Nigeria. Tuzo za Africa Magic Viewers’ Choice Awards (AMVCA) 2026 zilijaa matukio mengi ya mitindo ya kuvutia. Moja ya tukio lililozua gumzo ni gauni lenye muundo wa kanisa kuu ‘Cathedrals Cologne’ lililovaliwa na gwiji wa mitindo kutoka Ghana, Nana Akua Addo.

Gauni hilo ambalo lilibuniwa na mbunifu wa Nigeria, Mohammed Abbas Ossu, lilitengenezwa kwa mfumo wa kanisa kuu kutoka Ujerumani. Muundo wake ukijumuisha minara mirefu (spires), matao ya Kigothi, milango, madirisha, nguzo na hata misalaba. Jambo lililopelekea vazi hilo kuwavutia mastaa wengi akiwemo Chioma Ikokwu, Adunni Ade pamoja na Mary Remmy Njoku.

Mbali na kupata pongezi na kuwavutia wengi, gauni hilo liliingia katika utata mkubwa ambapo jumba la mitindo jijini Paris ‘ALmée Couture’ walidai kuwa wameibiwa wazo lao la muundo huo wa gauni.

ALmee walichapisha mchoro wao wa gauni huku wakimshutumu Abbas kuwa mwizi, wakieleza kuwa hapo awali Nana aliifuata kampuni hiyo akitaka kutengenezewa gauni lenye muundo wa kanisa kuu. Ambapo ALmee walitengeneza mchoro, lakini hawakuweza kuendelea walisitisha makubaliano na walikubaliana kuwa Almee wangebaki na umiliki wa mchoro na ubunifu huo.

ALmée pia walifafanua kuwa hawadai umiliki wa wazo la kanisa lenyewe. Bali wanadai juhudi zao walizotumia katika kuchora mchoro huo na kubadilisha kuwa gauni, huku wakidai haki yao iliyotumika bila kupewa taarifa wala kushirikishwa.

Aidha kwa upande wa Nana alijibu tuhuma hizo akieleza, yeye ndio alitoa wazo hilo na kuwa ALmée walikataa kulitekeleza kama alivyoelekeza kutokana na ugumu. Hivyo akarejeshewa fedha na akaenda kwa mbunifu mwingine ambaye ni Abbas Woman na alifanikisha kulitengeneza kama ambavyo alilihitaji.

Hata hivyo Nana alikiri kuwa gauni hilo linafanana na michoro ya ALmee. Lakini kufanana huko kumetokana na maelekezo yake aliyoyatoa hapo awali. Aidha ALmee walijibu wakisema mchoro wao ndio ulifanikisha gauni kukamilika hivyo walikuwa na haki ya ubunifu katika vazi hilo.

Mabishano hayo yamezua mijadala katika mitandao ya kijamii wengi wakiwaunga mkono Nana na Abbas Woman wakisema mteja ndiye mmiliki wa wazo. Huku baadhi wakiitetea kampuni ya ALmee kuwa wana haki katika ubunifu wa muundo katika gauni hilo.

Kwa upande wa Mohammed Abbas Ossu hakushiriki katika mabishano hayo yanayoendelea mtandaoni na badala yake alishare video namna alivyoanza kutengeneza gauni hilo. Huku akieleza changamoto alizokumbana nazo ikiwemo kupaka rangi misalaba pamoja na kuweka taa katika vazi hilo.

Gauni hilo la cathedral lililovutia zaidi katika tuzo za AMVCA 2026 limebaki njia panda hadi sasa hakuna taarufa rasmi kuwa mmiliki halali ni ALmee au Mohammed Abbas Ossu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *