Puma Energy Tanzania yaleta mfumo wa kutoa shukurani kwa wateja wakePuma Energy Tanzania yaleta mfumo wa kutoa shukurani kwa wateja wake

Dar es Salaam. Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania imezindua rasmi programu PRIS nchini Tanzania ambayo inalenga kuhamasisha matumizi ya njia za kidijitali katika kupata huduma.

Kupitia mfumo wa PRIS, wateja wataweza kujikusanyia pointi wanaponunua mafuta, vilainishi, pamoja na bidhaa zinazopatikana katika maduka ya Puma Energy Tanzania. Pointi hizo zinaweza kutumika kupata zawadi mbalimbali ikiwemo bidhaa za matumizi ya nyumbani, chakula pamoja na punguzo la mafuta kupitia mtandao mpana wa washirika wa Puma Energy.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba alisema uzinduzi wa PRIS ni hatua muhimu inayokwenda sambamba na mwelekeo wa taifa wa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma.

“Kwa mtazamo wa serikali, ubunifu kama huu wa PRIS unaongeza thamani kwa wananchi kwa kuwawezesha kunufaika moja kwa moja na kila manunuzi yao kupitia mfumo wa pointi na zawadi. Mfumo huu unaimarisha ujumuishi wa kidijitali na kuchochea ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kisasa.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania, Fatma Abdallah alieleza PRIS ni sehemu ya dhamira yetu ya kuwaweka wateja katikati ya kila tunachofanya.

Tunaendelea kuwekeza katika suluhisho zinazotoa thamani halisi kwa Watanzania. Mfumo huu unabadilisha matumizi ya kila siku kuwa zawadi zenye manufaa, huku tukiunga mkono safari kubwa ya Taifa, ya kuelekea maendeleo ya kidijitali na ukuaji wa uchumi.”

Programu hiyo imetengenezwa kwa kuzingatia urahisi na upatikanaji kwa kila mtumiaji. Wateja wanaweza kupakua app hiyo, kujisajili kwa kutumia namba yao ya simu na kuanza kujikusanyia pointi mara moja kwa kuonyesha QR Code wakati wa kufanya malipo. Baada ya kufikisha kiwango kinachohitajika cha pointi, wanaweza kuzitumia kupata bidhaa mbalimbali madukani au punguzo kwenye ununuzi wa mafuta siku zijazo.

Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusu mfumo huo, Meneja Mauzo wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania, Sulpis Mmasi, alisema “Programu ya PRIS imetengenezwa kwa kutumika kirahisi, kufikika kwa kila mtu na ina manufaa kwa wateja. Wateja wanajikusanyia pointi kila wanapoweka mafuta, na kununua bidhaa zingine za Puma, ambapo pointi hizo unaweza kuzitumia katika manunuzi yajayo kupitia mtandao unaoendelea kukua wa washirika wetu.”

Aidha PRIS tayari imefanikiwa kutumika katika masoko mengine barani Afrika ambako Kampuni ya Nishati ya Puma inafanya shughuli zake, ikiwemo Zimbabwe, Malawi na Botswana na  imeonyesha kupokelewa vizuri na wateja pamoja na kuongeza ushiriki wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *