Kufichuliwa kwa safari ya Netanyahu huko UAE wakati wa vita vya kichokozi vya Marekani na utawala haramu wa Israel dhidi ya Iran kumewafanya watawala wa UAE wawakasirikie sana wenzao wa utawala wa Kizayuni.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel imetangaza katika siku za hivi karibuni kuwa Benjamin Netanyahu alifanya safari ya siri huko Imarati wakati wa vita na Iran na kukaribishwa kwa shangwe na Rais Mohammed bin Zayed wa nchi hiyo. Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE imesema kwamba madai kuwa Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel aliitembelea nchi hiyo wakati wa vita na Iran “hayana msingi kabisa” na kuyakanusha vikali.
Saa chache baada ya ukanushaji huo, Zev Agmon, mkuu wa zamani wa ofisi ya Benjamin Netanyahu, ambaye alijiuzulu hivi karibuni na ambaye aliambatana naye wakati wa safari yake nchini UAE, alipinga maelezo ya serikali ya Abu Dhabi na kuandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: “Kama mtu ambaye alifuatana na Waziri Mkuu katika safari hii ya kihistoria ambayo imebakia siri sana hadi sasa, ninaweza kusema kwamba Waziri Mkuu alikaribishwa kama mfalme mjini Abu Dhabi.” Wakati huo huo, idhaa ya Israel ya “i24” iliripoti kwamba baada ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuthibitisha safari ya Benjamin Netanyahu huko Abu Dhabi mwezi Machi, UAE ilituma ujumbe wenye maneno makali wa kupinga hatua hiyo ya Israel.
Nukta nyingine ni kwamba Seyyed Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, akithibitisha ziara ya Netanyahu nchini Imarati, amesema, “Netanyahu sasa amefichua hadharani yale ambayo vyombo vya usalama vya Iran viliyawasilisha kwa uongozi wetu muda mrefu uliopita.”
Kwa hivyo, swali ni je, kwa nini UAE imekuwa na wasiwasi kuhusu kufichuliwa kwa ziara ya Netanyahu huko Abu Dhabi? Ni nini athari zake kwa UAE?
Sababu ya kwanza na muhimu zaidi ni kwamba ingawa UAE ina tamaa na matarajio makubwa kuhusiana na nafasi yake ya kikanda, pia inafahamu vizuri udhaifu wake katika uwanja huo.

UAE inajua kwamba kushirikiana waziwazi na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kunaweza kuifanya nchi hiyo kulengwa kihalali na vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo kuhatarishwa usalama wake dhaifu na unaolegalega. Kanali ya 12 ya Israel imeripoti kuwa UAE kujaribu kufunika safari ya Netanyahu nchini humo kumechochewa na hofu, kwa sababu Abu Dhabi inahofia kuonekana kama mshiriki wa mhimili unaoipinga Iran. Abu Dhabi ina wasiwasi kuwa inaweza kuwa shabaha ya moja kwa moja ya mashambulizi ya Iran kutokana na uhusiano wake na Israel.
Jambo jingine muhimu ni kwamba, kinyume na ushirikiano wa wazi wa Imarati na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nchi nyingine za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi hazijakuwa tayari kushirikiana hadharani na utawala wa Kizayuni au kuchukua hatua kali dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kuhusiana na hili, Bloomberg imeripoti kwamba “UAE ilijaribu kuzishawishi Saudi Arabia, Qatar na majirani wengine wa Ghuba ya Uajemi zishirikiane zaidi katika kukabiliana na mashambulizi ya Iran, lakini jitihada hizi zilikabiliwa na upinzani.” Kwa hivyo, hatua ya Wazayuni ya kufichua ushirikiano wa UAE na utawala huu wakati wa vita dhidi ya Iran inaweza kuiweka Imarati hatarini katika eneo.
Kwa kuzingatia mvutano wa hivi karibuni kati ya UAE na Saudi Arabia, kufichuliwa ushirikiano na Israel dhidi ya Iran kunaweza kuzileta pamoja Iran na Saudi Arabia katika kukabiliana na UAE, jambo ambalo ni tishio kubwa kwa nchi hiyo.
Jambo jengine muhimu ni kwamba, Imarati inafahamu vizuri kwamba, kuimarisha uhusiano na utawala wa Kizayuni ni jambo lisilokubaliwa na wengi katika ulimwengu wa Kiislamu, kwa sababu hivi sasa utawala huo wa Kizayuni unachukiwa zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu kuliko wakati mwingine wowote. Sababu ya chuki hiyo ni jinai ambazo utawala wa Kizayuni umezifanya dhidi ya nchi za Kiislamu katika miaka ya hivi karibuni. Imarati ina wasi wasi kwamba matokeo ya kufichuliwa safari ya Netanyahu huko Abu Dhabi wakati wa vita na Iran yataeneza chuki hii ya Israel hadi Imarati, suala ambalo watawala wa serikali ya Abu Dhabi wanalichukulia kuwa linakinzana na siasa zao za nje na mtazamo wao wa kiusalama kwa ujumla.
