Wajasiriamali 320 wa chakula Dodoma wapatiwa majiko banifuWajasiriamali 320 wa chakula Dodoma wapatiwa majiko banifu

Dar es Salaam. Wajasiriamali 320 wa chakula wamepatiwa mafunzo ya biashara pamoja na majiko banifu yatakayowasaidia kupunguza gharama za uendeshaji, kuboresha usalama wa mazingira ya kazi na kuimarisha biashara zao.

Hilo limefanyika kupitia programu ya Stanbic Biashara Incubator, kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) pamoja na Said Salim Bakhresa (SSB), ambayo imeendelea na juhudi za kuwawezesha wanawake na vijana wajasiriamali kwa kupeleka programu ya Rise Mama Lishe mkoani Dodoma.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo mjini Dodoma, Mkuu wa Stanbic Biashara Incubator, Kai Mollel amesema mama na mabalishe wana mchango mkubwa katika uchumi wa jamii na maisha ya kila siku ya wananchi.

“Kupitia Rise Mama Lishe, tunalenga kuwasaidia kutoka katika biashara za kujikimu na kuwa biashara imara, salama na zenye mpangilio bora zaidi,” amesema.

Amesema jiko banifu ni zaidi ya kifaa cha kupikia kwani linapunguza gharama za nishati, kupunguza moshi, kuboresha usalama wa mazingira ya kazi na kuweka msingi bora wa ukuaji wa biashara.

Meneja Miradi kutoka GIZ, Lisa Zschunke amesema programu hiyo inaonyesha namna ukuaji wa biashara na matumizi ya nishati safi ya kupikia, vinavyoweza kwenda pamoja katika kuboresha maisha ya wajasiriamali.

“Kupitia mafunzo ya biashara pamoja na majiko banifu, tunachangia mazingira salama zaidi ya kazi, usimamizi bora wa gharama na uimara wa biashara ndogo,” amesema.

Mafunzo yanayotolewa kupitia programu hiyo yanajumuisha usimamizi wa biashara, upangaji wa bei, huduma kwa wateja, usafi na usalama wa chakula pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika biashara.

Programu hiyo ni mwendelezo wa mpango wa kitaifa uliozinduliwa Dar es Salaam mwezi Novemba 2025 na tayari umefanyika katika mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Awamu ya mwaka 2025 hadi 2026, Stanbic Bank na GIZ wanalenga kuwawezesha zaidi ya wajasiriamali 2,000 kwa kuwapatia mafunzo ya biashara, usimamizi wa fedha na matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *