Serengeti Boys yafuzu Kombe la Dunia kibabeSerengeti Boys yafuzu Kombe la Dunia kibabe

Ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Angola leo Jumapili, Mei 17, 2026 huko Morocco, umeihakikishia timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kufuzu Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo mwaka huu.

Ushindi huo katika mechi hiyo iliyochezwa katika Uwanja namba 3 wa Kituo cha Kimataifa cha Soka kwa Vijana Wadogo cha Mfalme Mohammed VI, Rabat Morocco, umeifanya Serengeti Boys kujihakikishia uongozi wa kundi C la AFCON na kutinga robo fainali.

Baadhi ya wachezaji wa kikosi cha Serengeti Boys wakishangilia baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Angola katika mashindano ya AFCON kwa vijana chini ya miaka 17.

Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, timu nane zinazoingia hatua ya robo fainali, zinakata moja kwa moja tiketi ya kuliwakilisha bara la Afrika katika Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo, zikiungana na nyingine mbili ambazo zimeishia hatua ya makundi huku zikiwa na matokeo bora katika nafasi ya tatu.

Katika mchezo wa leo, mabao ya Serengeti Boys yamewekwa kimiani na Razaki Mbegelendi, Hasan Kizinga na Sadam Hamis.

Mbegelendi amefunga bao la kwanza kwa shuti hafifu la mguu wa kulia ndani ya eneo la hatari la Angola akimalizia pasi ya Luqman Mbalasalu katika dakika ya 27 na dakika ya 52, makosa ya beki wa Angola kushindwa kutuliza pasi ya kipa wake, yameipa faida Serengeti Boys ambayo ilinasa mpira huo kupitia Sadam Hamis aliyempasia Kizinga ambaye ameukwamisha wavuni.

Baadhi ya wachezaji wa kikosi cha Serengeti Boys wakishangilia baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Angola katika mashindano ya AFCON kwa vijana chini ya miaka 17.

Bao la tatu ambalo limeihakikishia Serengeti Boys kufuzu Kombe la Dunia, lilifungwa na Sadam Hamis kwa mkwaju wa faulo uliozama moja kwa moja wavuni baada ya Angola kufanya faulo nje kidogo ya eneo lao la hatari.

Serengeti Boys inakuwa timu ya kwanza ya kiume ya taifa ya Tanzania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia baada ya kujaribu bila mafanikio kufuzu katika fainali za 2017, 2019 na mwaka jana.

Baadhi ya wachezaji wa kikosi cha Serengeti Boys wakishangilia baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Angola katika mashindano ya AFCON kwa vijana chini ya miaka 17.

Pia hii ni mara ya kwanza kwa Serengeti Boys kukusanya idadi kubwa ya pointi katika Fainali za AFCON U17 ikivunja rekodi ya kizazi cha mwaka 17 kilichokusanya pointi nne.

Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika Qatar kuanzia Novemba 19 hadi Desemba 13 mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *