
Dar es Salaam. Jumanne, Mei 19, 2026, saa 5:00 asubuhi, Tanzania itapokea ugeni wa nyota wa zamani wa Manchester United na England, Rio Ferdinand ambaye anakuja kwa ziara ya siku nne itakayofikia tamati Mei 22, 2026.
Ferdinand anatua nchini kwa mwaliko wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda kama alivyothibitisha yeye mwenyewe kupitia video iliyosambaa katika mitandao tofauti ya kijamii.
“Ninatazamia kutembelea Tanzania wiki ijayo baada ya kuwa na mazungumzo mazuri na Waziri Paul Makonda pamoja na wengine kuhusu makubwa yaliyopo ndani ya nchi.
“Kwangu mimi, safari hii inahusu watu, utamaduni, soka na fursa. Tanzania ina shauku kubwa sana kwa michezo na ina kizazi cha vijana chenye hamasa kubwa, na ninatazamia kwa dhati kujifunza zaidi, kukutana na watu moja kwa moja na kutazama jinsi tunavyoweza kujenga fursa zenye maana pamoja katika siku zijazo.
“Ni heshima sana kupata fursa ya kukutana na Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wakati wa ziara yangu, na ninafurahia kupata uzoefu zaidi kuhusu nchi hii nzuri,” amesema Ferdinand kupitia video hiyo.
Kwa Tanzania ujio wa Ferdinand ni jambo lenye maana na umuhimu mkubwa kwa nchi na hilo linatokana na faida tatu ambazo zitapatikana kupitia ziara hiyo.
KUTANGAZA UTALII
Jina la Rio Ferdinand linajulikana karibia katika kila pembe ya dunia hasa na wapenzi wa soka ambao ni mchezo unaongoza kwa kupendwa na idadi kubwa ya watu ulimwenguni.
Pamoja na kwamba kwa sasa ameshastaafu soka, Rio Ferdinand ameendelea kuwa mtu anayefuatiliwa zaidi na mashabiki wa soka duniani kwa vile bado ameendelea kujihusisha na mchezo huo hasa kupitia uchambuzi wake wa Ligi Kuu ya England ambayo kwa mujibu wa ripoti ya Mtandao wa Win Sports, ligi hiyo inafuatiliwa na watu wanaokadiriwa kufikia bilioni 1.87 duniani na inaonyeshwa katika nchi 189.
Yeye mwenyewe binafsi ana wafuasi milioni 17.2 katika kurasa zake za mitandao ya Instagram na Twitter.
Hii ni fursa nzuri ya kuitangaza Tanzania hasa katika nyanja ya utalii kwani Ferdinand atatembelea vivutia baadhi vya utalii nchini kama hifadhi ya Serengeti.
FURSA MICHEZONI
Akiwa Tanzania, Rio Ferdinand pia atashiriki shughuli za kisoka kama mdahalo wa maendeleo ya michezo, kutembelea kituo cha soka Gymkhana na pia kutembelea Uwanja wa AFCON Arusha.
Hii itasaidia kuonyesha utayari wa nchi kuelekea tukio kubwa la AFCON 2027 na kuhamasisha muitikio wa Watanzania hasa mashabiki wa soka kuelekea tukio kubwa.
Kwa upande mwingine, kushiriki kwake katika program za vijana ni chachu ya kuhamasisha vijana wadogo kuwa na ndoto za kufika katika ngazi za juu kisoka.
KUITANGAZA TANZANIA
Ziara ya Rio Ferdinand ni chachu ya kutangaza hatua za kimaendeleo ambazo Tanzania kama nchi imezipiga katika nyanja tofauti.
Mfano wa maendeleo hayo ni katika sekta ya usafirishaji na uchukuzi ambapo mchezaji huyo atatumia usafiri wa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma siku ya Jumatano.
