Kibaha. Siku nane baada ya kutokea kwa vurugu katika eneo la Lupaso lililopo Vikawe, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, mapya yameibuka ikidaiwa kwamba wakazi wamekamatwa na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi bila kueleza wanawapeleka wapi.
Kamatakamata hiyo imetokea saa 8 usiku wa kuamkia leo Mei 14, 2026 katika eneo hilo lililotawaliwa na vurugu Mei 6, 2026 na kusababisha vifo vya watu wanne kufuatia mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kati ya wakazi wa eneo hilo na familia ya Juma Ngololo inayodai kumiliki eneo hilo.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Vikawe, Shaban Ally Shaban ameliambia Mwananchi kwamba watu 13 wamekamatwa katika kamatakamata hiyo.
“Walikuja polisi usiku na kuanza kukamata watu, wamewachukua 13 wakawafungia kwenye chumba, baada ya muda wakawaachia 10 na kuondoka na watatu ambao hatuelewi ni kwa sababu gani na wamewapeleka wapi,” amesema mwenyekiti huyo wa mtaa.
Mwananchi limemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase kutaka kufahamu chanzo cha kamatakamata hiyo, walipo waliokamatwa na hatima yao.
Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Kamanda huyo alipopigiwa simu yake ilikatwa, alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu na ilishindikana kuonana naye ofisini kwake.
Akifafanua zaidi kuhusu kamatakamata hiyo, mwenyekiti huyo wa serikali ya mtaa amesema baada ya vurugu za Mei 6, 2026katika eneo hilo, walipeana jukumu la ulinzi.
“Wakazi wa eneo hili tulikubaliana wawe wanalinda kwa zamu, hivyo kulikuwa na watu pale wakilinda, ndipo polisi wakaja usiku saa 8 na kuanza kukamata watu.
“Hawakutueleza sababu ya kamatakamata hiyo, waliwakamata 13 na kuwafungia kwenye chumba hadi muda ya saa 10 alfajiri walipowafungulia na kuondoka na watatu ambao hatuelewi wamewapeleka wapi,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Amesema uongozi wa mtaa unafikiria kwenda makao makuu ya polisi Pwani ili kufahamu kama waliokamatwa wako huko au la.
Vurugu za Vikawe zilizotokea alfajiri ya Mei 6, 2026 kufuatia mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kati ya wakazi wa eneo hilo na familia ya Ngololo inayodaiwa kuwa mmiliki halali wa maeneo hayo.
Mapigano hayo yaliwahusisha wananchi na watu waliotajwa kuwa mabaunsa waliodaiwa kupelekwa na Ngololo ili kubomoa nyumba zilizojengwa eneo hilo, hali iliyosababisha vifo vya watu wanne, majeruhi na uharibifu wa mali.
Mei 12, 2026, maofisa kutoka halmashauri walikwenda kufanya tathimini ya uharibifu katika eneo hilo na kuondoka huku wananchi walioathirika wakisema bado hawajui hatima yao.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John (Niki wa Pili) aliiambia Mwananchi kwamba Serikali ya Wilaya ilijaribu kusuluhisha mgogoro wa ardhi uliokuwepo baada ya kutokea uvamizi ambapo wenye maeneo 121 waliridhia wavamizi wawalipe, isipokuwa familia ya Ngololo.
Alisema kabla ya vurugu hizo kulikuwa na mchakato wa maridhiano kati ya wananchi waliokuwa wamejenga eneo hilo (wavamizi) na baadhi ya wamiliki halali, ambapo walikubaliana waliuziwa maeneo hayo kwa utapeli na kuwa tayari kuyalipia upya kwa gharama ya Sh3,000 hadi Sh3,500 kwa kila mita ya mraba.
“Familia ya Ngololo haikukubaliana na maridhiano hayo na badala yake ilitaka suala hilo liamuliwe mahakamani, hivyo mgogoro wa ardhi uliopo eneo hilo utamalizwa na Mahakama, kuhusu vurugu zilizotokea tayari mtuhumiwa amekamatwa kwa uchunguzi zaidi,” alisema.
Baadhi ya wakazi wa eneo la Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani wakiwa wanaangalia mali zao zilizoharibiwa baada ya kuibuka vurugu kati yao na watu waliotajwa ni mabaunsa, vurugu hizo zilizotokana na mgogoro wa ardhi zimesababisha vifo vitatu, majeruhi 15 na uharibifu wa mali, Picha na Imani Makongoro
Familia 10 zilizopoteza makazi katika vurugu hizo na kupata hifadhi kwenye mapagale huku zikisaidiwa chakula kupitia michango ya wadau mbalimbali iliyokusanywa na uongozi wa Serikali ya Mtaa na majeruhi ambao walipelekwa Hospitali ya Mkoa Tumbi wakiendelea na matibabu.