Kawaida ajitwisha ulezi wa vijana wanufaika wa mkopo MtwaraKawaida ajitwisha ulezi wa vijana wanufaika wa mkopo Mtwara

Mwenyekiti wa UVCCM, Mohammed Ali Kawaida ameahidi kuendelea kuvisaidia vikundi vya vijana vinavyonufaika na mikopo ya halmashauri baada ya kuvutiwa na mafanikio ya kikundi cha Mshikamano kilichopo mkoani Mtwara.

Kawaida ambaye jana alianza ziara ya kikazi mkoani humo kwa lengo la kutembelea vikundi mbalimbali vya vijana na miradi ya maendeleo, amesema mafanikio ya kikundi hicho yanaonyesha namna mikopo ya asilimia nne ya halmashauri inavyoweza kuwa chachu ya ajira na maendeleo kwa vijana ikiwa itasimamiwa vizuri.

Kikundi cha Mshikamano kinachojishughulisha na ufyatuaji wa tofali kilinufaika na mkopo huo Desemba mwaka 2025, ambapo tangu kupokea fedha hizo kimefanikiwa kuongeza ajira kwa vijana, kurejesha kwa wakati Sh3.8 milioni pamoja na kununua mchanga wa kutosha kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao kwa muda mrefu.

Akizungumza na wanakikundi hao leo Mei 18, 2026, Kawaida amesema ameridhishwa na namna walivyotumia mkopo huo kuzalisha na kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.

New Content Item (4)

“Nimefurahishwa kuona vijana mmetumia vizuri fursa hii ya mkopo. Hii ndiyo picha halisi ambayo tunataka kuiona kwa vikundi vingine vya vijana nchini,” amesema.

Amesema ataendelea kuwa mlezi wa kikundi hicho huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vikundi vingine vitakavyoonyesha usimamizi mzuri wa mikopo na nidhamu ya urejeshaji.

Kawaida aliwasihi vijana hao kuendelea kurejesha mkopo wao wa Sh50 milioni kwa wakati ili kutoa nafasi kwa vikundi vingine vya vijana kunufaika na fedha hizo.

“Mkopo huu si kwa ajili ya kikundi kimoja pekee, mnaporejesha kwa wakati mnawasaidia vijana wengine pia kupata fursa ya kujikwamua kiuchumi,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na UVCCM, ziara hiyo inalenga kuimarisha mawasiliano kati ya viongozi na vijana pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo.

Wananchi na vijana wa Mkoa wa Mtwara wamehamasishwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mikutano na shughuli zitakazoandaliwa wakati wa ziara hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *