Wawakilishi waikalia kooni Wizara ya Kilimo, wakiitaka kutumia teknolojiaWawakilishi waikalia kooni Wizara ya Kilimo, wakiitaka kutumia teknolojia

Unguja. Wakati Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo ikiomba kuidhinishiwa Sh181.8 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27 kutekeleza miradi 10 ya maendeleo, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesema mipango ya kilimo inaonekana kwa nadharia lakini haipo kivitendo.

Kutokana na hilo, wameitaka Serikali kutumia teknolojia na kujifunza ujuzi katika mataifa yaliyofanikiwa ili Zanzibar iachane na utegemezi wa chakula kutoka nje.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo katika mkutano wa bajeti wa Baraza la Wawakilishi leo Mei 18, 2026, Waziri mwenye dhamana, Suleiman Masoud Makame, amesema kiwango hicho cha fedha kinajumuisha ruzuku ya Sh12.4 bilioni kwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo na Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo.

Waziri Masoud amesema katika utekelezaji wa miradi hiyo ameomba Sh145 bilioni kati ya fedha hizo Sh86.5 bilioni kutoka Serikali ya Mapinduzi (SMZ) na Sh58.4 bilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Michango ya wawakilishi

Wakichangia hotuba hiyo baadhi ya wawakilishi wamesema bado mipango ya kilimo Zanzibar ipo midomoni lakini haijaakisi hali halisi, hivyo inatakiwa kubadilisha kilimo cha mazoea na kuwa na cha kisayansi.

Mwakilishi wa Mtambile, Alley Masoud Alley amesema wizara inaeleza kuhusu kilimo cha umwagiliaji lakini inategemea maji ya visima jambo ambalo haliwezi kuwezesha kilimo hicho.

“Kwa sasa kilimo kilichopo bado ni cha mazoea si kilimo cha kuwainua wakulima na kuongeza hifadhi ya chakula,” amesema.

Mwakilishi wa Magomeni (CCM), Mahfoudh Abdallah Mohamed ameitaka Serikali kuongeza jitihada katika teknolojia lakini ikiendelea kama ilivyo sasa hakutakuwa na mabadiliko yoyote kwenye sekta ya kilimo.

“Bila teknolojia hatutoboi, kama kweli tunataka kuondokana na utegemezi wa chakula, basi tuwekeze kwenye teknolojia lakini ikiwa tunakwenda kama ilivyo hivyo hatufiki, hatuna budi kujikita katika kilimo cha kisayansi,” amesema Mahfoudh.

Naye Mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad amesema Serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kilimo lakini matokeo yake hayaonekani badala yake yamebaki midomoni.

“Hakuna matokeo kwa wakulima, imeelezwa hapa taarifa ya bajeti kwamba asilimia 50 ya kaya Zanzibar hazina uhakika wa chakula lakini mnataka tupitishe bajeti ya Sh75 bilioni kufanya ukarabati wa maghala,” amesema

Amesema Zanzibar ni rafiki ya nchi tatu za Thailand, India na Vietnam ambazo zimepiga hatua kubwa katika sekta ya kilimo lakini bado haijaona umuhimu wa kuwatumia katika teknolojia zinazotumika kwenye mataifa hayo.

Mwakilishi nafasi za wanawake, Aza January Joseph naye amesema licha ya maelezo ya wizara ya kuongeza chakula lakini upo kinadharia badala ya vitendo.

“Kilimo kiuhalisia hakionekani, ukienda sokoni huoni hayo mazao yanayolimwa Zanzibar lakini tumekuwa tukiimba hapa kila siku kuhusu kilimo,” amesema.

Akieleza miradi inayokwenda kutekelezwa na wizara hiyo, Waziri Makame amesema ni pamoja na mradi wa kuimarisha mifumo ya chakula kwa kuongeza tija na uzalishaji kupitia huduma za kisasa za kilimo katika umwagiliaji.

“Lengo hasa ni kuimarisha usalama wa chakula Zanzibar na kuongeza kipato cha wakulima wa mpunga kwa kuboresha uzalishaji. Kuboresha miundombinu ya kilimo barabara za mashambani, sehemu za kuingilia matrekta, visima, uzio salama, ngome za ulinzi, sakafu ya kukaushia, vivuli vya trekta, hifadhi na vyoo) katika skimu sita za umwagiliaji,” amesema.

Mradi mwingine ni kutoa mashine za kilimo na vifaa vya usimamizi wa maji kwa Jumuiya za Wakulima na Wakala wa Serikali (GATFMS).

Mradi mwingine ni wa ukarabati wa maghala kuhifadhia chakula unaolenga kuimarisha kiwango bora cha akiba ili kuondoa uhaba wa chakula nchini na kukabiliana na mahitaji ya dharura.

“Ukarabati wa maghala chakavu 10, ujenzi wa vihenge vyenye ujazo wa tani 80,000 Unguja na Pemba, ununuaji wa mpunga kwa uhifadhi wa chakula cha akiba na ujenzi wa kituo cha uhifadhi wa chakula na maabara kuu ya kilimo,” amesema.

Kuhusu mradi wa mabadiliko ya mfumo wa chakula kwa kukuza uchumi jumuishi, Makame amesema unalenga kubadili mifumo ya chakula ili kuchochea uchumi jumuishi, na kuongeza usalama wa chakula na lishe nchini na kuimarisha minyororo ya thamani ya mazao ya chakula (migomba na mihogo) na mwani kwa kutumia mbinu jumuishi na zinazokabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Miradi mingine ni ya kuimarisha miundombinu na uwezo wa utafiti wa kilimo maliasili na mifugo.

“Huu ni Mradi mpya ambao unatarajiwa kuanza utekelezaji mwaka huu wa fedha. Kuimarisha uwezo wa kufanya utafiti wa kilimo, maliasili na mifugo Zanzibar kupitia uanzishaji na uimarishaji wa maabara za utafiti, vituo vya utafiti na majaribio ya Wanyama,” amesema.

Ameitaja miradi mingine kuwa ni mradi wa kuendeleza mifumo ya chakula, matumizi na urejesheaji wa ardhi, mradi wa ulinzi wa misitu ya mwambao wa Zanzibar kwa manufaa mchanganyiko, mradi wa kuendeleza miundombinu ya mifugo na misitu.

Maoni ya kamati

Akisoma maoni ya kamati, Mwenyekiti wa Kamati ya Utalii, Biashara na Kilimo, Fatma Ramadhan Mohamed, licha ya kupongeza kuongeza fungu katika programu ya maendeleo ya kilimo kutoka Sh49.3 bilioni hadi kufikia Sh147.7 bilioni, lakini imeishauri Serikali programu hiyo ipatiwe fedha kama inavyoombwa.

“Kwani programu hii ina lengo la kuimarisha miundombinu bora ya umwagiliaji ambayo itapelekea kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula, kusimamia uzalishaji wa mbegu bora za nafaka, kudhibiti milipuko ya maradhi ya mimea pamoja kuimarisha hifadhi na upatikanaji wa chakula nchini,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *