Dar es Salaam. Licha ya kusifika na wengi kwa uandishi mzuri na kutoa nyimbo kali tena mfululizo, bado kuna ndoto za mafanikio mapya zinazomnyima usingizi mwanamuziki wa Bongofleva, Marioo kutokea Bad Nation Label.
Marioo, mkali wa kibao cha Naogopa (2022), moja ya ndoto hizo ni kutengeneza wimbo mwingine atakaofanya vizuri kama ule uitwao Nairobi (2024), jina la mji mkuu wa Kenya.
Nairobi ni wimbo namba nne kutokea katika albamu yake ya pili, The God Son (2024), huku akimshirikisha mwimbaji wa Kenya, Bien kutokea kundi la Sauti Sol ambalo lilianzishwa mwaka 2005.
Tunapata picha ya jinsi Marioo anavyosaka wimbo mwingine mkubwa wa aina hiyo kufuatia ujio wa Extended Playlist (EP) mpya na ya kwanza kuachia, MMMCXII (2026).
Wimbo wa kwanza kuachiwa katika EP hiyo unaitwa Mombasa, mji wa pwani uliopo kusini mashariki mwa Kenya kandokando ya bahari ya Hindi.
Hivyo Marioo baada ya kuona wimbo alioupa jina la Nairobi umefanya vizuri, basi awamu hii kaamua kutoa wimbo mwingine wenye jina la mji wa Kenya, nao ni Mombasa, ambao kwa sasa unafanya vizuri.
Hii ni ndoto unayomtesa Marioo kwani wimbo wa Nairobi ameweka rekodi ambazo hakuwahi kuzifikia tangu alipotoka kimuziki na wimbo wake, Dar Kugumu (2018) uliotayarishwa na Abbah.
Kwa muktadha huo, sasa ni wazi kuwa anataka kuzipata tena rekodi hizo kupitia Mombasa, wimbo anaoelezea jinsi anavyoyakumbuka mapenzi aliyowahi kuyapata huko kwao Mombasa (katumia lugha ya sanaa).
Je, kwanini Mombasa? Ikumbukwe muda mfupi baada ya wimbo wa Nairobi kuanza kufanya vizuri, Marioo alipata nafasi ya kutumbuiza katika hafla ya tuzo za Trace 2024 zilizofanyika Zanzibar, ambapo alishirikiana na Bien.
Ngoma hiyo iliendelea kufanya vizuri katika majukwaa ya kidijitali (digital streaming), mathalani video ilishika namba mbili katika orodha ya nyimbo za Bongofleva zilizotazamwa zaidi YouTube 2025, ikiwa imetanguliwa na ‘Pawa’ yake Mbosso.
Hadi sasa video ya wimbo ‘Nairobi’ imeshatazamwa mara milioni 54 ikiwa ni mwaka mmoja na miezi mitatu tangu kuachiwa kwake, ukiwa ni mradi wake wa kwanza kufikia namba hizo ndani ya muda huo.
Nairobi inashika nafasi ya pili katika orodha ya video zake zilizofanyika vizuri katika mtandao huo kwa muda wote, ikiwa imetanguliwa na ile ya kolabo yake na Harmonize, Naogopa (2022) iliyoachiwa miaka minne iliyopita.
Haikushia hapo, Nairobi ulikuwa miongoni mwa nyimbo zilizoingia katika mchakato wa kupata kazi chache kwa ajili ya tuzo za 68 za Grammy 2026 ambazo zilitolewa Marekani hapo Februari Mosi. Huo ulikuwa ni wimbo wake wa kwanza kufanya hivyo ambapo alijitosa kipengele cha ‘Best African Music Performance’ kilichoanza rasmi mwaka 2023, kikiwa ni maalum kwa ajili ya muziki kutokea Afrika.
Lakini haukufanikiwa kuchaguliwa badala yake waliopata nafasi hiyo ni Burna Boy (Love), Davido (With You), Eddy Kenzo (Hope & Love), Ayra Starr (Gimme Dat) na Tyla (Push 2 Start) aliyeibuka mshindi. Kwa hiyo Marioo anapokuja na wimbo unaoitwa Mombasa, ni kwamba tayari ana kumbukumbu nzuri ya wimbo alioupa mji wa Kenya (Nairobi) na ukafanya vizuri.
Katika mazingira kama hayo, kwa msanii anayeijua na kuijali biashara yake ya muziki ni lazima atataka tena kupitia njia ile ile ili kupata matokeo sawa na mwanzo, na hii ni ndoto mpya anayotaka kuitimiza. Hata hivyo, hii imekuwa kama tabia ya Marioo, mathalani ukichunguza kwa umakini, hata majina ya albamu zake zote mbili ni kama yanataka kufanana au muktadha wake ni mmoja.
Albamu yake kwanza iliyoachiwa Desemba 2022, aliipa jina la ‘The Kid You Know’, akilenga kujitambulisha au kutaka kutambulika yeye ni kijana mwenye uwezo gani katika huu muziki. Na albamu yake pili iliyoachiwa Novemba 2024 akaipa jina la ‘The God Son’, awamu hii akijitambulisha kama ‘kijana wa Mungu’ katika upambanaji wake.
Kingine albamu zote majina yake ni ya Kiingereza, na zote zimeanza na neno “The”, vilevile zote zimeachiwa mwishoni mwa mwaka ya kwanza Desemba, ya pili Novemba. Ni wazi kuwa Marioo alitaka hiyo ya pili kubeba picha ya ile ya kwanza ambayo ilipokelewa vizuri hadi kuchaguliwa kuwania Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) katika kipengele cha Albamu Bora ya Mwaka.
Jina la Marioo liliibuka baada ya kuurudia wimbo wa Lameck Ditto, Moyo Sukuma Damu (2016) ambao ulimvutia mtayarishaji Emma The Boy na kumkaribisha THT. Miaka miwili baadaye akatoka rasmi kimziki, na sasa akiwa ameshinda tuzo tano za TMA.
