Dawasa mtaa kwa mtaa kupunguza upotevu wa majiDawasa mtaa kwa mtaa kupunguza upotevu wa maji

Dar es Salaam. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), imeanza kuziba mabomba, kukarabati na kubadilisha miundombinu chakavu ili kupunguza upotevu wa maji katika eneo inayotoa huduma.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa mkakati wake wa miaka mitano iliyouanzisha ili kushughulikia changamoto hiyo kubwa ya upotevu ambao kwa sasa maji yanapotea kwa asilimia karibu 35 nchini kote kiujumla.

Akizungumza leo Jumatatu, Mei 18, 2026 alipokuwa kituo cha Dawasa kilichopo Tegeta, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mkama Bwire amesema upotevu wa maji unatokana na shughuli mbalimbali kama upasukaji wa mabomba au maji kumwagika kutoka miundombinu ya Dawasa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mkama Bwire akiongoza timu ya watumishi wa mamlaka hiyo katika kuziba mabomba, kukarabati na kubadilisha miundombinu chakavu, ili kupunguza upotevu wa maji katika eneo inayotoa huduma. Picha na Sute Kamwelwe.

“Pia, kuna upotevu wa maji wa kibiashara unaotokana na watu kujiunganishia maji kinyume cha utaratibu na kutumia bila kuwa kwenye mfumo au kuchezea dira za mita,” amesema.

Kutokana na hali hiyo ndio maana Dawasa wameandaa mkakati huo wa miaka mitano kuanzia mwaka huu utakaohusisha ununuzi wa vifaa mbalimbali vya kisasa ikiwemo mita na mabomba.

“Mkakati huu umeainisha shughuli mbalimbali tutakazozifanya kwa miaka hii mitano lengo ikiwa ni kupunguza kiwango kinachokubalika ambacho ni asilimia 20 hadi 25.”

Bwire amesema mwaka huu wa kwanza watatumia Sh17 bilioni kupitia mapato ya ndani ya mamlaka kununua mabomba, mita na vifaa vya kisasa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mkama Bwire akiongoza timu ya watumishi wa mamlaka hiyo katika kuziba mabomba, kukarabati na kubadilisha miundombinu chakavu, ili kupunguza upotevu wa maji katika eneo inayotoa huduma. Picha na Sute Kamwelwe.

Wanaotumia maji kinyume kushughulikiwa

Katika utekelezaji wa mkakati huo wa miaka mitano, Bwire amesema watashughulika na wateja wasio waaminifu wanaotumia maji kinyume na taratibu.

“Kwa sasa tumeanza na upotevu wa maji wa mivujo tunaomba ushirikiano wa wananchi wapige simu watakapoona changamoto hiyo. Dawasa tumetoka ofisini kushughulikia changamoto hii.

Akizungumza hatua hiyo mwananchi wa Mbweni, Jamal Mustapha amesema itaimarisha huduma ya maji kwa kuwa upotevu si tu unaigharimu mamlaka bali hata wananchi wenyewe.

Naye, John Michael kutoka Tegeta amesema suala hilo la upotevu wa maji limekuwa likizungumziwa kwa muda mrefu hata katika ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na viongozi wengine mbalimbali.

“Kitendo cha kutoka kwenda kuziba mianya ya maji kumwagika liwe endelevu kama ilivyo kusudio kuhakikisha maji hayapotei,” amesisitiza alipokuwa akizungumza na Mwananchi Digital.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *