
Dar es Salaam. Utata umeibuka kati ya wakazi wa Mbagala Rangitatu walioathiriwa na bomoabomoa kupisha ujenzi wa stendi mpya ya daladala na mabasi ya Kusini dhidi ya Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, huku kila upande ukidai kumiliki eneo hilo.
Mgogoro huo unahusu viwanja namba 13 na 15, ambavyo vimekuwa chanzo cha mgogoro tangu kuanza kwa operesheni ya ubomoaji iliyofanywa Mei 3, 2026 na kampuni ya udalali ya Yono, iliyopewa kazi hiyo na Manispaa ya Temeke.
Katika operesheni hiyo, zaidi ya nyumba 20 pamoja na fremu za biashara zilibomolewa katika eneo lililopo karibu na stendi ya sasa ya Mbagala Rangitatu.
Wananchi walioathirika wamedai wanamiliki eneo hilo kihalali tangu mwaka 1980. Baadhi yao wamesema wana leseni za makazi zinazodumu hadi mwaka 2029 na wameshangazwa na hatua ya ubomoaji iliyofanywa bila kushirikishwa.
Halmashauri nayo imedai viwanja hivyo vilipimwa awali kwa matumizi ya viwanda chini ya Manispaa ya Temeke, hivyo ni mali ya halmashauri hiyo, huku wananchi waliokuwa wakiishi hapo wakitajwa kuwa wavamizi.
Akizungumza na Mwananchi baada ya kutembelea eneo hilo wiki hii, kiongozi wa waathirika hao, Riziki Robert, amesema wao si wavamizi bali ni wakazi halali wenye leseni za makazi zinazotambuliwa na mamlaka husika.
“Kama halmashauri inasema sisi ni wavamizi, kwa nini walikuwa wakitupatia leseni za makazi na kupokea malipo yetu, na baadhi ya leseni hizo bado hazijaisha muda wake?” amehoji.
Amesema hawapingi maendeleo, lakini kama halmashauri ilihitaji eneo hilo kwa ajili ya mradi huo, ilipaswa kufanya mazungumzo na wananchi ili kupata mwafaka, ikiwamo suala la fidia.
“Kwa kuwa tumedharauliwa, tunajiandaa kufungua kesi ya madai kutokana na vitendo hivi vya uvunjifu wa sheria. Maandalizi kupitia kwa wakili wetu tayari yameshakamilika,” amesema.
Akielezea historia ya eneo hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Jomaary Satura, amesema viwanja namba 13 na 15 vilipimwa awali kwa matumizi ya viwanda, lakini upimaji huo haukukamilika kwa taratibu zote za kisheria za umilikishaji.
Kwa mujibu wa Satura, hali hiyo ilisababisha maeneo hayo kuvamiwa na wananchi.
Amesema mwaka 2023 halmashauri ilifanya upimaji upya kuthibitisha mipaka na kuhalalisha umiliki wa eneo hilo. Katika hatua hiyo, kiwanja namba 15 kilithibitishwa kisheria na kupatiwa hati miliki kwa jina la Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.
Kiwanja namba 13, amesema, kilibainika kuwa na changamoto ya kuwepo kwa hati mbili za umiliki (P17786 na P17787) zilizotolewa kwa watu wasiokuwa halali ndani ya sehemu ya eneo hilo, huku sehemu iliyobaki ikiendelea kumilikiwa bila utaratibu rasmi.
Satura amesema changamoto hiyo imekuwa ikikwamisha mchakato wa umilikishaji halali wa kiwanja namba 13.
Kuhusu matumizi ya eneo hilo, amesema kwa muda mrefu wananchi waliokuwa wakiishi hapo walikuwa wakilitumia kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi bila kibali cha Serikali.
Matumizi hayo yalijumuisha nyumba za kudumu 57, vibanda vya biashara, maegesho pamoja na fremu za maduka.
“Wananchi hao hawakulipa kodi ya pango wala tozo rasmi za Serikali, hali iliyosababisha upotevu wa mapato kwa halmashauri na kuchelewesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo,” amesema Satura.
Amesema hatua mbalimbali za kisheria na kiutawala zilichukuliwa kurejesha umiliki wa eneo hilo. Januari 22, 2025, halmashauri ilitoa notisi ya kuwaondoa wananchi hao ifikapo Februari 29, 2025, kabla ya kukumbushia tena agizo hilo Februari 27, 2025.
Baadaye, Machi 6, 2025, anasema wananchi hao waliomba kuongezewa muda wa kuondoka, na halmashauri ikaidhinisha ombi hilo kwa kutoa nyongeza ya miezi miwili.
Satura amesema baada ya muda huo kuisha, halmashauri ilitekeleza operesheni ya kuwaondoa waliokuwa wakiishi eneo hilo Mei 3, 2026, kwa kuzingatia taratibu za kisheria na kiutawala, kwa lengo la kurejesha eneo katika umiliki wa Serikali na kuruhusu matumizi yaliyopangwa.
Mmoja wa waathirika hao, Ibrahim, akizungumza na Mwananchi amesema ubomoaji huo umemrudisha nyuma kiuchumi baada ya kupoteza nyumba ya familia, fremu 10 za biashara pamoja na banda la kuoneshea mpira.
“Sasa tunaishi maisha ya kutangatanga. Kutoka kumiliki nyumba hadi kuwa kama watu wasio na makazi. Walikuja kubomoa bila hata kutupa muda wa kuondoa mali zetu,” amesema.
Ibrahim amesema ameishi eneo hilo tangu mwaka 1980. Awali, maeneo hayo yalitolewa kama mashamba ya kulima kabla ya wananchi kuanza kujenga nyumba na kuishi hapo bila matatizo.
Amesema kuanzia mwaka juzi, manispaa ilianza kuonesha nia ya kulitwaa eneo hilo kwa ajili ya shughuli za maendeleo ikidai kuwa ni eneo la wazi, madai ambayo wananchi waliyapinga.
Mkazi mwingine, Gabriel Shayo, amesema ubomoaji huo umewaacha katika mazingira magumu baada ya kupoteza makazi na vitega uchumi vyao bila maandalizi.
“Hili ni eneo letu la kihistoria. Baba zetu waliishi hapa na sisi tumekulia hapa. Inashangaza kuona halmashauri inakuja kubomoa nyumba na fremu bila taarifa ya kutosha,” amesema.
Kwa upande wake, mwanasheria wa waathirika hao, Mashiku Sabasaba, amesema hatua iliyochukuliwa na halmashauri haikufuata utaratibu wa kisheria.
“Tutafungua kesi mahakamani kudai haki za wateja wetu. Tunaamini mahakama ndiyo chombo cha kutoa haki, na tayari tupo katika hatua za mwisho za maandalizi hayo,” amesema.