Matumaini, mashaka Tume uchunguzi wa jinai matukio ya Oktoba 29Matumaini, mashaka Tume uchunguzi wa jinai matukio ya Oktoba 29

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, ameunda Tume ya uchunguzi wa kijinai wa matukio ya ghasia ya wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29,2025, huku wadau wakionyesha matumaini na mashaka kwa wakati mmoja.

Wanaoonyesha matumaini, wanasema hiyo ndiyo tume iliyosubiriwa kwa hamu hasa ukizingatia itategua kitendawili cha nani alihusika kupanga, kuratibu na kutekeleza na nani awajibike au kuwajibishwa.

Kwa upande wa wanaoonyesha mashaka, wanasema muundo wake unahusisha wastaafu kutoka serikalini, hivyo huenda wasiwe huru kuamua na kupendekeza. Pia, wanasema kwa kuwa ripoti ya tume ya awali ilifichwa wanakosa matumaini kwa hii.

Uamuzi wa kuundwa kwa tume hiyo, ni utekelezaji wa mapendekezo ya tume ya uchunguzi wa matukio hayo iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Othman Chande, iliyotaka uchunguzi wa kijinai ufanywe na tume maalumu ya kijinai.

Katika pendekezo hilo, Jaji Chande alisema tume hiyo itakuwa na jukumu la kupeleleza na kufuatilia masuala mahsusi yanayohitaji upelelezi zaidi ili kushughulikia tuhuma zilizobainishwa katika taarifa ya Tume.

”Masuala hayo ni pamoja na kubaini wahusika wakuu wa ghasia, matukio tatanishi ya vifo na majeruhi, maiti ambazo hazijapatikana, na kupendekeza hatua za uwajibikaji,” alisema Aprili 23, mwaka huu alipokabidhi ripoti kwa Rais Samia.

Taarifa ya kuundwa kwa tume hiyo ya kijinai, imetolewa leo Jumatatu Mei 18, 2026 na kutiwa saini na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka.

Makamishna wa Tume

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Lila ameteuliwa kuwa Kamishna na Mwenyekiti wa tume hiyo.

Wengine walioteuliwa kuwa makamishna wa tume hiyo ni Jaji mstaafu Gad Mjemmas, Jaji mstaafu Awadh Bawazir na Jaji mstaafu Aishieli Sumari, wote walikuwa Mahakama Kuu.

Itakumbwa na utata

Akizungumzia tume hiyo, Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo, amesema uundwaji wa tume hiyo ni utekelezaji wa ahadi, ingawa itapitia utata kwa kuwa jamii imejenga picha kuwa Rais hapaswi kuunda tume kuhusu matukio ya Oktoba 29.

Ameeleza katika jamii kuna mitazamo ya wengi wakitaka kuundwe tume ya kimataifa kufanya uchunguzi wa matukio hayo, ikishirikiana na makundi mbalimbali.

Kwa msingi huo, amesema hata ikifanya kazi nzuri kiasi gani haitaliponya Taifa, kwa kuwa ripoti ya tume ya Jaji Chande haikuwekwa hadharani.

”Kufichwa ripoti hiyo hata hii ikiwatuhumu watu, hawakubali kuwa wanatuhumiwa kwa haki, inaweza ikalipasua zaidi Taifa. Tulianza na msingi mbovu baada ya kuzuia ripoti hiyo kuwa hadharani,” amesema.

Amesema hata ingeundwa kwa namna gani kwa sasa baadhi ya watu hawataikubali tume, kwa kuwa Taifa linapitia katika kipindi cha kutoaminiana.

”Ilitakiwa Serikali ikiri kuwa watu waliuawa, waliuawa na askari kwa silaha za moto kisha uchunguzi ulenge ilikuwaje katika mauaji hayo. Bila hivyo, kuwatuhumu watu kutaibua tatizo kubwa zaidi,” amedai.

Ametaka Serikali na wadau wajikite kwenye kujenga kuaminiana kwanza bila kuibua mpasuko mbaya zaidi.

Matumaini, mashaka

Kwa upande wake, kiongozi wa kiroho, Askofu William Mwamalanga, amesema hiyo ndiyo tume iliyosubiriwa na wengi kwa kuwa itategua kutendawili cha wahusika na watakavyowajibishwa.

“Mimi ninaiona tume hii kuwa ndiyo iliyotakiwa kuundwa mara tu baada ya matukio hayo kutokea. Matukio yaliyotokea ni ya kijinai kabisa hivyo tulitegemea tuione tume ya aina hii tangu mwanzo,” amesema.

Lakini, ameshuku muundo wake umeegemea zaidi kwa wastaafu wa Serikali, akipendekeza ingehusisha watu kutoka makundi mengine.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga, amesema kuundwa kwa tume nyingine kunaongeza gharama kwa Serikali na kuchelewesha hatima ya jambo hilo linalobeba hisia za wengi.

“Kuendelea kuunda tume kunapoteza rasilimali na kupoteza muda kwani Tume ya Jaji Chande ndiyo iliyotakiwa kukusanya taarifa zote hizi na siyo kuishia nusu na kuunda tume nyingine nayo ije na mapendekezo yake,” amesema.

Naye, ameshuku wajumbe, akisema wanatokana na utumishi wa serikalini hivyo anahofia kuwa huenda wasiwe na nguvu ya kuwaibua na kupendekeza wanaopaswa kuwajibishwa.

Jaji Lila ni nani?

Jaji Lila aliapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Juni 10, 2016, akitoka kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu kwa miaka mitatu tangu Juni 2014.

Kabla ya kuwa Jaji Kiongozi, Lila alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu Idara ya Masjala akishughulikia uanzishwaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Ilala.

Jaji Lila, alianza kuhudumu katika muhimili wa mahakama mwaka 1995, kwa nafasi mbalimbali.

Mjemmas, alistaafu utumishi ndani ya mahakama miaka minane iliyopita, akiwa na wadhifa wa Jaji wa Mahakama Kuu, aliokuwa nao tangu   2006 alipoteuliwa kwa mara ya kwanza.

Katika muhimili wa mahakama, amewahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi Dar es Salaam, kadhalika Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.

Mbali na nyadhifa ndani ya mahakama, Jaji mstaafu mjemmas amewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Mwenyekiti wa Mahakama ya Rufaa ya Mashauri ya Kikodi (TRAT), wadhifa aliohudumu hadi 2025.

Jaji Sumari, naye ametumikia mahakama kwa zaidi ya miongo mitatu. Amekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Jaji Mfawidhi katika Kanda za Mwanza na Moshi.

Pia, amewahi kuwa Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Lushoto mkoani Tanga.

Awadh Bawazir

Jaji mstaafu Bawazir naye amehudumu katika muhimili wa mahakama kwa zaidi ya miongo mitatu, kabla ya kustaafu na alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Kwa sasa ni Mwenyekiti wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *