
Dar es Salaam. Kampuni ya Connect Space imetangaza uzinduzi wa Globe Connect 24/7, ubia mpya kati yake na kampuni ya kimataifa ya ajira za sekta ya madini, Globe 24/7, ukiwa na lengo la kuimarisha huduma za ajira katika sekta hiyo Afrika Mashariki.
Ubia huo, wenye makao yake nchini Tanzania, umetajwa kuwa kitovu cha kwanza maalum cha huduma za ajira kwa sekta ya madini katika ukanda wa Afrika Mashariki, ukilenga kusaidia shughuli za migodi pamoja na kukuza vipaji vya ndani.
Kupitia ushirikiano huo, kampuni hizo mbili zitachanganya uelewa wa soko la ndani na uzoefu wa kimataifa katika sekta ya madini ili kutoa huduma zinazolenga mahitaji halisi ya waajiri na wataalamu wa sekta hiyo.
Globe Connect 24/7 itafanya kazi kwa mfumo wa kuunganisha wataalamu wa Kitanzania na fursa za kazi katika miradi ya madini duniani, sambamba na kusaidia kampuni za kimataifa zinazofanya shughuli zake Afrika Mashariki kupata wataalamu wenye ujuzi kutoka ndani ya nchi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mfumo huo unalenga kuhakikisha uwezo wa ndani unaenda sambamba na uzoefu wa kimataifa ili kukidhi mahitaji ya sasa ya nguvu kazi katika sekta ya madini.
Aidha, kampuni za madini zinazoingia au kupanua shughuli zake katika ukanda huo zinatarajiwa kunufaika na huduma za ajira zinazozingatia sheria za ndani, mazingira ya kazi pamoja na muktadha wa kijamii na kiutamaduni.
Kwa upande wa wataalamu wa Kitanzania, ushirikiano huo umeelezwa kufungua fursa za ajira zenye uwazi na kuzingatia maadili ya kimataifa ya sekta ya madini bila waombaji kazi kutozwa ada yoyote.
Mwanzilishi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Connect Space, Judith Godwin, amesema uzinduzi huo ni hatua muhimu katika kupanua uwezo wa kampuni hiyo kwenye huduma za ajira nchini Tanzania.
“Madini ni sekta muhimu ya ukuaji Afrika Mashariki. Globe Connect 24/7 inatuwezesha kutumia utaalamu wetu wa ndani kushughulikia changamoto za nguvu kazi katika sekta ya madini, huku tukihakikisha waendeshaji wa kimataifa na wataalamu wa ndani wanapata msaada kupitia mfumo wa ajira wenye maadili, uwazi na uthabiti,” amesema.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Globe 24/7, Alastair Fisher, amesema ushirikiano huo umejengwa katika msingi wa maadili ya pamoja na maono ya muda mrefu.
“Afrika Mashariki inaendelea kujitokeza kama eneo muhimu kimkakati katika sekta ya madini. Globe Connect 24/7 inaongeza uwezo wetu wa kusaidia wateja moja kwa moja huku tukichangia maendeleo endelevu ya nguvu kazi kupitia huduma za ajira zinazotokana na uelewa wa ndani na kuungwa mkono kimataifa,” amesema.
Uzinduzi wa Globe Connect 24/7 unaongeza juhudi za Connect Space katika kutoa huduma za ajira zinazoweka watu mbele, huku ukilenga kuwawezesha wataalamu wa ndani na kuchangia maendeleo ya jamii kupitia sekta ya madini.
