
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika Mkutano wa Pili wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa BRICS kwamba: Ubadilishanaji wa teknolojia na rasilimali watu unapaswa kufanywa bila vikwazo miongoni mwa wanachama wa BRICS.
Sayyid Abbas Araqchi amesema katika Mkutano wa Pili wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa BRICS kuhusu mada ya “Kuunda Jukwaa la Ustahimilivu, Ubunifu na Ushirikiano Uendelevu” huko New Delhi, mji mkuu wa India kwamba: Ubunifu katika BRICS haupaswi kuishia kwenye maabara, lakini pia unapaswa kufanyika katika uundaji wa sera. “Lazima tuunde jukwaa ambamo ubadilishanaji wa teknolojia, maarifa na rasilimali watu miongoni mwa nchi wanachama unaweza kufanywa bila vikwazo”, amesema Araqchi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa: “Ulimwengu wa leo unakabiliwa na mishtuko mtawalia katika nyanja za uchumi, mazingira na usalama. Mifumo ya sasa imekuwa dhaifu sana dhidi ya mishtuko hiyo. Vita ni mojawapo ya mishtuko hiyo. Vita vikali vya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, Lebanon, Gaza na maeneo mengine ya dunia vimesababisha uharibifu usioweza kurekebishwa kwa miundombinu ya kibiolojia.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza: “Kwa hivyo, njia yetu uendelevu inapaswa kujikita katika kuimarisha ustahimilivu wa kitaifa na kikanda. Nchi wanachama wa BRICS lazima zilinde minyororo yao ya usambazaji, ziwe na mifumo ya aina mbalimbali ya fedha na kujenga miundo imara ya ulinzi wa kiuchumi dhidi ya mashinikizo ya upande mmoja ili iweze kusasishwa wakati wa migogoro, badala ya kuchakaa.”
Sayyid Abbas Araqchi amesema: “Ushirikiano ndio njia pekee ya uokovu katika zama ambapo sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na kutenga wengine zinaongezeka. Hatufuatilii ushirikiano wa muda; badala yake, tunataka ushirikiano wa kimuundo. Lazima tuondoke katika ushirikiano wa jadi na kuelekea kwenye ushirikiano wa kimkakati; ambapo uwezo wa kila nchi unakamilisha mahitaji ya nchi nyingine.”