Mabao mawili yaliyofungwa katika dakika za mwisho  yametosha kuipa ushindi Azam FC wa mabao 2-0 dhidi ya Pamba Jiji, leo usiku.

Dakika ya 90 na zile tatu za nyongeza zimetosha kuamua mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Ushindi huo unaifanya Azam kurudi njia ya ushindi baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya TRA United kwa mabao 4-1, ikifikisha pointi 46 kutokana na michezo 23 na kuifanya kuendelea kuganda katika nafasi ya tatu.

Ikionekana kama mchezo huo utamalizika kwa sukuhu, lakini Azam imepata bao dakika ya 90 likifungwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ kwa kichwa akimalizia mpira wa kona uliopigwa na Idd Seleman ‘Nado’.

Bao hilo linamfanya Fei Toto kufunga la 11 msimu huu akiendelea kuwa kinara wa ufungaji kwa timu yake.

Wakati Pamba Jiji wakijiuliza, mshambuliaji Japhte Kitambala akaweka kambani bao la pili katika dakika ya tatu ya nyongeza kwa shuti kali na kukamilisha ushindi huo kwa Azam FC.

Kabla ya kupatikana kwa mabao hayo timu zote zilitengeneza mashambulizi mazuri, lakini kikwazo kilikuwa makipa wa timu zote mbili Mohammed Camara wa Pamba na Aishi Manula (Azam FC) ambao wamefanya kazi nzuri kuokoa.

Ushindi huo unaifanya Azam kuvuna pointi nne kwa Pamba msimu huu ambapo kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza timu hizo zilimaliza kwa sare ya kufungana mabao 2-2.

Pamba itajilaumu kwa kushindwa kuidhibiti Azam katika dakika za mwisho zilizoamua mchezo huo ikipoteza umakini kwenye mashambulizi  mawili yaliyoamua mechi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *