Shinyanga. Zaidi ya miaka 10 tangu kuanza kwa ujenzi wa Soko la Ndala kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), wananchi wa kata hiyo wameibuka na kilio kipya wakiiomba Serikali kulinusuru soko hilo ambalo sasa limeanza kuharibika na kugeuka makazi ya popo kutokana na kutotumika kwa muda mrefu.
Wakazi wa Kata ya Ndala wanasema wamechoshwa na ahadi za muda mrefu kuhusu kukamilishwa kwa soko hilo huku wakilazimika kusafiri umbali mrefu kwenda kupata huduma katika masoko ya Nguzonane na Kambarage.
Wakizungumza na Mwananchi leo Mei 14, 2026, wananchi hao wamesema kuchelewa kukamilika kwa soko hilo si tu kunawaathiri kiuchumi, bali pia kunachangia kudorora kwa shughuli za biashara katika eneo hilo.
Mkazi wa Ndala, Holo Alani, amesema viongozi mbalimbali wamekuwa wakifika mara kwa mara na kuahidi kukamilisha mradi huo bila kuona utekelezaji wake.
“Tumekuwa tukisikia ahadi kila wakati lakini hakuna kinachoendelea. Sasa hivi soko limeanza kuharibika, na vibanda vichache tu ndivyo vinatumika. Kwa kweli hali hii inatuumiza sana,” amesema Holo.
Kwa upande wake,Janeth Pastory, mkazi wa Mtaa wa Mlepa, amesema wananchi wamekuwa wakifuatilia suala hilo kwa viongozi wao lakini bado hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa.
“Kila tukifuatilia tunaambiwa utekelezaji utaanza, lakini miaka inaenda hakuna kinachofanyika. Tumekata tamaa kwa sababu tulitegemea soko hili litatusaidia kupata huduma karibu na kuongeza biashara,” amesema.
Kaimu Mkuu wa Division ya viwanda, biashara na uwekezaji Manispaa ya Shinyanga Shamimu Shaban akifafanua jambo.
Wananchi hao wamesema kukamilika kwa soko hilo kutasaidia kukuza biashara ndogondogo, kuongeza kipato cha wananchi na kuchochea uchumi wa eneo hilo.
Akizungumza hivi karibuni katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga, Diwani wa Kata ya Ndala, Zamda Shaban, amesema licha ya soko hilo kutengewa bajeti tangu mwaka 2023, utekelezaji wake bado haujaanza.
Amesema hali ya miundombinu ya soko hilo inaendelea kuwa mbaya na kwamba kuna hatari ya baadhi ya maeneo kushindwa kutumika ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.
“Tunaiomba Serikali kutoa fedha zilizotengwa, kiasi cha Sh20 milioni, ili kuanza maboresho ya haraka na kulinusuru soko hili kabla halijaharibika zaidi,” amesema Zamda.
Diwani wa Kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga Zamda Shaban akizungumzia changamoto ya soko la Ndala.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Manispaa ya Shinyanga, Shamimu Shaban, amesema halmashauri inaendelea na jitihada za kuboresha miundombinu ya masoko pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Naye Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Salum Kitumbo, amesema halmashauri ina mpango wa muda mrefu wa kuboresha masoko yote katika manispaa hiyo ili kuyawezesha kufanya kazi katika mazingira bora na kusaidia kukuza uchumi wa wananchi.
Amesema maboresho hayo yanakusudia kuongeza mazingira rafiki kwa wafanyabiashara pamoja na kuimarisha huduma kwa wananchi wanaotegemea masoko hayo katika shughuli zao za kila siku.