Morogoro. Baadhi ya wamiliki wa shule za msingi na sekondari binafsi wamesema huenda wakaongeza gharama za usafiri kwa wanafunzi wanaotumia mabasi ya shule hizo iwapo bei ya mafuta itaendelea kuwa juu katika miezi ya Mei na Juni.

Wamesema ongezeko la bei ya mafuta limeongeza gharama za uendeshaji wa shule, hasa katika huduma ya usafiri wa wanafunzi, hali inayowalazimu kutafakari upya viwango vya malipo vinavyotozwa kwa wazazi.

Akizungumzia changamoto hiyo, mmiliki wa Shule ya Awali na Msingi Patricia, Selestine Mbilinyi amesema tangu kupanda kwa bei ya mafuta shule yake imekuwa ikitumia fedha nyingi zaidi kwa ajili ya kuendesha mabasi ya shule.

“Kwa sasa huduma hii tunaitoa kwa hasara kwa sababu fedha wanazolipa wazazi hazitoshi kununua mafuta. Tunalazimika kutafuta fedha sehemu nyingine ili kuongeza mafuta,” amesema.

Amesema iwapo hali hiyo itaendelea hadi mwezi Juni, shule italazimika kutangaza viwango vipya vya usafiri mwezi Julai wakati wa kufungua muhula mpya.

Mbilinyi amesema kwa sasa hawawezi kuongeza gharama hizo kwa sababu baadhi ya wazazi tayari walishalipia huduma ya usafiri, huku akieleza kuwa si busara kufanya mabadiliko hayo kipindi hiki ambacho shule zinakaribia kufungwa.

“Fedha tunayotumia kununua mafuta kwa siku imeongezeka mara mbili huku wazazi wakilipa kiwango kilekile. Kupitia vikao vya wazazi tutakubaliana kiwango kitakachofaa ili shule isipate hasara na mzazi asiathirike sana,” amesema.

Mmiliki wa shule binafsi ya msingi ya A Plus, Seif Chomoka, amesema kwa sasa analazimika kutumia busara licha ya kuwa huduma hiyo imekuwa ya hasara kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta.

“Wapo baadhi ya wamiliki wa shule ambao tayari wameongeza gharama za usafiri, lakini mimi nimeamua kusubiri kuona hali itakuwaje. Ikiendelea hivi, nami nitalazimika kuongeza,” amesema Chomoka.

Baadhi ya wazazi wamezitaka shule hizo kutafuta njia mbadala za kupunguza gharama badala ya kuongeza malipo ya usafiri.

Mmoja wa wazazi hao, Esther Mgonja, amesema shule zinaweza kushirikiana na wazazi kwa kupanga maeneo maalumu ya kukusanyia watoto badala ya mabasi kufuata kila mwanafunzi nyumbani kwake.

“Watoto wa eneo moja wanaweza kukusanywa sehemu moja ili basi liwachukue kwa pamoja. Hii itasaidia kupunguza mizunguko ya mabasi na matumizi ya mafuta,” amesema.

Amesema iwapo gharama za usafiri zitapandishwa zaidi, baadhi ya wazazi watalazimika kuwahamishia watoto wao katika shule za umma.

Wakati huohuo, baadhi ya wafanyabiashara wa baiskeli wamesema biashara hiyo imeanza kuongezeka kutokana na wazazi wengi kuanza kuwanunulia watoto wao baiskeli kwa ajili ya kwenda shule.

Mmoja wa wazazi aliyejitambulisha kwa jina la Gift Joachim amesema amelazimika kununua baiskeli kwa watoto wake wawili baada ya shule wanayosoma kuongeza gharama za usafiri kwa asilimia 50.

“Awali nilikuwa nalipa Sh60,000 kwa kila mtoto, lakini sasa nimetakiwa kulipa Sh90,000 kwa kila mmoja. Hiyo ni Sh180,000 kwa mwezi, siwezi kumudu, ndiyo maana nimeamua kununua baiskeli,” amesema Joachim.

Aidha, baadhi ya wazazi wameanza kuwazoesha watoto wao kutumia daladala kama njia mbadala ya usafiri kuelekea shule, wakijiandaa na uwezekano wa kupanda kwa gharama za usafiri kuanzia Julai mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *