Vikao vya madiwani vyaendelea kuwaumiza wabungeVikao vya madiwani vyaendelea kuwaumiza wabunge

Dodoma. Malalamiko ya wabunge kuhusu ratiba ya vikao vya madiwani kwa halmashauri za majiji, manispaa na miji bado ni mzigo mzito na sasa wanaomba ziandikwe barua rasmi za maelekezo kwa wakurugenzi.

Swali hilo limeshaulizwa mara ya tatu sasa katika mkutano wa Bunge unaoendelea.

Mara mbili limeulizwa kwenye maswali ya kawaida na mara moja limeulizwa katika maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba.

Katika majibu yake kwa wabunge, Waziri Mkuu aliagiza Wakurugenzi kuwasiliana na wabunge katika maandalizi ya vikao vya madiwani lakini kwa sehemu akata vifanyike siku za mapumziko ikiwemo jumamosi.

Leo Jumanne Mei 19, 2026 mbunge wa Kinondoni (CCM) Tarimba Abbas ameomba Serikali ibadili mpango wa kutoa maagizo badala yake itume waraka maalumu kwa wakurugenzi ili wanapoandaa vikao vyao washirikishe wabunge.

“Je Serikali haioni ni wakati sasa badala ya kutoa maagizo ambayo hayatekelezeki, itume waraka maalumu ili vikao vya halmashauri vinapoandaliwa viwe vinawahusisha waheshimiwa wabunge bila kuathiri mipango ya halmashauri,” ameuliza Abbas.

Katika swali la msingi, mbunge huyo ameuliza kuna mpango gani wa kuondoa mgongano wa vikao vya Bunge na halmashauri za majiji, manispaa na miji ili wabunge washiriki.

Akijibu maswali hayo kwa pamoja, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi, Dk Festo Dugange amesema Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa maelekezo kwa halmashauri ili kuhakikisha kwa kiwango kikubwa ratiba za vikao vya halmashauri hazigongani na ratiba za vikao vya Bunge.

Naibu Waziri amesema halmashauri zilielekezwa kuzingatia kalenda ya shughuli za Bunge wakati wa kuandaa kalenda zao za vikao vya mwaka husika ili kutoa fursa kwa wabunge, ambao ni wajumbe wa mikutano hiyo kushiriki kikamilifu.

“Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi itaendelea kuzisimamia halmashauri kuhakikisha zinaandaa ratiba ya vikao kwa mwaka 2026/27 kwa kuzingatia ratiba za vikao vya bunge kwa kadri inavyowezekana,”amesema Dk Dugange.

 Amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuwasiliana na wabunge wakati wa kupanga tarehe za vikao vya kamati na mabaraza ya madiwani ili kuona namna viongozi hao wanaweza kushiriki vikao hivyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *