Waziri: Marekani haiwezi kuizuia Afrika Kusini kushiriki kwenye kikao cha G20Waziri: Marekani haiwezi kuizuia Afrika Kusini kushiriki kwenye kikao cha G20

Waziri wa Afrika Kusini wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ronald Lamola, amesema Marekani haiwezi kuizuia nchi yake kushiriki kwenye Mkutano wa kilele wa nchi za G20 mwezi Desemba, akisisitiza kuwa nchi hiyo ni mwanachama mwanzilishi.

Lamola amezungumza na vyombo vya habari akiwa New Delhi, India, wakati wa mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa BRICS, uliofanyika mnamo Mei 14 na 15, 2026.

Alipoulizwa kuhusu uhusiano wa Afrika Kusini na Rais wa Marekani, Donald Trump, waziri huyo alikiri kuwa “mazingira yamekuwa yasiyotabirika.”

Kuhusu suala la mkutano wa G20 na kutokuwa na uhakika kuhusu kuhudhuria kwa Afrika Kusini, Lamola amesema si jukumu la Trump kuamuru kama Afrika Kusini inaweza au haiwezi kuhudhuria.

Ameongeza kuwa: “Hawezi kusema kwamba hatuwezi kuwa kwenye G20, kwa sababu sisi ni mwanachama mwanzilishi wa G20, na hakuna mwanachama mwingine wa G20 anayeweza kuamua kwamba nchi hii isihudhurie tena G20.”

Lamola pia amebainisha: “Sijui kama unaweza kuuita G20 ikiwa Afrika Kusini haipo.”

Waziri huyo alieleza kuwa hali hiyo si sawa na mwaka jana, kwa sababu mwaka jana Marekani iliombwa kuhudhuria lakini iliamua kutoshiriki kikao kilichofanyika Afrika Kusini. Rais Trump wa Marekani amekuwa na msuguano mkubwa na serikali ya Afrika Kusini ambapo ametoa madai yasiyo na msingi kuwa eti Wazungu Waafrikana wanakabiliwa na mauaji ya kimbari nchini humo. Serikali ya Afrika Kusini imekanusha madai hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *