WHO yatangaza tahadhari kimataifa, Ebola ikisambaa Afrika MasharikiWHO yatangaza tahadhari kimataifa, Ebola ikisambaa Afrika Mashariki

Dar es Salaam. Hofu ya mlipuko wa Ebola imeongezeka barani Afrika baada ya ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya ‘Bundibugyo’ kusambaa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) hadi Uganda, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likitangaza hali ya dharura ya afya ya umma ya kimataifa.

WHO imetoa tamko hilo jana Jumapili Mei 17, 2026 baada ya kuthibitishwa kwa wagonjwa wapya nchini Uganda waliotokea Congo, hali inayozua wasiwasi wa kusambaa zaidi kwa ugonjwa huo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kwa mujibu wa WHO, hadi Mei 16, jumla ya wagonjwa wanane waliothibitishwa maabara na wagonjwa 246 wanaoshukiwa kuwa na Ebola walikuwa wameripotiwa katika Mkoa wa Ituri, mashariki mwa DRC.

Watu 80 wanaodaiwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo pia wameripotiwa.

Wakati huohuo, Uganda imethibitisha wagonjwa wawili wa Ebola mjini Kampala, ambapo mmoja ameripotiwa kufariki dunia. Wagonjwa hao walikuwa wametokea DRC, jambo lililothibitisha rasmi kusambaa kwa ugonjwa huo kuvuka mipaka ya kimataifa.

WHO imeeleza kuna uwezekano idadi halisi ya maambukizi kuwa kubwa zaidi kuliko inayoripotiwa sasa kutokana na mazingira magumu ya kiusalama mashariki mwa Congo, uhamaji mkubwa wa wananchi na uwepo wa vituo vingi vya afya visivyosajiliwa.

“Dalili zote zinaonyesha huu unaweza kuwa mlipuko mkubwa zaidi kuliko unaoonekana sasa,” imeeleza sehemu ya taarifa ya WHO.

Tofauti na aina nyingine ya Ebola ya Zaire, WHO imesema kwa sasa hakuna chanjo wala dawa maalumu zilizoidhinishwa kwa virusi vya Bundibugyo, hali inayoongeza hatari ya ugonjwa huo kuendelea kusambaa.

Mlipuko huo umeibua kumbukumbu za janga kubwa la Ebola lililotokea katika majimbo ya North Kivu na Ituri mwaka 2018 hadi 2019 ambapo maelfu ya watu waliambukizwa na wengine kupoteza maisha.

WHO imezitaka nchi zote zinazopakana na DRC kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa wagonjwa, uchunguzi wa maabara na udhibiti wa maambukizi katika vituo vya afya.

Shirika hilo limeonya kuwa wafanyakazi wa afya wapo katika hatari kubwa zaidi, ambapo wanne wameshafariki dunia mpaka sasa  katika maeneo yaliyoathirika, hali inayodokeza uwezekano wa maambukizi ndani ya hospitali.

Aidha, WHO imezitaka nchi kuhakikisha wagonjwa wanaotiliwa shaka wanatengwa mapema, kufuatilia watu waliokutana nao na kuimarisha elimu kwa jamii kuhusu dalili za Ebola na namna ya kujikinga.

Miongoni mwa hatua zilizopendekezwa ni uchunguzi wa afya mipakani, viwanja vya ndege na bandari, pamoja na kuzuia safari za kimataifa kwa watu waliothibitishwa au wanaoshukiwa kuwa na Ebola hadi watakapothibitishwa kuwa salama.

Hata hivyo, WHO imeonya dhidi ya kufungwa kwa mipaka au kusitishwa kwa biashara na safari kati ya nchi na nchi, ikisema hatua hizo mara nyingi huchochea matumizi ya njia zisizo rasmi za mipakani ambazo ni vigumu kudhibiti.

“Hatua za kufunga mipaka hazina msingi wa kisayansi na zinaweza kuongeza hatari ya maambukizi,” WHO imeeleza.

Katika tahadhari yake, WHO imezitaka nchi zilizo katika hatari kuandaa haraka mifumo ya kukabiliana na Ebola, ikiwa ni pamoja na kuunda timu za dharura, kuandaa maeneo ya kutolea matibabu maalumu na kuhakikisha vifaa kinga kwa wahudumu wa afya vinapatikana vya kutosha.

Pia imeshauri kuahirishwa kwa mikusanyiko mikubwa katika maeneo yenye maambukizi hadi ugonjwa utakapodhibitiwa.

Kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki, tahadhari hiyo inakuja wakati ukanda huo ukiwa na mwingiliano mkubwa wa biashara, usafiri na watu kati ya nchi jirani, jambo linaloongeza umuhimu wa hatua za mapema za kudhibiti maambukizi.

Dalili za Ebola ni pamoja na homa kali ya ghafla, uchovu kupitiliza, kutokwa damu, maumivu ya misuli, kutapika na kuharisha. Ugonjwa huo huenea kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa au aliyefariki kutokana na Ebola.

WHO imeahidi kuendelea kushirikiana na serikali za DRC na Uganda pamoja na wadau wa afya duniani kuhakikisha mlipuko huo unadhibitiwa kabla haujasambaa zaidi katika ukanda wa Afrika na duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *