Unguja. Wenyeviti wa Mikoa 11 wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar wameunga mkono maazimio ya kamati kuu ya chama hicho juu ya taarifa ya Tume ya Jaji Chande ya kuchunguza matukio ya vurugu  ya Oktoba 29, 2025.

Tume hiyo ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya kutokea kwa vurugu kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akitoa taarifa hiyo leo Mei 14, 2026, Mwenyekiti wa Mkoa wa Mjini, Haji Dude Haji kwa niaba ya wenyeviti wa mikoa 11 kichama ya Zanzibar, amesema wametoa kauli hiyo kwa umoja wao.

Wenyeviti hao ni pamoja na Haji Dude Haji, Raisa Abdallah Mussa, Rashid Khalid Salim, Juma Khamis Alli, Yussuf Salum Khamis, Moh’d Abdalla Bakar, Issa Idrissa Mwinyi, Silima Juma Abdalla, Mcha Rajab Haji, Vuai Abdul Qadir na Abdillahi Jihad Hassan.

Dude amesema, wameunga mkono na kuipongeza Kamati ya chama hicho kuikataa Tume hiyo na kutokubali taarifa yake kwani imeundwa kwa ajili ya kuwalinda wauaji badala ya kuwawajibisha.

Mwenyekiti wa chama cha Act wazalendo Mkoa wa Mjini, Haji Dude Haji.

“Tunaunga mkono wito wa kamati kuu ya chama kuchukuliwa hatua za dharura ikiwemo kuitishwa kwa uchunguzi huru wa kimataifa kuchunguza mauaji ya Oktoba 2025, kuachiwa kwa watu waliofunguliwa kesi ikiwemo Tundu Lissu na kuwajibisha wizara, vitengo na ofisi zilizochangia kutokea mauaji,” amesema.

Vile vile, Wenyeviti hao wameunga mkono azimio la kamati Kuu la kuhitaji kuanza kwa mchakato wa katiba mpya, mageuzi ya Jeshi la Polisi na kufutwa kwa sheria kandamizi kama vile   ya uchunguzi,  ya vyama siasa na sheria 40 kandamizi zilizotajwa kwenye ripoti ya Tume ya Jaji Nyalali.

Mbali na hilo, wenyeviti hao wametoa rai kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuiweka hadharani ripoti yote ya Jaji Chande kwani akifanya hivyo itasaidia wananchi kuelewa kwa kina mbinu za kiuchunguzi za tume na matokeo ya uchunguzi huo.

“Ingawa tume ya Jaji ni ya Rais kama ambavyo Rais Samia alivyosema lakini suala ambalo ilipewa ilichunguze ni zito lenye masilahi mapana ya Taifa. Watanzania wana haki ya kujua ambacho Tume ya Jaji Chande imekiwasilisha,” amesema Dude kwa niaba ya wenzake.

Hata hivyo, Wenyevito hao wametuma salamu za mshikamano za kumpa moyo Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba kwa kuwa sehemu ya viongozi wastaafu waliosimamia ukweli kwenye ripoti ya Jaji Chande.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *