Dar es Salaam. Hali ya vifo vya wajawazito katika Mkoa wa Dar es Salaa vimepungua kutoka vifo 72 vilivyokuwa vinaripotiwa katika robo mwaka ya 2021/2022 hadi kufika vifo 30 katika robo mwaka mwaka ya 2025/2026.
Huku vifo vya watoto katika kipindi hicho vikipungua kutoka watoto 500 mpaka 600 hadi kufika watoto 300.
Takwimu zinaonyesha kwa siku katika mkoa huo watoto 500 huzaliwa katika vituo vinavyomilikiwa na serikali, hali inayoonyesha uhitaji mkubwa wa utoaji wa huduma.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Mohamed Mang’una, katika mkutano wa kutambulisha mradi unaohusu uboreshaji wa afya ya mtoto katika Mkoa wa Dar es Salaam unaoenda sambamba na uboreshaji wa afya ya mama unaosimamiwa na hospitali ya CCBRT.
Dk Mang’una amesema hali hiyo inatokana na serikali kuendelea kuboresha sekta ya afya ikiwemo kufanya upanuzi wa vituo vyake vya afya na kuongeza vifaa na watumishi.
“Huko nyuma tulikuwa na changamoto ya kuripoti vifo vingi vya wamama wajawazito na watoto katika taarifa zetu, lakini kutokana na serikali kujitahidi kuboresha huduma zake za afya ndio maana takwimu hizo za vifo kwa sasa zinazidi kushuka.
Amesema kwa siku katika Mkoa wa Dar es Salaam watoto 500 huzaliwa katika vituo vinavyomilikiwa na serikali, hali inayoonyesha uhitaji mkubwa wa utoaji wa huduma.
Pamoja na mafanikio hayo, Mganga huyo amesema upande wa watoto bado hawajafanya vizuri hasa wanaoanzia umri wa siku 0 hadi siku 28 na kubainisha kuwa mradi wa programu hiyo utasaidia kuendeleza juhudi za kupambana na vifo hivyo.
Kwa mujibu wa Dk Mang’una vifo vinavyotokea kwa watoto husababishwa na tatizo la upumuaji kunakochangiwa na mama kupata mimba pingamizi au mtoto kuzaliwa kabla ya muda, kunakomfanya kutoka tumboni mapafu yakiwa bado hayajakomaa.
Hata hivyo amesema ujio wa mradi huo unaolenga kuongeza ujuzi wa kitaaluma kwa watumishi na unaoendana na mwongozo wa Wizara ya Afya ambao wanatakiwa waupate ili kuweza kutoa huduma vizuri kwa watoto, na kumsaidia mama katika hatua ya ujauzito hadi pale atakapojifungua,” amefafanua.
“Pia utasaidia kuwezesha vituo vya afya kufanya ufuatiliaji ikiwemo vifo kujua sababu na kutumia kama somo kuhakikisha havitokei tena huko siku za usoni,” amesema Mganga huyo.
Ameeleza kuwa mradi huo utafanya kazi katika vituo vya afya 32 kati ya 40 vya serikali vinavyotoa huduma ya mama na mtoto katika mkoa huo ikiwemo upasuaji.
Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Miradi na Utafiti kutoka CCBRT, Rhoda Ndakwe amesema mradi huo ulifandiliwa na mfuko wa “La caixa” ni wa mwaka mmoja na utagharimu zaidi ya Euro 200 (Sh600 milioni).
Rhoda amesema wanafanya hivyo ikiwa ni mwendelezo wa miradi ambayo walishawahi kuifanya hapo awali katika miaka 10 ya kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Hata hivyo amesema katika mkutano huo ameweza kukutana na wadau kutoka vituo 32, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, lengo likiwa ni kujadiliana namna ya kuutekeleza mradi huo.
“Nitumie nafasi hii kuwashukuru Mkoa walivyotupokea ninaamini kuwa tutapata matokeo mazuri bila kusahau mfadhili ambaye huu ni mradi wake wa kwanza kuuleta Tanzania na ninaahidi kwamba hatutamuangusha,” amesema Rhoda.
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa vituo vya afya, Kaimu Muuguzi Mkuu wa Manispaa ya Temeke, Magreth Pesambili amesema wameupokea mradi huo kwa mikono miwili kwa kuwa utawasaidia kuboresha huduma ya afya ya mama na mtoto na hasa kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.
“Tunashukuru kuletewa mradi huu kwani kama tulivyosikia katika mradi huu kutakuwa na afua mbalimbali zitakazofanyika kama vile mafunzo kwa watoa huduma, kuletewa vifaa na mafunzo katika vyumba vya upasuaji unaohusu mama mjamzito ili kuokoa maisha ya mama na mtoto,” amesema Magreth.