorofa nane unatarajiwa kugharimu Sh13 bilioni zitokanazo na mapato ya ndani ya Manispaa ya Geita.

Hadi sasa, halmashauri hiyo imetenga Sh7 bilioni kwa awamu ya kwanza ya utekelezaji huku mradi ukiwa umefikia asilimia 12.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba akizungumza na waandishi wa habari alipokagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la kitegauchumi la ghorofa nane, The Gedeco Tower mkoani Geita.

Akizungumza Mei 13, 2026 wakati akikagua maendeleo ya mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba amesema jengo hilo litasaidia kusogeza huduma za kisasa karibu na wananchi, kuongeza fursa za ajira pamoja na kuboresha mandhari ya mji wa Geita.

“Halmashauri imeamua kujenga jengo kubwa litakalowezesha upatikanaji wa huduma za kisasa katika mji wetu. Wanachi watapata huduma bora ambazo awali walilazimika kuzifuata katika miji mingine mikubwa,” amesema Komba.

Mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya Nusak Company Limited chini ya usimamizi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Kwa mujibu wa taarifa za mradi huo, Gedeco Tower itakuwa na migahawa, kumbi kubwa na ndogo za mikutano, eneo la kuogelea, sehemu za mazoezi, ofisi, vyumba vya biashara pamoja na maeneo ya burudani. Mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu.

Mkurugenzi Manispaa ya Geita, Yefredi Myenzi akizungumzia maendeleo ya jengo la kitegauchumi la Ghorofa nane ‘Gedeco Tower’, linalojengwa Manispaa hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Geita, Yefred Myenzi amesema pamoja na mkoa huo kutegemea shughuli za uchimbaji madini, bado umekuwa ukikabiliwa na uhaba wa miundombinu ya kisasa ya biashara na huduma.

Amesema kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia kutoa nafasi kwa huduma mbalimbali ikiwemo biashara ya vito vya thamani na dhahabu.

“Tumetenga maeneo maalumu kwa ajili ya maduka ya kuuza vito na dhahabu kutoka kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini. Tunaamini mradi huu utakuwa suluhisho la changamoto za huduma za hoteli, biashara na burudani ambazo wananchi wamekuwa wakizikosa,” amesema Myenzi.

Aidha, amesema Manispaa ya Geita inatarajia kukusanya mapato ya kati ya Sh600 milioni hadi Sh700 milioni kila mwaka kupitia jengo hilo, sambamba na kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani kutoka Sh25 bilioni hadi Sh30 bilioni ndani ya miaka mitatu ijayo baada ya mradi kukamilika.

Baadhi ya fundi ujenzi wakiendelea na kazi katika jengo la kitega uchumi ‘Gedeco Tower’ linalojengwa katika kata ya Kalangalala, Manispaa ya Geita ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 12.

Meya wa Manispaa ya Geita, Leonard Bugomola, amesema baraza la madiwani limeendelea kushirikiana na ofisi ya mkurugenzi kuhakikisha ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya ndani unaimarishwa ili fedha hizo zitumike kutekeleza miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi.

Amesema tayari mradi huo umetoa zaidi ya nafasi 200 za ajira kwa wananchi wa eneo hilo.

Nao baadhi ya wafanyakazi wa mradi huo, akiwemo Zainabu Mahona na Edson Edward, wameishukuru Manispaa ya Geita kwa kuibua chanzo cha ajira zinazowasaidia kukidhi mahitaji yao ya kila siku kupitia ajira za muda mfupi na muda mrefu ziliz zilizotolewa na mradi huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *