Vifo vya Ebola vyafikia 131, maambukizi yakishika kasiVifo vya Ebola vyafikia 131, maambukizi yakishika kasi

Dar es Salaam. Hofu ya kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola imeongezeka katika ukanda wa Afrika Mashariki baada ya mamlaka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuthibitisha watu wasiopungua 131 wamefariki dunia kutokana na mlipuko mpya wa ugonjwa huo, huku zaidi ya 500 wakiambukizwa.

Ebola sasa inasambaa zaidi Congo, ambapo maeneo yaliyotajwa kugundulika kuwa na wagonjwa wapya ni pamoja na Nyakunde katika jimbo la Ituri, Butembo mkoani Kivu Kaskazini na jiji la Goma ambalo ni kitovu muhimu cha biashara na usafiri katika ukanda huo.

Akitoa taarifa hiyo, leo Jumanne, Mei 19, 2026 Msemaji wa Serikali ya DRC amesema maambukizi hayo sasa yameripotiwa katika maeneo mapya, jambo linaloongeza hofu ya kuenea kwa ugonjwa huo ndani na nje ya nchi hiyo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) tayari limetangaza mlipuko huo wa Ebola unaosababishwa na kirusi cha aina ya Bundibugyo kuwa ni dharura ya afya ya umma ya kimataifa.

Mbali na DRC, Uganda nayo imeripoti wagonjwa wawili waliothibitishwa na kifo kimoja, kwa mujibu wa Kituo cha Marekani cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC).

Katika hatua nyingine, daktari mmoja raia wa Marekani aliyekuwa akifanya kazi ya kimishionari nchini DRC amethibitishwa kuambukizwa Ebola na sasa anatarajiwa kuhamishiwa nchini Ujerumani kwa matibabu zaidi.

Kundi la kimishionari la Serge limemtaja daktari huyo kuwa ni Peter Stafford, huku mkewe Dk Rebekah Stafford akiwa miongoni mwa watu waliowekwa karantini baada ya kukutana na wagonjwa wa Ebola, ingawa bado hajaonyesha dalili za maambukizi.

Kwa mujibu wa CDC, raia kadhaa wa Marekani wanaofanya kazi DRC wameathirika au kukutana na watu wenye maambukizi ya Ebola, hali iliyosababisha nchi hiyo kuanza mpango wa kuwaondoa baadhi yao kwenda maeneo salama ya karantini.

Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa kundi hilo linaweza kupelekwa katika kituo cha kijeshi cha Marekani kilichopo Ujerumani, ingawa taarifa hiyo bado haijathibitishwa rasmi.

Kutokana na hali hiyo, Marekani imetoa tahadhari ya kiwango cha nne dhidi ya safari za kwenda DRC, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi cha onyo la usalama wa kiafya na usafiri.

CDC pia imetangaza hatua mbalimbali za kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini humo, ikiwamo kuongeza uchunguzi kwa wasafiri wanaotoka DRC, Uganda na Sudan Kusini.

Hatua hizo zinahusisha ufuatiliaji wa abiria viwanjani, kuongeza uwezo wa vipimo vya Ebola pamoja na kuimarisha maandalizi ya hospitali kwa ajili ya kukabiliana na wagonjwa watakaobainika.

Shirika la WHO limeonya kuwa mlipuko huo unaweza kuwa mkubwa zaidi kuliko idadi ya wagonjwa wanaoripotiwa sasa, hasa kutokana na uwezekano wa maambukizi kusambaa katika maeneo ya mipakani.

Mkurugenzi wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Jean Kaseya, amesema jamii zinapaswa kufuata maelekezo ya afya hasa katika mazishi ya watu waliofariki kutokana na Ebola.

WHO imezitaka DRC na Uganda kuimarisha uchunguzi katika maeneo ya mipakani ili kuzuia ugonjwa huo kuenea kwenda nchi nyingine jirani.

Nchi jirani za Rwanda na Tanzania tayari zimetangaza kuimarisha ukaguzi mpakani mwa DRC kama hatua ya tahadhari, huku Nigeria ikisema inaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mlipuko huo.

Mlipuko mkubwa zaidi wa Ebola kuwahi kutokea ulitokea Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 na 2016 ambapo zaidi ya watu 28,600 waliambukizwa na watu 11,325 kupoteza maisha katika nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia.

Ebola ni ugonjwa hatari unaosambazwa kwa kugusana na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa au aliyefariki kutokana na ugonjwa huo. Dalili zake ni pamoja na homa kali, kutapika, kuharisha, uchovu mkubwa na kutokwa damu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *