Arusha. Wanahisa wa Benki ya CRDB wameeleza matumaini yao ya kuona Mkurugenzi Mtendaji, Dk Abdulmajid Nsekela akiendelea kuongoza hata baada ya ukomo wa kawaida wa miaka 10 ya uongozi.
Kauli hiyo inatokana na kile wanachoamini, bado ana nguvu, maono, uzoefu na uwezo mkubwa wa kuendelea kuipeleka benki hiyo katika hatua nyingine ya mafanikio makubwa zaidi.
Wanahisa hao wanaeleza sababu kubwa inayowafanya kuwa na imani kubwa na uongozi wa Dk Nsekela ni kiwango kikubwa cha thamani ambacho wamekipata kupitia uwekezaji ndani ya benki hiyo katika kipindi chake cha uongozi.
Wakati Dk Nsekela anachukua uongozi wa CRDB mwaka 2018, thamani ya hisa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ilikuwa wastani wa Sh95 kwa hisa, lakini kufikia Aprili 2026, thamani hiyo ilikuwa imefikia wastani wa Sh3,000 kwa hisa, hatua ambayo imeongeza imani kubwa ya wanahisa.
Kwa upande wa gawio, mwaka 2018 wanahisa walilipwa Sh5 kwa hisa, lakini kutokana na matokeo makubwa ya kihistoria yaliyopatikana mwaka jana, wanahisa walipitisha gawio la Sh90 kwa kila hisa, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 1,000.
Benki hiyo pia imeendelea kuwa miongoni mwa kampuni zenye thamani kubwa zaidi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ikiwa na thamani ya Dola 2.8 bilioni za Marekani, jambo ambalo limeendelea kuongeza imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya Tanzania.
Wanahisa wa Benki ya CRDB wakishangilia baada ya kupitishwa kwa gawio la kihistoria la Sh90 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 38 kulinganisha na gawio la Sh65 kwa hisa lililotolewa mwaka 2024.
Akizungumza kwenye mkutano mkuu uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Arusha, Godfrey Mosha mmoja ya wanahisa waanzilishi wa CRDB tangu mwaka 1996, amesema tangu awe mwanahisa hajawahi kushuhudia ukuaji mkubwa wa thamani ya wanahisa na biashara ya benki hiyo kama ambavyo imetokea katika kipindi cha uongozi wa Dk Nsekela.
“Hakika tumeshuhudia ukuaji wa ajabu na wakihistoria katika sekta ya fedha nchini,” amesema.
“Licha ya faida ya benki yetu kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 1000 tangu Dk Nsekela alipochukua hatamu ya uongozi, jumla ya mali za CRDB zimefikia Sh23.9 trilioni mwaka 2026 kutoka takribani Sh7.6 trilioni mwaka 2018. Amana za wateja zimeongezeka kutoka Sh4.8 trilioni mwaka 2018 hadi kufikia Sh16.2 trilioni, mikopo ikikua kutoka Sh3.6 trilioni hadi Sh14.7 trilioni.
“Huu ni ukuaji wa ajabu hatupaswi kumuacha kijana huyu aondoke mapema wakati bado ana nguvu za kutupeleka mbali zaidi,” amesema Mosha.
Taarifa ya mwaka ya CRDB inaonesha ukuaji huu umeifanya benki hiyo kuendelea kuongoza soko la fedha nchini ikishika soko la benki kwa asilimia 28 ya Amana zote za wateja nchini, asilimia 27 ya mali zote za sekta ya benki, asilimia 29 ya mikopo iliyotolewa na taasisi za fedha pamoja na asilimia 30 ya faida baada ya kodi miongoni mwa zaidi ya benki 40 zilizopo nchini.
Kwa wanahisa wengi, takwimu hizi si tu alama ya mafanikio ya biashara, bali ni ushahidi wa uongozi wenye maono makubwa na uwezo wa kutekeleza mikakati kwa ufanisi.
Katika mkutano mkuu huo, sauti ya wanahisa ilikuwa moja; pongezi kwa matokeo yaliyopatikana na matumaini makubwa kuhusu mustakabali wa benki hiyo.
Wengi wao wameeleza kuwa, mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka minane iliyopita yanaonesha wazi namna ambavyo uongozi imara, wenye maono na uthubutu unavyoweza kubadilisha taasisi.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema, “katika ulimwengu wa fedha duniani kote, ofisa mtendaji mkuu kama hana matatizo na anafanya vizuri kwa viwango hivi vya Dk Nsekela, huwa hawambadilishi kirahisi kwa sababu ukimbadilisha hisa zinashuka, lakini pia utendaji wa taasisi unaweza kushuka kwa sababu imani ya wateja na wawekezaji ipo kwenye maono na uongozi imara.”
Wanahisa wengi wamekuwa wakitaja mkakati wa biashara wa “Evolve” kama moja ya hatua muhimu zaidi zilizobadilisha sura ya CRDB.
Kupitia mkakati huo wa miaka mitano (2023/27), benki hiyo imefanikiwa kuimarisha mifumo ya kidijitali, kuongeza ujumuishi wa kifedha, kupanua huduma zake nje ya mipaka ya Tanzania, kuboresha uzoefu wa wateja na kuongeza thamani kwa wanahisa kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa hapo awali.
Hivi sasa, zaidi ya asilimia 98 ya miamala yote ya benki hiyo inafanyika nje ya matawi, hatua inayoonesha mafanikio ya uwekezaji katika teknolojia.
Aidha, asilimia 50 ya akaunti mpya sasa zinafunguliwa kupitia majukwaa ya kidijitali huku asilimia 40 ya miamala yote ikifanyika nje ya muda rasmi wa kazi wa matawi.
Pia, CRDB imeendelea kupanua ushawishi wake nje ya Tanzania. Kupitia uwekezaji katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi pamoja na uwepo wake Dubai, benki hiyo imeendelea kuwa daraja muhimu la biashara linalounganisha Afrika Mashariki, Afrika ya Kati, Ghuba ya Uarabuni pamoja na masoko ya Asia.
Hatua hiyo imeongeza fursa kwa wafanyabiashara, wawekezaji na wajasiriamali wa Tanzania kupata masoko mapya ya kikanda na kimataifa.
Wanahaisa wa Benki ya CRDB wakishangilia baada ya kupitishwa kwa gawio la kihistoria la Sh90 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 38 kulinganisha na gawio la Sh65 kwa hisa lililotolewa mwaka 2024.
Katika umri wa miaka 54 pekee, wengi wanaamini kuwa Dk Nsekela bado ana nguvu, uzoefu, maono na uwezo wa kuendelea kuiongoza benki hiyo kuelekea hatua nyingine kubwa zaidi ya ukuaji.
“Tunaimba Serikali itusikilize sisi wanahisa wa CRDB, bado tuna imani na Dk Nsekela tunapoelekea kuanza na kutekeleza mkakati mpya wa biashara utakaoanza mwaka 2028/2032,” amesema Chedego moja ya wanahisa waanzilishi huku akisema kwa utendaji alioonesha Dk Nsekela ni ngumu kwa wanahisa kumuacha aondoke.
Hata hivyo, wanahisa hao wanaheshimu sheria zilizowekwa na Serikali pamoja na mamlaka za udhibitina kusema kuwa, maombi yao ni kwa masilahi mapana ya CRDB na mustakabali wa sekta ya fedha kwa jumla.
Maombi ya wanahisa yameungwa mkono pia na baadhi ya viongozi wastaafu wa sekta ya fedha na wanahisa wakubwa akiwamo Dk Charles Kimei pamoja na Dk Ally Laay, ambao wamekuwa wakieleza kuvutiwa na kasi ya ukuaji, uthabiti wa utendaji wa benki hiyo.
Katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, CRDB imeandika historia mpya kwa kuongoza katika viashiria vyote vikuu vya kiutendaji nchini.
Benki hiyo ilirekodi faida baada ya kodi ya Sh206 bilioni, kiwango kikubwa zaidi kuwahi kufikiwa na benki nchini ndani ya robo ya kwanza.
Katika mazingira hayo ya utendaji, wanahisa wameadhimia kuunda jopo la ushauri linaloongozwa na Christopher Gachuma ili kuwasilisha maoni yao kwa kufuata taratibu stahiki kwa Serikali kuhusu Dk Nsekela.
