TIRA: Elimu ya bima mashuleni ni msingi wa kukuza sekta ya bima nchiniTIRA: Elimu ya bima mashuleni ni msingi wa kukuza sekta ya bima nchini

Dar es Salaam. Katika kuadhimisha kuelekea Siku ya Bima, wadau wa sekta ya bima nchini wameendelea kutumia majukwaa ya elimu kwa vitendo kuwafikia vijana, hususan wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vikuu, kupitia mashindano ya mjadala maarufu kama ‘Bima Debate’ yaliyojikita katika kuelimisha na kuhamasisha uelewa wa sekta hiyo.

Mashindano hayo yamewakutanisha wanafunzi kutoka shule mbalimbali za sekondari na taasisi za elimu ya juu, ambapo walipata nafasi ya kujadili kwa kina masuala yanayohusu umuhimu wa bima katika maisha ya kila siku, mchango wake katika uchumi, pamoja na changamoto zinazoikabili sekta hiyo kutokana na uelewa mdogo wa wananchi.

Akizungumza katika hafla ya mashindano hayo, Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Mashariki, Zakaria Muyengi, ambaye pia alikuwa Jaji Mkuu wa mjadala huo na mgeni rasmi, amesema mashindano hayo yana lengo la kujenga msingi imara wa uelewa kwa wanafunzi kuhusu sekta ya bima wakiwa bado shuleni.

Amesema kuwa elimu hiyo ya mapema inawasaidia vijana kutambua umuhimu wa bima na namna inavyoweza kulinda maisha na mali, hivyo kuwaepusha na kuwa wageni wa sekta hiyo wanapofikia hatua za utu uzima.

“Lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wanapata uelewa wa kina kuhusu bima mapema iwezekanavyo, ili wanapokua watu wazima wawe tayari kutumia na kushiriki kikamilifu katika sekta hii inayokua kwa kasi nchini,” amesema Muyengi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa maandalizi ya mashindano hayo, Esther Mwamengo, amesema tukio hilo limebuniwa mahsusi kuwajengea wanafunzi uelewa wa mapema kuhusu huduma za bima, sambamba na kuondoa hofu na dhana potofu zilizozoeleka katika jamii kuhusu sekta hiyo.

Amesema changamoto kubwa inayokwamisha ukuaji wa sekta ya bima nchini ni ukosefu wa elimu kwa wananchi, hali inayochangia baadhi ya watu kutoielewa vyema au kutoitumia ipasavyo huduma hizo muhimu.

Mwamengo ameongeza kuwa wanafunzi waliopata elimu kupitia mashindano hayo wanatarajiwa kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha matumizi ya bima katika familia zao na jamii kwa ujumla, hatua ambayo itasaidia kukuza uelewa na ushiriki mpana zaidi wa wananchi katika sekta hiyo muhimu ya kiuchumi.

Mashindano hayo yameelezwa kuwa sehemu ya mikakati ya wadau wa bima nchini ya kuimarisha uelewa wa umma, hususan miongoni mwa vijana, ambao ndio nguvu kazi ya taifa la kesho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *