
Kibaha. Wakazi wa Wilaya ya Mafia mkoani Pwani wameendelea kulalamikia changamoto ya usafiri wa majini kufuatia kuharibika kwa kivuko cha MV Kilindoni kilichosimamisha safari zake tangu Mei 12, 2026.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wamesema wamebaki wakitegemea majahazi na boti ndogo ambazo haziwezi kukidhi mahitaji ya usafiri kati ya Mafia, Nyamisati na Dar es Salaam.
Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa) Mkoa wa Pwani, Alvina Bushunda amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo akisema kivuko hicho kinafanyiwa matengenezo na huduma zitarejea mara baada ya ukarabati kukamilika.
“Spea zote zipo na mafundi wanaendelea kufanya matengenezo, hivyo wakati wowote kivuko kitakamilika na huduma kurejea,” amesema.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi, mkazi wa Kilindoni, Faki Sosi, amesema changamoto ya usafiri katika Wilaya ya Mafia imekuwa ya muda mrefu na imeendelea kuathiri shughuli za wananchi wanaotegemea usafiri wa baharini.
“Wananchi wa Mafia hatuna mbadala wa usafiri, lazima tusafiri kwa njia ya bahari. Lakini kuharibika mara kwa mara kwa kivuko chetu cha MV Kilindoni kunaonyesha ipo haja ya Serikali kufungua milango kwa wawekezaji kusaidia sekta hii,” amesema Faki.
Amesema kuna umuhimu wa kuanzishwa kwa huduma za ‘spidi boti’ ili kupunguza adha ya safari ndefu na kuongeza uhakika wa usafiri kwa wananchi wa Mafia.
Faki ameongeza kuwa usafiri wa sasa wa meli unatumia muda mrefu tofauti na mahitaji ya wananchi wengi wanaosafiri kwenda Dar es Salaam.
“Meli inatumia karibu saa tano kwa safari ambayo ingeweza kuchukua saa moja na nusu kwa kutumia usafiri wa kisasa zaidi. Serikali ione umuhimu wa kuwaruhusu wawekezaji katika eneo hili,” amesema.
Mkazi mwingine, Dad Karimu Mohammed Hassan, amesema kwa sasa wananchi wanalazimika kutumia majahazi na boti ndogo ambazo hazitoshelezi mahitaji ya usafiri.
“Tunaiomba Serikali ifanye jitihada za haraka kukarabati kivuko hiki ili wananchi waendelee kupata huduma ya usafiri kwa usalama,” amesema.
Naye Omary Kipemba amesema ni muhimu Serikali kuangalia uwezekano wa kurejesha huduma ya usafiri ya MV Songosongo ambayo imesimama kwa muda mrefu bila kutoa huduma.
“MV Songosongo nayo inaweza kusaidia kupunguza changamoto ya usafiri kwa wananchi wa Mafia kama itarejeshwa kutoa huduma,” amesema.